• HABARI MPYA

    Friday, December 13, 2019

    MALINZI NA MWESIGWA WAACHIWA HURU LEO DAR BAADA YA KUIPA FAINI ZAO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    ALIYEKUWA Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamal Malinzi na aliyekuwa Katibu wake, Selestine Mwesigwa leo wameachiwa huru baada ya kulipa faini ya fedha taslimu Sh. 1,500,000 kama walivyaogizwa na Mahakama jana.
    Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam jana iliwahukumu kifungo cha miaka miwili gerezani au faini ya Sh. 500,000 kila mmoja, Malinzi na Mwesigwa kwa mashitaka ya kughushi nyaraka za muhtasari wa kikao cha Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo.
    Mwesigwa yeye alitakiwa kulipa faini ya Sh. 1,000,000 kutokana na kukutwa na mashitaka mawili; kughushi nyaraka za kikao cha Kamati ya Utendaji ya TFF na kutengeneza nyaraka za uongo.
    Pamoja na wote wawili kukubali kulipa faini jana jioni baada ya kusomewa hukumu yao, lakini ofisi zilikuwa zimekwishafungwa hivyo wamerudishwa rumande na zoezi hilo limefanyika leo ndipo wakaachiwa huru.
    Malinzi na Mwesigwa kwa pamoja na aliyekuwa Mhasibu, Nsiande Isawafo Mwanga walipelekwa rumande Juni 29, mwaka 2017 baada ya kusomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya shirikisho hilo iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam.
    Washitakiwa wengine katika kesi hiyo mbali ya Malinzi mwenye umri wa miaka 57, Mwesigwa miaka 46 na Nsia miaka 27 ni Meneja Ofisi wa TFF, Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya ambao kwa pamoja wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 na wanakabiliwa na mashitaka 30.
    Katika mashtaka hayo, Malinzi pekee alipewa mashtaka 28 ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha dola za Kimarekani 173,335 na Sh 43,100,000, wakati Mwesigwa alikuwa na mashitaka sita ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi na utakatishaji wa fedha.
    Nsiande alishitaka mawili ya utakatishaji wa fedha, Miriam anakabiliwa na mashitaka tisa ya kughushi na Frola anakabiliwa na shitaka moja la kughushi na wote walikana mashitaka hayo.
    Ikumbukwe, Malinzi aliingia madarakani TFF Oktoba mwaka 2013 baada ya kupata kura 72 kati ya 126 zilizopigwa akimshinda aliyekuwa mpinzani wake wa karibu, Athumani Nyamlani.
    Hata hivyo, Malinzi alishindwa kutetea nafasi yake Agosti 12, mwaka 2017 katika uchaguzi uliofanyika mjini Dodoma kutokana na kesi hiyo huku aliyekuwa Makamu wake, Wallace Karia akishinda kiti cha Urais wa shirikisho hilo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MALINZI NA MWESIGWA WAACHIWA HURU LEO DAR BAADA YA KUIPA FAINI ZAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top