• HABARI MPYA

    Tuesday, December 15, 2015

    NIYONZIMA AWAIBUKIA YANGA AMEFUNGWA ‘HOGO’, ASEMA ALIUMIA KWENYE CHALLENGE

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    KIUNGO Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima (pichani kulia) ameibuka leo Dar es Salaam na kujisalimisha kwa uongozi wa Yanga SC, akiwa amefungwa plasta gumu (PoP), maarufu kama ‘hogo’. 
    Niyonzima anaibuka siku moja baada ya Yanga SC kusema itamchukulia hatua za kinidhamu kwa kitendo cha kuchelewa kurejea katika timu baada ya majukumu ya kitaifa.
    Nahodha huyo wa Rwanda aliruhusiwa kwenda kuichezea timu yake ya taifa katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge nchini Ethiopia, lakini baada ya mashindano hajarejea Dar es Salaam.
    Lakini leo, Katibu wa Yanga SC, Dk. Jonas Tiboroha amesema; “Niyonzima amekuja akiwa amefungwa PoP, anasema aliumia kwenye Challenge, ila sisi tutaomba uthibitisho wa vyeti vya hospitali aliyotibiwa tuamini, vinginevyo hatua za kinidhamu zitabaki pale pale,”amesema.
    Tiboroha amesema hiyo ni kwa sababu tabia hiyo sugu ya Niyonzima imekuwa ikiiathiri timu kwa namna moja au nyingine, kwa sababu yeye ni mchezaji tegemeo katika timu.
    Juzi Tiboroha alisema Niyonzima amechangia Yanga kutoibuka na ushindi katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Mgambo JKT mjini Tanga, ikitoa sare ya 0-0.
     “Mfano hii mechi ya jana (Jumamosi dhidi ya Mgambo), tulitegemea yeye angekuwapo angeisaidia timu, hakuwepo matokeo yake tumetoa sare, sasa tunataka hadi mashabiki ambao wanampenda huyo mchezaji, wajue matatizo yake,”alisema Tiboroha.
    Katibu huyo amesema kwamba mara nyingi mchezaji huyo amekuwa akiondoka katika klabu kinyume cha taratibu, kwa sababu Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) huwa halitumi barua ya kumuombea ruhusa.
    “Hata safari hii, yeye aliondoka mapema mno akisema amepata msiba kwao na hakucheza mechi mbili za mwisho, lakini bado amechelewa kurudi. Mwenzake, Mugiraneza (Jean Baptiste) amerudi mapema Azam FC na amecheza dhidi ya Simba (Jumamosi), kwa nini yeye hajarudi?”amehoji Tiboroha.
    “Kinachosikitisha zaidi amezima simu zake zote kiasi kwamba sisi hatujui yuko wapi. Wakati alipokuwa Ethiopia, alikuwa anawasiliana na kocha (Hans van der Pluijm) na alijua umuhimu wa kuwahi, sasa kitendo hiki tukitafsiri vipi?”amehoji tena Tiboroha.
    Niyonzima mwenyewe hakupatikana kwenye simu alipotafutwa jioni ya leo kuzungumzia suala hilo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NIYONZIMA AWAIBUKIA YANGA AMEFUNGWA ‘HOGO’, ASEMA ALIUMIA KWENYE CHALLENGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top