• HABARI MPYA

  Saturday, March 18, 2017

  YANGA ‘FULL KUJIAMINI’, MSUVA ASEMA WATACHEZA BILA PRESHA LUSAKA

  Na Jeff Leah, LUSAKA
  WINGA wa Yanga, Simon Happygod Msuva amesema kwamba wana matumaini ya kucheza vizuri bila presha leo na kushinda ugenini dhidi ya wenyeji Zanaco katika mchezo wa marudiano hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Yanga watakuwa wageni wa Zanaco jioni ya leo Uwanja wa Taifa wa Mashujaa, Lusaka kuanzia Saa 10:00 jioni wakilazimika kushinda kwa vyovyote baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 katika mchezo wa kwanza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi iliyopita.
  Na akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online mjini hapa jana, Msuva alisema kwamba wanatarajia kuendeleza utamaduni wao wa kucheza vizuri na kupata matokeo mazuri kwenye viwanja ugenini.
  “Tunatarajia kucheza kwa utulivu bila presha tofauti na nyumbani na kupata matokeo mazuri. Kikubwa tunafahamu tunaingia katika mchezo mgumu, lakini tayari tuna uzoefu wa mashindano makubwa kama haya, tunasimamia kwenye dhamira yetu,”alisema.
  Kwa upande wake, beki Mtogo Vincent Bossou alisema kwamba utakuwa mchezo mgumu, lakini wamejipanga kupigania matokeo mazuri ili wafuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
  “Tulifanya makosa kwenye mchezo wa kwanza wakapata sare, lakini hatutafanya makosa tena kwenye mchezo huu. Tutajitahidi sana tusiruhusu bao,”alisema. 
  Kocha Mkuu, George Lwandamina alikuwa ‘bize’ zaidi kufikiria mchezo huo, kiasi cha kutokuwa tayari kuzungumza na Waandishi wa Habari, badala yake akazungumza Msaidizi wake, Juma Mwambusi.
  Mwambusi alisikitikia kuingia kwenye mchezo huo bila washambuliaji wake wote wawili tegemeo, Donald Ngoma na Amissi Tambwe.
  Mrundi Tambwe na Mzimbabwe Ngoma hawakusafiri na Yanga kwa ajili ya mchezo huu kutokana na kuwa mejeruhi. Tambwe hakucheza kabisa mechi ya kwanza Dar es Salaam, wakati Ngoma alijaribu kucheza kwa mara ya kwanza tangu Januari, lakini hakumaliza hata kipindi cha kwanza akatonesha goti na kutoka.
  Wachezaji wengine ambao hawajasafiri na timu ni kipa wa tatu, Beno Kakolanya, beki Pato Ngonyani, kiungo Yussuf Mhilu na washambuliaji wengine wawili, wote wazawa, Malimi Busungu na Matheo Anthony ambao pia ni wagonjwa. 
  Wachezaji waliopo na timu Lusaka ni makipa; Deogratius Munishi ‘Dida’ na Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki ni Oscar Joshua, Mwinyi Hajji Mngwali, Hassan Kessy, Juma Abdul, Vincent Bossou, Andrew Vincent ‘Dante’, Kevin Yondan na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
  Viungo ni Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Justine Zulu, Said Juma ‘Makapu’, Juma Mahadhi, Simon Msuva, Geoffrey Mwashiuya, Obrey Chirwa na Emanuel Martin. 
  Na bila shaka Lwandamina atawaanzisha; Dida, Kessy, Mwinyi, Cannnavaro, Bossou, Yondan, Kaseke, Kamusoko, Chirwa, Msuva na Mwashiuya. Kila la heri Yanga SC. Mungu ibariki Yanga, Mungu ibariki Tanzania. Amin.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA ‘FULL KUJIAMINI’, MSUVA ASEMA WATACHEZA BILA PRESHA LUSAKA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top