• HABARI MPYA

    Sunday, June 29, 2014

    KILA LA HERI SIMBA SC, KUMBUKA MTAVUNA MTAKACHOKIPANDA LEO

    SIMBA SC inatarajiwa kufanya uchaguzi wake Mkuu leo, katia bwalo la Maofisa wa jeshi la Polisi,  Oystrebay, Dar es Salaam kuanzia saa 3:00 asubuhi 
    Hiyo inafuatia uongozi wa sasa chini ya Mwenyekiti Alhaj Ismail Aden Rage kumaliza muda wake.
    Uongozi wa Rage umemaliza muda wake ukiwa na makovu mengi baada ya miaka minne migumu, hali iliyosababisha baadhi ya viongozi, akiwemo aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ kujiuzulu.
    Rage anaweza kujivunia kumfunga mtani, Yanga SC mabao 5-0 katika miaka yake minne ya kuwa madarakani, lakini kwa ujumla Simba SC haikuwa bora kipindi chake chote, ndiyo maana miaka miwili mfululizo imekosa tiketi ya kucheza michuano ya Afrika.

    BIN ZUBEIRY inafahamu mchakato wa uchaguzi huo unaofikia kilele chake leo, ulipitia katika misukosuko mingi, wagombea kuenguliwa kwa kukiuka taratibu na baadhi ya wanachama kwenda mahakamani kutaka kuzuia zoezi hilo.
    Lakini kwa kuwa klabu hiyo imeweza kuvuka salama kwenye vigingi hivyo na leo wanachama wake wanakutana Oysterbay kuchagua viongozi, ipo haja ya kusahau yaliyopita.
    Wanachama wa Simba SC wanapaswa kusahau yaliyopita na kuelekeza fikra zao katika kuteua viongozi bora kutoka wagombea waliopitishwa ili kuitengezea mazingira klabu yao iweze kujiinua upya.
    BIN ZUBEIRY inafahamu, wapo wanachama ambao wagombea waliowaunga mkono wameenguliwa katika uchaguzi- lakini huo si mwisho wa Simba SC na bado wanabaki na wajibu wa kuchagua viongozi bora wa kuongoza klabu yao.
    Kitendo cha kwenda kupiga kura za hasira kwa mgombea hata asiyefaa, kwa sababu mgombea waliyemtaka ameenguliwa kitaiathiri klabu yao wenyewe na itaingia katika miaka mingine minne migumu ya migogoo na matokeo mabaya.
    Hekima, busara na mapenzi ya dhati ya klabu yao, ndiyo mambo ambayo wanachama wa Simba SC wanatakiwa kuyatanguliza leo, kwa kuhakikisha wanachagua viongozi watakaorejesha heshima ya klabu yao.
    BIN ZUBEIRY inaamini wanachama walio wengi wa Simba SC wanafahamu ubora wa wagombea waliopitishwa- na wanaweza kutumia silaha hiyo kwa kuiwekea misingi imara klabu yao kwa kuwateua wale walio bora. Sisi wa BIN ZUBEIRY tunawatakia uchaguzi mwema, wa amani, huru na wa haki. Wana Simba SC, watumie kura zao kuwekeza viongozi bora watakaorejesha heshima ya klabu yao, kila la heri na mfungo mwema wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.      
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KILA LA HERI SIMBA SC, KUMBUKA MTAVUNA MTAKACHOKIPANDA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top