• HABARI MPYA

  Wednesday, December 16, 2015

  MOISE KATUMBI ANGEWEZA KUVUMILIA MAMBO HAYA YANGA SC?

  MIEZI minne baada ya kusaini Mkataba wa miaka mitatu uliogharimu kiasi kisichopungua Sh. Milioni 40, kipa Mudathir Khamis ametemwa klabu ya Yanga SC wiki iliyopita.
  Mudathir aliyekuwa analipwa Sh. Milioni 1.3 kwa mwezi, amevunjiwa Mkataba kwa makubaliano ambayo ni siri yake na Yanga SC na amehamia Mgambo JKT ya Tanga.
  Kiutaratibu, upande unaoamua kuvunja Mkataba ndiyo hulipa – na malipo anayostahili mvunjiwa Mkataba ni sehemu iliyobaki ya Mkataba wake.
  Kwa adhabu kama hizi, tumeona baadhi ya klabu hata Ulaya, zikishindwa kuwavunjia Mikataba wachezaji iliyowapa Mikataba mirefu na kuamua kubaki nao katika timu, ili kukwepa kuwapa fedha nyingi kwa wakati mmoja, ili iwalipe taratibu.

  Sasa Yanga wamemlipa kiasi gani cha fedha Mudathir? Ni siri yao. Aidha, Yanga SC wiki mbili zilizopita ilifikia makubaliano ya kuvunja Mkataba na kiungo Mbrazil, Andrey Coutinho akiwa amebakiza karibu mwaka mmoja.
  Kimsingi Coutinho naye pia kalipwa. Mwanzoni mwa msimu, wachezaji Hassan Dilunga na Edward Charles pia walivunjiwa mikataba yao, maana yake nao walilipwa.
  Aidha, mwanzoni mwa msimu pia, Yanga SC ilimleta beki Joseph Zuttah kutoka Ghana, lakini naye akavunjiwa Mkataba ndani ya mwezi mmoja, kabla ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuanza, maana yake naye alilipwa.
  Awali ya hapo, Desemba mwaka jana Yanga ilimuacha mshambuliaji Mbrazil Genilson Santana Santos ‘Jaja’ baada ya nusu msimu.
  Baadaye kidogo ikamuacha kiungo Mbrazil, Emerson De Oliviera Neves Roque aliyekuja kuchukua nafasi ya Jaja baada ya wiki tatu akiwa amesaini na kulipwa dau zuri.
  Kwa Emerson ilielezwa hakupata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) maana yake huyu inawezekana aliruhusiwa kuondoka tu bila malipo zaidi ya yale ya kusaini.  
  Na Agosti mwaka huu, Yanga SC imeleta beki Mtogo, Vincent Bossou ambaye amekuja kuanza kucheza baada ya mzalendo Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kuumia.
  Wakati tunasubiri kuona mustakabali wa Bossou, Yanga tena imeleta winga kutoka Niger, Issoufou Boubacar Garba ambaye amesaini Mkataba wa mwaka mmoja.
  Yaani inakuwa si shida Yanga kutoa fedha kusajili, au kutoa fedha kumlipa mtu aondoke – maana yake watu hawana uchungu na hizo fedha hata kidogo.
  Inafahamika hizo fedha zinatoka kwa mfadhili, ambaye pia ni Mwenyekiti, Yussuf Manji ambaye kwa bahati mbaya yeye hata hajishughulishi sana na timu, hivyo hata kama ‘kupigwa’ atakuwa haelewi chochote.
  Watu ambao wanasimamia usajili Yanga wameshindwa kuwa na haya japo kidogo, kufikiria namna wanavyofanya ubadhirifu wa fedha kupitia kivuli cha usajili.
  Usajili. Usajili usajili. Usajili imekuwa kama dili ambalo kuna watu ndani ya Yanga wanaomba muda ufike, ili Manji atoe fedha timu isajili na wao ‘wapige chao’.
  Hiyo ndiyo dhana ambayo anaweza kuwa nayo mtu yeyote kulingana na hali halisi inayoendelea ndani ya Yanga SC kwa sasa.
  Ally Mustafa ‘Barthez’ na Deo Munishi ‘Dida’ makipa wote wanaoaaminiwa wanaelekea kumaliza Mikataba yao na uongozi umemuacha kipa Mudathir badala ya japo kumtoa kwa mkopo kwa kisingizio eti ni mvivu wa mazoezi na ananenepa ovyo.
  Jamani kwa waliomuona Mudathir ni kweli amenenepa? Si kweli. Pengine amepungua kuliko wakati anaingia Yanga.
  Na suala wa uvivu wa mazoezi kuna adhabu nyingi za kumuadabisha mchezaji, ikiwemo kumkata mshahara au kumpeleka timu ya pili, ili abadilike na kurudi kwenye mstari.
  Lakini kwa kumuacha watu wataona tu umetengenezwa mwanya wa dili la kusajili kipa mwishoni mwa msimu ‘zipigwe hela’ tena.
  Wakati yote haya yanaendelea, klabu inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo jengo la makao makuu, Jangwani kuwa kama pagala, kutokuwepo kwa Uwanja wa mazoezi na hata msingi imara wa timu ya vijana.
  Yanga SC pamoja na kuwa na rasilimaliwatu kubwa, majengo mawili katikati ya mji, bado imeendelea kuwa tegemezi.
  Haijulikani viongozi wa Yanga SC wanafanya shughuli gani hata waitwe viongozi – matokeo yake sasa timu inaposafiri kwenye mechi za mikoani hadi walinzi wa ofisi nao wanakwenda.
  Ndiyo. Anasafiri Katibu, Mhasibu, Msemaji na wafanyakazi wote wa Ofisi pamoja na wajumbe wa Kamati ya Utendaji na wote kwa gharama za klabu, kuanzia mafuta ya gari zao, au tiketi za ndege, malazi na posho.
  Na hii ni kwa sababu hawana shughuli nyingine za kufanya kuiletea maendeleo Yanga SC na ndiyo maana hata wakati wa mapumziko hulazimisha mechi za kirafiki kwa maslahi yao. 
  Watu wanafikiria kupata mwanya wa kuchukua hela kwa Mwenyekiti ambaye pia ni Mfadhili, Manji kwa kuzua kambi za mikoani na kadhalika.
  Angalau wakati ule wa Lawrence Mwalusako alijitahidi kubana matumizi wakati mwingine wachezaji waliweka kambi makao makuu ya klabu, Jangwani.
  Lakini sasa hivi timu inaishi hoteli wakati wote wa msimu – hii watu watafikiria tu ni namna nyingine ya ‘kupiga pesa’ kwa njia ya ‘pasu’ na wenye hoteli. 
  Yaani ukweli ulivyo Manji ni mtu mwenye moyo wa kipekee wa kuipenda Yanga SC, kwani sina uhakika kama hata bilionea Moise Katumbi Chapwe angeweza kuvumulia mambo kama haya pale TP Mazembe. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MOISE KATUMBI ANGEWEZA KUVUMILIA MAMBO HAYA YANGA SC? Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top