• HABARI MPYA

  Sunday, March 19, 2017

  SIMBA NA MADINI LEO KAZI IPO SHEIKH AMRI ABEID

  Na Mwandishi Wetu, ARUSHA
  VINARA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Simba SC leo wanahamishia mawindo yao katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup (ASFC) watakapomenyana na wenyeji, Madini FC Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
  Mchezo huo wa Robo Fainali unatarajiwa kuanza Saa 10:00 jioni na utakuwa wa pili baada ya jana Mbao FC ya Mwanza kuwatoa Kagera Sugar kwa ushindi wa mabao 2-1 Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
  Simba SC inayofundishwa na Mcameroon, Joseph Marius Omog itaingia kwenye mchezo wa leo ikiwa na kumbukumbu ya kufanya vizuri katika Ligi Kuu, ambako inaongoza dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga na washindi wa pili wa msimu ulioipita, Azam FC.
  Hiyo inatarajiwa kuwa kama chachu ya kufanya vizuri pia kwenye michuano hiyo ya kusaka mwakilishi wa nchi kwenye Kombe la Shirikisho la Soka Afrika mwakani.
  Simba leo itaendelea kumkosa beki wake wa kati, Mzimbabwe Method Mwanjali, lakini hakuna shaka Omog ataendelea kuwatumia Abdi Banda na Novaty Lufunga, ingawa anaye pia Mganda, Juuko Murshid.
  Katika mchezo wa hatua ya 16 Bora dhidi ya Polisi Dar ee Salaam, Omog alimpanga kipa wa kwanza, Mghana Daniel Agyei – lakini leo haitakuwa ajabu akimuweka langoni kipa wa pili mwenye uwezo mkubwa na kipaji, Peter Manyika.
  Kikosi hakitarajiwi kuwa na mabadiliko makubwa kutoka kile kikosi cha kawaida cha kwanza cha timu, kwani hata Madini FC ya Daraja la Kwanza si timu ya kubeza ikiwa imetoka kuitoa timu ya Ligi Kuu, JKT Ruvu.
  Janvier Bokungu anaweza kucheza beki ya kulia, kushoto kama kawaida Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, katikati Banda na Lufunga, viungo wanaweza kuanza Jonas Mkude na Said Ndemla katikati, pembeni kulia Shiza Kichuya na kushoto Ibrahim Hajib wakati katikati anaweza kuwpanga Juma Luizio na Mrundi, Laudit Mavugo.
  Katika benchi wanaweza kuwapo Agyei, Hamad Juma, Vincent Costa, Juuko Murshid, Muzamil Yassin, Mohammed Ibrahim, Pastory Athanas, James Kotei na Jamal Mnyate.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA NA MADINI LEO KAZI IPO SHEIKH AMRI ABEID Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top