• HABARI MPYA

    Sunday, June 22, 2014

    USHAURI GANI ZAIDI YA HUU VAN PERSIE ANGETUPA WATANZANIA?

    ENGLAND imekuwa moja ya timu za mwanzoni kabisa kuaga michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu nchini Brazil, ikicheza mechi mbili za mwanzo Kundi D bila kuvuna pointi.
    Baada ya kufungwa na Italia na Uruguay, England watakabidhi funguo za vyumba katika hoteli waliyofikia wiki ijayo watakapocheza mechi yao ya mwisho ya kundi dhidi ya Costa Rica.
    Baada tu ya kufungwa mechi ya kwanza, kama ilivyo ada ya vyombo vya habari nchini humo, husifia sana wachezaji wao, lakini huwageuka mara moja wanapofanya vibaya- safari hii ilikuwa hivyo pia.

    Basi kwa mara nyingine vyombo vya habari England vikaanza kuponda wachezaji na lawama zaidi zikapelekwa kwa mshambuliaji Wayne Rooney.
    Baada ya kipigo cha pili mbele ya Uruguay, vyombo vya habari pamoja na kuwaponda wachezaji akiwemo Rooney, pia vimeanza kumshambulia kocha Roy Hodgson vikitaka afukuzwe.
    Unaweza ukajiuliza Hodgson afukuzwe kwa kosa lipi, wakati tayari wachezaji wamekwishalaumiwa maana yake wao ndio tatizo.
    Hapo ndipo wakati mwingine unaweza kuvidharau vyombo vya habari vya England- kwamba navyo kwa kiasi kikubwa vinachangia matatizo ya soka ya nchi hiyo.
    Vimejaa ushabiki wa klabu, vipo mstari wa mbele kushabikia wachezaji wakubwa wa kigeni kusajiliwa na klabu za nchini humo, jambo ambalo linawanyima nafasi wazawa katika klabu hizo.
    England hawataki kuteseka katika kutengeneza soka yao, katika ngazi ya klabu wamefanikiwa. Klabu zao zinafika mbali kwenye michuano ya Ulaya na kubeba mataji pia zikibebwa na nyota wa kigeni.
    Lakini linapokuja suala la timu ya taifa, haina makali na matokeo yake ndiyo kama haya sasa wanaanza kuvurugana wenyewe kwa wenyewe.
    Baada ya mechi na Uruguay, mshambuliaji wa Manchester United, Robin van Persie aliombwa maoni yake na gazeti la Daily Mail la Uingereza juu ya kufanya vibaya kwa timu hiyo Brazil. 
    Kwanza, van Persie aliwaambia Rooney hatakiwi kubeba lawama kwa England kutolewa mapema katika Kombe la Dunia, pili akawashauri Chama cha Soka nchini humo kutazama msingi wake wa soka ya vijana.
    Van Persie amesema Rooney na England walicheza vizuri dhidi ya Uruguay kiasi cha kutosha kushinda na kusonga mbele, na akamfagilia mshambuliaji mwenzake wa Mancheser United, ambaye alishutumiwa vikali baada ya kipigo cha England katika mechi ya kwanza dhidi ya Italia.
    "Niliangalia sehemu kubwa ya mchezo dhidi ya Italia na mchezo wote dhidi ya Uruguay, na ninafikiri ni aibu. England ilicheza vizuri mno na hawakuwa na bahati kabisa. Wayne alipambana sana, alicheza vizuri sana na angeweza kufunga mabao manne, hivyo sifikiri ni wa kulaumiwa.
    "Wayne ni mchezaji mkubwa. Nimesema hivi mara nyingi, Wayne alikuwa sehemu ya sababu ya mimi kuja Manchester United. Sijawahi kujuta kusema hivyo, kwa sababu kwa kufanya naye mazoezi na kucheza naye ananioyesha ni mchezaji wa kiwango cha dunia.
    "Alipiga mpira wa adhabu vizuri mno, alipiga shuti zuri lililookolewa na kipa, alipiga kichwa kilichogonga mwamba wa juu na akafunga bao. Si wa kulaumiwa, Alijitoa kwa kitu kwa ajili ya nchi yake. Si haki kumshutumu sana yeye.
    "Alipoteza nafasi tatu za kufunga kwa inchi chache, na hiyo maana yake alikuwa katikati ya mstari wa kushinda na kushindwa, baina ya kurudi nyumbani na kusonga mbele,”.
    Van Persie amesema FA ya England inapaswa kutazama muundo wake wa makocha na kuwekeza zaidi katika maendeleo ya vijana, kama ilivyo kwa Uholanzi na nchi nyingine zinazoongoza Ulaya. 
    "Sasa ni juu ya FA kuwa na mtazamo sahihi ili kuona England itaelekea wapi.
    "Ni muhimu sana kuwekeza kwenye soka ya vijana, katika makocha wazuri na vifaa kwa ajili ya nyota chipukizi kucheza," amesema.
    Alichokisema mshambuliaji huyo wa zamani wa Arsenal ndiyo hali halisi juu ya England na kweli ni juu ya FA yao kuamua kwa mustakabali wa soka yao.
    Tazama soka ya leo, unaweza kujionea mabadiliko makubwa, nchi nyingi zimeimarika mno na hakuna timu ya kudharau tena.
    Argentina inadhibitiwa na Iran, hayo ni matunda ya kufuata njia sahihi za uwekezaji katika soka- lakini kwa nchi ambazo bado hazijaona umuhimu wa jambo hilo, ndio kama England.
    Heri yao England, wanavurugana, lakini wamefika Kombe la Dunia, lakini vipi nchi yetu Tanzania? Kabla na tangu Uhuru wetu mwaka 1961, mafanikio makubwa ni kucheza Fainali za Mataifa ya Afika mara moja tu mwaka 1980 nchini Nigeria. Wachezaji waliokuwamo kwenye kikosi cha Taifa Stars iliyofuzu na kucheza fainali hizo ni wakubwa sana, ni magwiji na wa kihistoria.
    Ndiyo mfano. Ndiyo wanaotajwa kila siku. Maana yake hilo ndilo kubwa la nchi yetu kujivunia katika ulimwengu wa soka. Fikiri kiasi gani sisi ni mufilisi kisoka?
    Sitaki kuamini tumejikatia tamaa, labda tu mipango ya wakubwa inatofautiana na njia halisi za kuelekea kwenye mafanikio, au dhana halisi ya uwekezaji kwenye soka ya vijana haijaeleweka.
    Sisi ni hodari wa kuanzisha mashindano ya kuibua vipaji, lakini siku zote tunashindwa kuwa na mikakati ya kuwaendeleza vijana baada ya kuwaibua.
    Kipaji ni sawa na mbegu unapokiibua- kinachofuata ni kuipanda hiyo mbegu na kuistawisha ili kukuza mmea, siku moja uje kuvuna matunda.
    Lakini kwetu inatosha baada ya kupata bingwa wa Copa Coca Cola na tunasubiri msimu mwingine tena, hatutaki kujishughulisha na vipaji vilivyoonekana katika mashindano yaliyomalizika.
    Hatuwezi kufika popote kwa staili hii nasi tutakuwa kama Waingereza, Ligi yao inatawaliwa na wachezaji wa kigeni, yetu hivyo hivyo- Kipre Tchetche wa Ivory Coast kamrithisha Amisi Tambwe wa Burundi ufungaji bora.  
    TFF kama imemuelewa van Persie katika ushauri wake kwa England, basi na yenyewe itazame muundo wake wa maendeleo ya soka ya vijana, kama kweli umekaa vizuri.
    TFF ichimbe na ijue maana halisi ya uwekezaji kwenye soka ya vijana na baada ya hapo, nii juu yao sasa kuamua kwa mustakabali wa soka ya vijana.
    Ushauri ambao van Persie amewapa England, BIN ZUBEIRY amekishawapa sana TFF, tangu bado FAT, tangu bado Muhiddin Ndolanga ndiye kiongozi mkuu wa mpira wa miguu nchi hii. Na huyo van Persie angeijua Tanzania na matatizo ya soka yake, asingewapa ushauri mwingine zaidi ya huo huo aliowapa England. Alamsiki. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: USHAURI GANI ZAIDI YA HUU VAN PERSIE ANGETUPA WATANZANIA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top