• HABARI MPYA

  Saturday, March 04, 2017

  CHIRWA AFUTIWA KADI NYEKUNDU, KESHO KUICHEZEA YANGA DHIDI YA MTIBWA

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI Obrey Chirwa yuko huru kuichezea Yanga kesho katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar mjini Morogoro.
  Hiyo inafuatiwa mchezaji huyo wa Zambia kufutiwa kadi nyekundu aliyoonyeshwa kwenye mchezo uliopita wa Ligi Kuu dhidi ya Ruvu Shooting ya Pwani, Jumatano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Habari kutoka Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambazo Bin Zubeiry Sports – Online imezipata zimesema kwamba kadi hiyo imefutwa baada ya kubainika mchezaji huyo wa zamani wa FC Platinums ya Zimbabwe alionyeshwa kimakosa.
  Obrey Chirwa yuko huru kuichezea Yanga kesho dhidi ya Mtibwa Sugar mjini Morogoro 

  “Kadi ya Chirwa imefutwa kufuatia Yanga kuwasilisha malalamiko dhidi ya mwamuzi Ahmada Simba wa Kagera. Na Bodi imejiridhisha kwamba mwamuzi huyo alipitiwa, hivyo kuifuta kadi hiyo na sasa yuko huru kuichezea timu yake katika mchezo ujao,”amesema Ofisa mmoja wa Bodi ambaye hakutaka kutajwa jina.
  Chirwa alionyeshwa kadi mbili za njano za utata ndani ya dakika mbili na kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 45 katika mchezo ambao Yanga ilishinda 2-0.
  Alionyeshwa kadi ya kwanza ya njano dakika ya 44 baada ya kuifungia Yanga bao safi ambalo lingekuwa la pili kwa kichwa akimalizia krosi ya beki wa kulia, Hassan Kessy, lakini refa Ahmada Simba wa Kagera akalikataa na kumuonyesha kadi ya njano.
  Na Mzambia huyo akaonyeshwa kadi ya pili njano dakika ya 45 baada ya kuudunda mpira chini na kutolewa kwa kadi nyekundu.
  Mapema dakika ya 31 Chirwa alifumua shuti kali langoni mwa Ruvu, ambalo lilimbabatiza mkononi beki Damas Makwaiya na Simba akaamuru mkwaju wa penalti, uliotiwa nyavuni na Simon Msuva kuipatia Yanga bao la kwanza.
  Yanga ilipata bao lake la pili kupitia kwa Emmanuel Martin dakika ya nne ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika 90 za kawaida akimalizia kwa kichwa krosi ya Simon Msuva kutoka upande wa kulia.
  Yanga imeondoka leo Alfajiri Dar e Salaam kuelekea Morogoro tayari kwa mchezo huo dhidi ya Mtibwa Sugar.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: CHIRWA AFUTIWA KADI NYEKUNDU, KESHO KUICHEZEA YANGA DHIDI YA MTIBWA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top