• HABARI MPYA

  Monday, March 20, 2017

  JKT OLJORO YABISHA HODI DARAJA LA KWANZA, YAIPIGA 1-0 COSMO

  Na Clement Shari, ARUSHA
  TIMU ya JKT Oljoro ya mjini Arusha imejiweka katika mazingira mazuri ya kurejea Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara msimu ujao mara baada ya ushindi wa 1-0 jioni ya leo dhidi ya Cosmopolitan ya Dar es Salaam Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
  Asante nyingi kwa mfungaji wa bao hilo la JKT Oljoro, beki Yussuph Machogote aliyefunga dakika ya 15 kwa kichwa kufuatia kona iliyopigwa na Nahodha Salehe Hussein.
  Kwa ushindi huo, JKT Oljoro wanafikishaa pointi saba baada ya kucheza michezo minne, wakishinda miwili, kutoka sare mmoja na kupoteza mchezo mmoja.
  JKT Oljoro ilimaliza pungufu mchezo huo, baada ya refa Meshack Suda kutoka Singida kumtoa kwa kadi nyekundu beki Omary Mamba dakika ya 73 kwa kumchezea rafu mshambuliaji wa Cosmo, Salum Hami.
  JKT Oljoro imejiweka katika mazingira mazuri ya kurejea Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara

  Kocha wa Cosmo, Salum Kulambatalu alisema kushindwa kwa vijana wake kumetokana na maamuzi mabovu ya marefa na pia wachezaji wa JKT Oljoro walikuwa wanajiangusha mara kwa mara kiasi cha kuharibu ladha ya  mchezo.
  Kwa upande wake, kocha wa Oljoro, Emanuel Masawe aliwapongeza vijana wake kwa ushindi walioupata na kwamba  hivi sasa wanaelekeza nguvu zao katika michezo miwili iliyobakia.
  Michezo maalum ya kuwania kufuzu Ligi Daraja la Kwanza inashirikisha jumla ya timu nne  
  zilizoongoza katika hatua ya makundi ya Ligi Daraja la Pili Tanzania Bara na mbali na JKT Oljoro na Cosmo, timu nyingine mbili ni Mawenzi ya Morogoro na Transit ya Shinyanga.
  Timu tatu zitakazofanya vizuri zitapanda Daraja la Kwanza msimu ujao, wakati timu moja itarejea Daraja la Pili.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: JKT OLJORO YABISHA HODI DARAJA LA KWANZA, YAIPIGA 1-0 COSMO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top