• HABARI MPYA

    Thursday, June 26, 2014

    MAXIMO: NIMEFURAHI SANA KUJA YANGA

    Na Nagma Said, DAR ES SALAAM
    KOCHA mpya wa Yanga SC, Mbrazil Marcio Maximo amesema kwamba amefurahi kurudi Tanzania baada ya takriban miaka minne, lakini mengi juu ya ujio wake wa pili nchini, atazungumza kesho. 
    Kocha huyo wa zamani wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars amewasili nchini mchana wa leo kwa ajili ya kuja kuwafundisha mabingwa wa kihistoria nchini, Yanga.
    Maximo alitua katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam saa nane mchana kwa Shirika la Ndege ya Afrika Kusini, akiwa  na kocha msaidizi wake, Leonaado Neiva na kulakiwa na mashabiki wa Yanga waliojitokeza kumpokea, wakiongozwa na Katibu Mkuu wa klabu, Benno Njovu.
    Nimefurahi kuja tena; Maximo akizungumza na Waandishi wa Habari baada ya kuwasili nchini leo

    Kocha huyo aliyeiwezesha Taifa Stars kushiriki fainali za kwanza za CHAN mwaka 2009 nchini Ivory Coast, ilimchukua muda wa nusu saa kutoka nje kufuatia kukamilisha taratibu ya Uhamiaji na kuvalisha stafu ya Yanga.
    Katika mapokezi hao,  polisi walilazimika kumpitisha mlango  wanaotumia kupita watu maarufu (VIP) kutokana na pilika pilika za uwanjani hapo.
    Kutokana na umati wa mashabiki  uliokuwa umefurika katika mlango unaotumiwa kupita stafu na wageni, Polisi walishindwa kumpitisha katika mlango huo na gafla waliamua kumpitisha VIP.
    Baadhi ya mashabiki wa Yanga, waliokwenda kumpokea walionekana kuwa na furaha huyo huku wakimtaka aonyeshe vidole vitano juu, wakiashiria kama ataweze kurudisha mabao 5-0 waliyofungwa na watani wao wa jadi Simba, katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, iliyochezwa  Mei 6 mwaka juzi, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili, alisema amefurahi kurejea tena Tanzania, baada ya kuishi nchini kwa takribani miaka minne wakiifundisha timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars.
    Maximo alisema anatarajia kuanika mikakati yake kesho katika Mkutano na Waandishi wa Habari Dar es Salaam.
    Baadaye, Maximo na msaidizi wake, alipanda gari namba T390 aina ya Harrier,  lililokuwa likiendeshwa na Katibu wa Yanga, Njovu na kuelekea moja kwa moja katika makao makuu ya klabu hiyo, yaliyopo Mtaa wa Twiga na Jangwani.
    Katika msfara wake ulipitia Barabara ya Msimbazi, ambao ulipita hadi makao makuu ya Simba, lakini mashabiki wa klabu hiyo, walionekana kutoshtusha na ujio wake.
    Baada ya kuwasili katika makao makuu wa klabu hiyo, Maximo alilakiwa na mashabiki wengi ambao walikuwa wakimsubiri kwa hamu kubwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAXIMO: NIMEFURAHI SANA KUJA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top