• HABARI MPYA

  Wednesday, November 02, 2016

  SIMBA SC NA YANGA MAWINDONI LIGI KUU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM 
  MIAMBA ya soka nchini, Simba na Yanga inajitupa kwenye viwanja tofauti leo katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Mabingwa watetezi, Yanga watakuwa Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya kumenyana na wenyeji, Mbeya City wakati vinara wa msimu huu hadi sasa, Simba SC wapo Uwanja wa Kambarage Shinyanga kumenyana na wenye mji wao, Stand United.
  Kocha Mholanzi wa Yanga, Hans van der Pluijm alisema jana kwamba watapambana kwa bidii kushinda mchezo wa leo ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutetea ubingwa wao.
  Lakini Pluijm amesema wamekuwa wakipaniwa mno na wapinzani wao kiasi cha kuifanya kila mechi yao kuwa kama fainali. “Lakini kwa sababu tunajua. Sisi (benchi la Ufundi) na wachezaji wetu tumejipanga vya kutosha kuondoka na ushindi katika mchezo wa leo,”alisema.
  Kwa upande wake, kocha Mkuu wa Mbeya City, Mmalawi Kinnah Phiri alisema nao wameajindaa vizuri kukabiliana na Yanga leo.
  “Kweli mchezo na Yanga utakuwa mzuri kwa sababu timu zote zimeshinda michezo iliyopita, sisi tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunashinda, hatuna shaka yoyote kwa sababu timu zote zina mchezo sawa, jambo jema ni maandalizi tuliyoyafanya na sapoti ambayo tutaipata kutoka kwa mashabiki wetu, watu waje uwanjani na wajiandae kushangaa kile kitakachofanywa na timu yangu,” alisema.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Africans Lyon ya Dar es Salaam pia watakuwa wageni wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani, wakati JKT Ruvu watakuwa wageni wa Majimaji Uwanja wa Majimaji, Songea, Ndanda itawakaribisha Prisosn Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara naToto Africans itawakaribisha Azam Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.
  Ligi hiyo itaendelea Alhamisi kwa michezo miwili, Mwadui waakiikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Mwadui Complex huko Shinyanga na Mbao FC wakiwa wenyeji wa Kagera Sugar Uwanja wa CCM Kirumba, mjini Mwanza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC NA YANGA MAWINDONI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top