• HABARI MPYA

    Wednesday, November 02, 2016

    NI MAPEMA SIMBA SC KUJIONA MABINGWA, LIGI BADO MNO!

    ANGALAU sasa Evans Elieza Aveva, Rais wa klabu ya Simba anaweza kuwa anapata usingizi mnono, baada timu kuanza kupata matokeo mazuri.
    Aveva aliingia madarakani Simba SC Juni 29, mwaka 2014 kwa ushindi wa kishindo wa kura 1,455 dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Andrew Tupa, aliyepata kura 388.
    Na Aveva alipita kiulaini katika uchaguzi huo baada ya kuenguliwa mgombea aliyetarajiwa kuwa mpinzani wake mkuu, Michael Richard Wambura kwa tuhuma za kukiuka taratibu za uchaguzi.
    Aveva aliingia kwa pamoja na Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ aliyeshinda Umakamu wa Rais kwa kura 1,046 dhidi ya Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ aliyepata 412, Swedy Nkwabi 373 na Bundala Kabula aliyeambulia kura 25.
    Wajumbe wa Kamati ya Utendaji walioshinda ni Iddi Kajuna aliyepata kura 893, Said Tully (788), Collins Frisch (758), Ally Suru ( 627) na kwa upande wa mwanamke aliyeibuka kinara ni Jasmine Badour aliyepata kura 933 akiwashinda Asha Muhaji aliyepata kura 623 na Amina Poyo 330. 
    Timu hiyo ya uongozi mpya iliyoingia madarakani baada ya Alhaj Ismail Aden Rage kumaliza muda wake, imeshuhudia misimu miwili ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na mmoja wa Kombe la Shirikisho Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).
    Bahati mbaya katika misimu miwili ya Ligi Kuu walitupwa nje ya timu mbili za juu na msimu mmoja uliopita wa Kombe la ASFC walitolewa Nusu Fainali na Coastal Union ya Tanga iliyoshuka Daraja.
    Maana yake katika kipindi chote cha Aveva na timu yake kuwa madarakani, Simba haijapata nafasi ya kushiriki michuano ya Afrika, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.
    Kwa sababu hiyo wamekuwa wakitaniwa na mahasimu wao, Yanga kwamba wao ni wa kucheza michuano ya ‘mchangani’ hivyo kuwaita ‘Wa Matopeni’.
    Lakini pia uongozi umekuwa hauna raha mbele ya wanachama na mashabiki wake kutokana na matokeo hayo mabaya hususan katika kipindi ambacho mahasimu wao, Yanga SC wamekuwa wakifanya vizuri.
    Msimu uliopita, Simba SC ilikuwa ina mwanzo mzuri katika mashindano yote, kwani mbali na kwenda hadi Nusu Fainali ya Kombe la ASFC, pia walifikia kuongoza Ligi Kuu kwa pointi 11 zaidi dhidi ya Azam na Yanga.
    Haikuwa ajabu kwa kiwango hicho, aliyekuwa Kaimu kocha Mkuu wa Simba, Mganda Jackson Mayanja akaanza kutamba kwamba timu yake itatwaa ubingwa.
    Ulikuwa ni wakati ambao wapenzi wa Simba walipenda kuwasikia viongozi wao, kama Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe na Msemaji wa timu, Hajji Manara wakitamba kwenye vyombo vya Habari.
    Ni wakati ambao Aveva alianza kupata matumaini ya kuipa taji la kwanza klabu tangu achaguliwe kwa kishindo katika uchaguzi wa Juni 29, mwaka 2014.
    Lakini ajabu Simba SC ikapoteza mwelekeo ghafla na kuanza kufanya vibaya hadi kupitwa na Azam na Yanga kwenye Ligi Kuu na pia kutolewa na Coastal Union katika Kombe la ASFC.
    Na haya yote yalitokea baada ya klabu kupata nguvu ya fedha kiasi cha Sh. Milioni 600 za mauzo ya mshambuliaji Emmanuel Okwi klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia.
    Maana yake klabu ilikuwa haina shida ya kifedha, lakini ajabu mambo yalibadilika ghafla hadi kufikia kutolewa Kombe la ASFC na kupitwa na Azam na Yanga katika Ligi Kuu. Mwisho wa msimu, Yanga ilitwaa mataji yote na Azam ikawa ya pili Ligi Kuu na Kombe la ASFC.
    Ulikuwa msimu wa kuumiza kwa mashabiki wa Simba na tangu hapo wakaanza kulilia mabadiliko, wakitaka mfanyabiashara Mohamed ‘Mo’ Dewji anayetaka kununua asilimia 51 ya hisa za klabu apewe timu.
    Na hiyo ni kwa sababu wana Simba wanaamini klabu yao inazidiwa kifedha na Azam inayomilikiwa na bilionea Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na Yanga iliyo chini ya Mwenyekiti, bilionea pia, Yussuf Mheboob Manji.  
    Wakati mchakato wa Mo Dewji kuuziwa hisa Simba ukiendelea, timu imeanza vizuri tena katika msimu mpya, hadi sasa ikiwa inaongoza Ligi Kuu kwa kuwazidi mabingwa watetezi, Yanga wastani wa pointi nane ingawa wamecheza mechi moja zaidi.
    Ligi Kuu itafikia tamati Mei mwakani, lakini tayari tumeanza kuona fulana za Simba Bingwa 2016-2017 hata mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu haujamalizika. 
    Nini ninataka kuwaambia Simba SC, wasubiri kwanza kutwaa ubingwa ndiyo waanze sherehe kwa sababu Ligi Kuu bado haijafika hata nusu safari. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NI MAPEMA SIMBA SC KUJIONA MABINGWA, LIGI BADO MNO! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top