• HABARI MPYA

    Tuesday, December 10, 2019

    MO DEWJI AAHIDI KUWAPA SH MILIONI 100 NA BODABODA TAIFA STARS WAKIBEBA KOMBE LA CHALLENGE

    Na Mwandishi Wetu, KAMPALA
    MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya klabu ya Simba, Mohamed ‘Mo’ Dewji ameahidi kuwapa Sh. Milioni 100 wachezaji wa kikosi cha Tanzania Bara kama watafanikiwa kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge michuano inayoendelea nchini Uganda.
    Dewji yupo Uganda kwa shughuli zake za kibiashara na jana alitembelea kambi ya Kilimanjaro Stars na pamoja na ahadi ya Milioni 100 kwa kikosi kikitwaa taji hilo, ameahdi kumpa kila mchezaji na Maafisa wote benchi la ufundi pikipiki.
    “Kama Mtanzania ambaye napenda kuona nchi yangu inafanya vizuri kwenye mchezo wa soka nimeahidi kutoa zawadi ya Tsh. 100m na zawadi ya pikipiki za MO Boxer kwa wachezaji na benchi la ufundi la timu yetu ya Tanzania Bara iwapo itashinda ubingwa wa michuano ya Cecafa ambayo inafanyika hapa nchini Uganda,”alisema.
    Baada ya kufungwa 1-0 na Kenya katika mchezo wake wa kwanza wa Kundi B Jumapili Uwanja wa Lugogo mjini Kampala, Kilimanjaro Stars inayofundishwa na kocha Juma Mgunda anayesaidiwa na Zubery Katwila itateremka tena dimbani leo kumenyana na ndugu zao, Zanzibar kabla ya kukamilisha mechi zake za kundi hilo kwa kumenyana na Sudan Jumamosi.
    Tanzania Bara imewahi kutwaa taji la CECAFA Challenge mara tatu, 1975 Dar es Salaam, 1994 Kenya na 2010 Dar es Salaam pia wakiwa chini ya kocha Mdenmark, Jan Borge Poulsen.
    CECAFA Challenge ndiyo michuano mikongwe zaidi ya soka barani Afrika ambayo ilianza mwaka 1926 ikijulikana kama Kombe la Gossage hadi mwaka 1966, ilipobadilishwa na kuwa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati hadi mwaka 1971 ilipobadilishwa tena na kuwa CECAFA Challenge.
    Uganda ndiyo mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo tangu mwaka 1971, wakiwa wamelitwaa mara 14, wakifuatiwa na Kenya mara saba, Ethiopia mara nne na Tanzania mara tatu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MO DEWJI AAHIDI KUWAPA SH MILIONI 100 NA BODABODA TAIFA STARS WAKIBEBA KOMBE LA CHALLENGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top