• HABARI MPYA

    Sunday, June 01, 2014

    MALINZI ATAHUKUMIWA KWA KAULI ZAKE

    KWA muda sasa soka ya Tanzania imekuwa ikihusishwa na upangwaji matokeo, lakini bado viongozi wa mchezo huo nchini hawajathubutu kuchukua hatua.
    Ni jambo la kawaida kusikia wachezaji wamesimamishwa au kufukuzwa katika klabu kwa tuhuma za kuhujumu timu zao.
    Bahati mbaya haiwi wazi sana, lakini taarifa za vyombo vya habari kutoka kwenye vyanzo vya klabu zimekuwa zikileta tuhuma hizo mara kwa mara.
    Klabu mpya na ambayo inategemewa mno katika kuleta mabadiliko kwenye soka ya Tanzania kutokana na mfumo wake wa kisasa uendeshwaji, Azam FC bahati mbaya nayo imeingizwa katika mkumbo huo.

    Azam imewahi kuwasimamisha wachezaji wake watatu tegemeo, kipa Deo Munishi ‘Dida’ na mabeki Erasro Nyobi na Said Morad kwa tuhuma za kuhongwa kuhujumu timu hiyo.
    Lakini pia, Azam nao baada ya kufanikiwa kutwaa ubingwa msimu huu, wameshutumiwa na waliokuwa wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa, Yanga SC kwamba eti walikuwa wanahonga.
    Zote zinabaki kuwa ni tuhuma ambazo ni wajibu kufanyiwa kazi, ili kama kweli kuna uozo huo kwenye soka yetu uondolewe.
    Wiki hii, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi aliapa kwa jina la Mungu, kwamba akimgundua mtu anatoa rushwa kupanga matokeo katika mashindano yoyote chini ya utawala wake, ajuta kuzaliwa.
    Malinzi alisema hayo wakati akizungumza katika usiku wa sherehe za tuzo na zawadi za washindi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu uliopita Jumanne wiki hii ukumbi wa Golden Jubilee Tower, Mtaa wa Ohiao, Dar es Salaam,.
    Malinzi aliwashutumu marefa kwamba wanahongwa mno na wamejisahau kiasi kwamba msimu unapoanza wanaanza kupanga bajeti za matumizi makubwa kwa kutegemea rushwa.
    Hata hivyo, Malinzi amesema; “Ila nasema, siku nikimgundua mtu anayetoa rushwa katika soka ya nchi hii, wallahi (haki ya Mungu) atanitambua mimi ni nani, nasema atajuta kunifahamu,”.
    Malinzi aliwaasa viongozi wa klabu baada ya kusajili wachezaji wa gharama kubwa, basi waachane na desturi ya kuhonga marefa, kwani inaharibu soka ya Tanzania.
    Malinzi aliwapongeza mabingwa wapya wa Ligi Kuu, Azam FC waliowapiku waliokuwa mabingwa watetezi, Yanga SC waliomaliza nafasi ya pili msimu huu.
    Pamoja na hayo, Malinzi ametoa changamoto kwa wadhamini wa ligi hiyo, Vodacom Tanzania kuboresha udhamini wao na akasema anafurahi atakuwa na kikao nao hivi karibuni kuzungumzia suala hilo.
    Katika sherehe za utoaji wa tuzo hizo usiku wa jana, mshambulaji wa Azam FC kutoka Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche aliibuka mchezaji bora wa Ligi Kuu msimu wa 2013-2014 akiwapiku Anthony Matogolo wa Mbeya City na Lugano Mwangama wa Prisons.
    Kwa ushindi huo, Kipre amezawadiwa kitita cha Sh. Milioni 5.2, wakati kipa wa Mtibwa Sugar ya Morogoro, Hussein Sharrif ‘Cassilas’ ameshinda tuzo ya mlinda mlango bora wa Ligi Kuu akiwapiku David Burhan wa Mbeya City na Beno Kakolanya. 
    Juma Mwambusi Mwambusi wa Mbeya City, alishinda tuzo kocha bora, akiwaangusha Charles Boniface Mkwasa wa Yanga SC na Mecky Mexime wa Mtibwa Sugar na kupewa Sh. Milioni 5.2. 
    Refa Israel Mujuni Nkongo wa Dar es Salaam ameibuka mwamuzi bora akilamba Sh. milioni 7.8 baada ya kuwabwaga Isihaka Shirikisho wa Tanga na Jonasia Rukia wa Kagera walioingia kwenye kipengele hicho.  
    Tuzo ya Mfungaji bora wa msimu ilikwenda kwa mshambuliaji wa Simba, Mrundi Amisi Tambwe.
    Tambwe aliyefunga magoli 19, alizawadiwa Sh. milioni 5.2.
    Tambwe aliwashinda Elias Maguri wa Ruvu Shooting, Kipre Tchetce wa Azam FC wote mabao 13, Mrisho Ngassa na Hamisi Kiiza wote wa Yanga SC ambao wote walifunga mabao 12 kila mmoja. 
    Yanga SC imeibuka timu yenye nidhamu kwa mara nyingine baada ya kutwaa tuzo hiyo pia msimu wa 2012/13 wa Ligi Kuu na kuzawadiwa Sh. Milioni 16 ikizipiku Azam FC na JKT Oljoro.
    Zawadi nyingine zilizotolewa ni pamoja na Sh. milioni 75 iliyokwenda kwa Azam FC waliotwaa ubingwa, Yanga SC Sh. milioni 35, Mbeya City Sh. milioni 26 na Simba SC Sh. 21.
    Angalau Malinzi amekuwa kiongozi wa kwanza wa TFF kuonyesha anakerwa na rushwa katika mchezo huo hata kuahidi kuchukua hatua.
    Lakini vyema ikawa kauli inayotokana na msimamo thabiti au dhamira aliyonayo kiongozi huyo wa juu wa soka nchini- na si kauli ya kuifanya hotuba yake ya siku ya tuzo za washindi wa Ligi Kuu iwe na mashiko.
    Ukweli ni kwamba upangwaji wa matokeo ni kitu kibaya katika soka yetu na ambacho tunapaswa kukipiga vita kwa nguvu zote.
    Kwa wapenda maendeleo ya soka yetu, hapana shaka watakuwa wamefurahia kauli ya Malinzi na sasa watakaa mkao wa kusubiri matokeo yake. 
    Vyema Malinzi atambue kwamba Watanzania sasa wanataka kushuhudia soka ya matokeo halisi ya uwanajani ili kupata bingwa halali bila mizengwe- na kwa maana hiyo kauli yake itamhukumu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MALINZI ATAHUKUMIWA KWA KAULI ZAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top