• HABARI MPYA

    Sunday, June 29, 2014

    ZAIDI YA DOMAYO, TUNAHATARISHA MAISHA YA WACHEZAJI WANGAPI WENGINE NCHINI?

    KLABU ya Azam FC imelazimika kuingia gharama za zaida kumtibu kiungo Frank Domayo baada ya kugundua ilimsajili kwa mamilioni mengi kutoka Yanga akiwa majeruhi.
    Baada ya kukamilisha usajili wa mchezaji huyo aliyekuwa huru, Azam FC ilimpeleka kwenye vipimo vya afya na ndipo ikagundulika kiungo huyo alikuwa ana matatizo kwenye misuli ya nyama za paja.
    Domayo alikuwa anahatarisha maisha yake ya uwanjani kwa kuthubutu kuendelea kucheza wakati msuli wake mmoja wa nyama za paja umechanika.

    Wataalamu wamesema, iwapo kiungo huyo angechanika msuli mwingine wa eneo hilo, ina maana asingeweza kucheza tena soka.
    Taifa lingepoteza kipaji cha mchezaji mdogo tu, aliyeibuka miaka mitatu iliyopita katika timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 na kupandishwa timu ya wakubwa.
    Mchezaji mwenyewe angepoteza dira yake maisha yake, kwa sababu soka ndio ajira yake.
    Mungu saidia, hekima na busara za Azam ziliwatuma kwenda kumfanyia vipimo vya afya na kugundua tatizo hilo- na ikawa bahati zaidi kwake kwa klabu hiyo kuamua kumtibu.
    Azam ilihitaji kuanza kumtumia mara moja mchezaji huyo baada ya kumsajili, lakini sasa italazimika kumsubri hadi mwakani wakati akiuguza maumivu yake baada ya upasuaji.
    Mchezaji huyo alifanyiwa upasuaji wa kiwango kizuri nchini Afrika Kusini na anatakiwa kuwa nje kwa miezi mitatu.
    Kwa miaka yote mitatu tangu kuibuka kwake katika soka ya Tanzania, Domayo amekuwa akicheza mechi za klabu na timu za taifa, kuanzia U20 hadi ya wakubwa.
    Na kwa ujumla kwa miaka yote miwili iliyopita amekuwa mchezaji chaguo la kwanza na tegemeo la timu ya taifa na klabu yake ya zamani, Yanga SC.
    Kama ilivyo kwa Yanga SC, timu ya taifa pia wakati wote imekuwa na Madatkari wa kiwango cha juu, unaweza kujiuliza wamewezaje kumuacha mchezaji huyo acheze katika hali kama hiyo?
    Na kama Domayo alikuwa anacheza akiwa majeruhi na kuhatarisha maisha yake ya soka, je ni wachezaji wangapi hivi sasa nchini wanacheza wakiwa katika hali kama hiyo?
    Ni tatizo. Tatizo kwa sababu hizi ni dalili za kukosa umakini kwa wahusika katika majukumu yao.
    Hii ni hatari sana- uzembe kama huu hakika haupaswi kuvumiliwa hata kidogo, kwa sababu unayaweka rehani maisha ya vijana wengi katika soka yetu. 
    Yanga SC ilikuja kugundua baada ya kumsajili kwa fedha nyingi beki Mbuyu Twite kama anacheza na chuma mguuni, baada ya kufanyiwa upasuaji uliolazimu awekewe kifaa hicho kutokana na msuli wake kuvunjika kabisa alipokuwa APR ya Rwanda.
    Wazi kama Yanga SC wangekuwa na utamaduni wa kumfanyia vipimo vya afya mchezaji kabla ya kumsajili, basi tatizo la Mbuyu wangelijua mapema na maamuzi yao yangetokana na majibu ya vipimo hivyo.
    Inaonekana tuna matatizo ya kipimo cha MRI hapa nchini, lakini bado zipo hospitali ambazo vipimo vyake ni vya uhakika kama Agha Khan- ambako waligundua tatizo la Domayo.
    Basi ipo haja ya kuchukua hatua zaidi, kuhakikisha kwamba mchezaji anaingia uwanjani akiwa salama kabisa kuliko kuhatarisha maisha yake.
    Stori ya Domayo inasikitisha, inaelezwa akiwa Yanga SC kila alipokuwa anasikia maumivu sehemu hiyo, alikuwa anafungwa barafu kumpoza maumivu na kisha anaendelea kucheza.
    Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linapaswa kuchukua hatua madhubuti, kuhakikisha mchezaji anaingia uwanjani kucheza akiwa salama kwa asilimia 100.
    Na si vibaya TFF ikiweka utaratibu wa kuomba taarifa za kitaalamu za afya za wachezaji kabla ya msimu na kila mchezaji anapoumia, baada ya kukamilisha tiba kabla ya kurejea uwanjani, bodi hiyo ya soka nchini ikabidhiwe taarifa zake za madakari.
    Kwa kiasi fulani hiyo itatuondoa kwenye hatari ambayo tupo nayo kwa sasa. Tafakari kwa staili hii ya sasa wachezaji kuchezeshwa bila kujali afya zao, ni wachezaji wangapi zaidi ya Domayo wanaocheza nchini wakiwa majeruhi? Ramadhani karim.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ZAIDI YA DOMAYO, TUNAHATARISHA MAISHA YA WACHEZAJI WANGAPI WENGINE NCHINI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top