• HABARI MPYA

    Monday, November 05, 2018

    TFF YAMFUNGIA MAISHA KUTOJIHUSISHA NA SOKA WAKILI MSOMI REVOCATUSS KUULI ALIYEUWEKA MADARAKANI UONGOZI WA KARIA

    Na Nasrsah Omary, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemfungia maisha kutojihusisha na soka aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi TFF, wakili Revocatus Kuuli.
    Akitaja hukumu hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili TFF, Hamidu Mbwezeleni, alisema wamemfungia wakili huyo kutokana na kukiuka misingi ya katika ya TFF.
    Mbwezeleni alisema Kuuli alikiuka misingi ya katiba ya TFF kwa kusambaza nyaraka ya siri aliyetumiwa na Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao hivi karibuni juu ya suala la uchaguzi wa klabu ya Simba.

    Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili TFF, Hamidu Mbwezeleni wakati akitangaza kumfungia Wakili Revocatus Kuuli leo

    Kuuli amefungiwa baada ya kufunguliwa mashitaka matatu kufuatia sakata la uchaguzi Simba uliofanyika jana mjini Dazr es Salaam.
    Shitaka la kwanza la Kuuli ni kusambaza barua za TFF kinyume cha kufungu cha 16 (1) cha kanuni za Maadili za TFF tole la mwaka 2013 kinyume cha ibara ya 12.1 (b).
    Shitaka la pili ni kutoa maelezo yanayoonyesha  kuwa na mgongano wa maslahi kwa kuwapa watu wasiohusika kinume cha kifungu cha 16 (2) cha kanuni za Maadili  za TFF na kosa la tatu ni kufanya vitendo vinavyoshuhsa hadhi ya shirikisho kinyume cha ibara ya 50 (1).
    Na haya yote yanatokea wakati tayati TFF imekwishafanya mabadiliko ya Kamati ya Uchaguzi, ikimuondoa  Kuuli na wenzake wote na kumteua Malangwe Ally kuwa Mwenyekiti mpya.
    Na chanzo cha yote ni tofauti baina yake na Mtendaji Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau kiasi cha kufikia kulumbana kwenye vyombo vya Habari.   
    Ikumbukwe, Kuuli ndiye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF uliofanyika Agosti 12, mwaka jana na Wallace Karia akashinda nafasi ya Urais.

    TAARIFA KAMILI YA TFF JUU YA ADHABU YA WAKILI KUULI
    Kamati ya Maadili ya TFF iliyokutana Jumamosi Novemba 3,2018 pamoja na mambo mengine ilipitia shauri linalomkabili Ndugu Revocatus Kuuli, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), ambaye ameshtakiwa kwa makosa matatu ya kimaadili.

    2.0               TUHUMA ZILIZOWASILISHWA
    Sekretarieti ya TFF iliwasilisha mbele ya Kamati mashtaka matatu (3) ambayo ni;
    i).   Kusambaza nyaraka/barua za Shirikisho kinyume na ibara ya 12(1)(b) ya Katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ya Mwaka 2013 (kama ilivyorekebishwa Mwaka 2015) na kinyume na kifungu cha 16(1)&(2) cha Kanuni za Maadili za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Toleo la 2013.
    ii). Kutoa maelezo yanayoonesha kuwa na mgongano wa maslahi kwa kuwapa watu wasiohusika kinyume na kifungu cha 19(2) cha Kanuni za Maadili za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Toleo la 2013.
    iii). Kufanya vitendo vinavyoshusha hadhi ya Shirikisho kinyume na ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF ya Mwaka 2013 (kama ilivyorekebishwa Mwaka 2015).

    3.0               MAELEZO YA KOSA
    Ndugu Revocatus Kuuli kati ya tarehe 20 – 22 Septemba 2018, akiwa katika nafasi yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa makusudi na bila ya uhalali alitoa nyaraka ya TFF kabla ya wakati wake ikiwa ni barua rasmi ya Shirikisho na kuisambaza kwa watu wasiohusika.

    4.0               SHAURI LILIVYOENDESHWA
    Ndugu Revocatus Kuuli alipelekewa hati ya mashtaka ili afike mbele ya Kamati ya Maadili siku ya Jumamosi tarehe 3 Novemba 2018 saa 4.00 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zilizoko Uwanja wa Karume Ilala Dar es salaam. Hata hivyo Ndugu Kuuli hakufika mbele ya Kamati na wala hakutuma taarifa ya kuomba udhuru, kama alikuwa nao. Baada ya kupitia nyaraka na vielelezo mbalimbali, Kamati iliamua kuendelea na shauri bila ya kuwepo Ndugu Kuuli, kwa kuwa katika wito wake alielezwa kuwa Kamati itakuwa na haki ya kufanya uamuzi dhidi yake endapo hatafika wala kutuma mwakilishi wa kumtetea.
    Baada ya kukubaliana kuendelea na shauri, Kamati ilitaka maelezo ya kina kutoka Sekretarieti. Sekretarieti ya TFF iliieleza Kamati kuwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF chini ya uenyekiti wa Ndugu Revocatus Kuuli, ilifanya kikao Dodoma Hotel siku ya Jumamosi tarehe 15 Septemba 2018 jijini Dodoma. Katika kikao hicho, miongoni mwa mambo yaliyojadiliwa, ni suala la uchaguzi wa Simba ambapo Kamati ya Uchaguzi iligundua mapungufu kadhaa. Klabu ya Simba ikaelekezwa, kupitia barua Kumb. Na. DLM/LM.679/2018 ya tarehe 15 Septemba 2018, kuyafanyia marekebisho mapungufu hayo ili yawasilishwe kwa ajili ya kupitishwa. Hata hivyo, Ndugu Kuuli alianza kutangaza kwenye vyombo vya habari kuwa amesimamisha uchaguzi wa klabu ya Simba huku akijua fika kuwa hayo si maamuzi ya Kamati ya Uchaguzi. 
    Sekretarieti ya TFF, baada ya kusikia taarifa hizo kwenye vyombo vya habari, ilimwandikia Ndug Kuuli barua Kumb. Na. TFF/ADM/LM.748/2018 ya tarehe 19 Septemba 2018, kuomba ufafanuzi kama hayo anayotangaza kwenye vyombo vya habari ni maamuzi ya kikao. Sekretarieti iliwasilisha mbele ya Kamati ushahidi unaoonyesha kuwa barua hiyo ilipokelewa na Bi Mariamu Mirambo, msaidizi wa Ndugu Kuuli, tarehe 20 Septemba 2018. Ndugu Kuuli, badala ya kuijibu, aliisambaza barua hiyo kati ya tarehe 20 – 22  Septemba 2018 kwa watu ambao hawakuwa wahusika katika jambo hili wenye anuani zifuatazo; michaelwambura5@yahoo.com na aden.rage@yahoo.com bila kuwa na mamlaka wala idhini kutoka TFF. Sekretarieti iliwasilisha ushahidi unaoonyesha kuwa mmoja wa watu waliotumiwa barua hiyo ni Ndugu Michael Wambura, ambaye amefungiwa kutojihusisha na masuala ya mpira wa miguu ndani na nje ya nchi maisha. Mwingine aliyetumiwa barua hiyo ni Ndugu Aden Rage. Kitendo cha kuwatumia barua hiyo watu hao kinadhihirisha wazi kuwa Ndugu Kuuli alikuwa na maslahi ya aina yake katika suala hilo kwani watu hao waliwahi kuwa viongozi wa klabu ya Simba katika nyadhifa mbalimbali kwa nyakati tofauti. 
    Pamoja na Sekretarieti ya TFF kumuomba mwongozo kuhusiana na kusimamisha uchaguzi wa Simba kupitia barua Kumb. Na. TFF/ADM/LM.748/2018 ya tarehe 19 Septemba 2018, Ndugu Kuuli hakujibu bali aliendelea kuongea na vyombo mbalimbali vya habari huku akitumia lugha chafu na ya kashfa dhidi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Sekretarieti iliwasilisha ushahidi mbele ya Kamati wa mahojiano yake na vyombo mbalimbali vya habari yakimnukuu Ndugu Kuuli akitoa maneno yenye kushusha hadhi ya Shirikisho. 
    Baada ya kupitia shauri hilo, Kamati imemtia hatiani pasipo na shaka kwa makosa yote matatu (3).

    5.0               HUKUMU
    i).  Shitaka la kwanza
    Kamati imejiridhisha kuwa Ndugu Revocatus Kuuli, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF alisambaza barua (waraka) iliyotoka kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) bila kuwa na mamlaka wala idhini ya kufanya hivyo. Barua hiyo ilisambazwa kwa watu wasiohukika huku mmoja wao akiwa amefungiwa kujihusisha na masuala ya mpira wa miguu ndani na nje ya nchi maisha. Katika mahojiano na kituo kimoja cha redio Ndugu Kuuli alikiri kuwa aliamua kuisambaza barua hiyo kwa vile hakuuona usiri wowote kwani haikugongwa mhuri wa siri. Kamati ilisikitishwa na kauli hiyo ya Ndugu Kuuli kwani akiwa kama kiongozi wa taasisi ya umma, alipaswa kufahamu kuwa barua na nyaraka ni siri za taasisi na hazitakiwi kusambazwa kwa wasiohusika. Aidha kwa nafasi yake kama wakili na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF alitegemewa kuwa mstari wa mbele katika kusimamia utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu za Shirikisho. Kitendo hicho ni kinyume na ibara ya 12(1)(b) ya Katiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ya Mwaka 2013 (kama ilivyorekebishwa Mwaka 2015) inayosema “Every member of TFF shall have the following obligations; to be loyal to TFF, meaning, in particular, that members must abstain from any actions contrary to the interest of TFF” na kifungu cha 16(1)&(2) cha Kanuni za Maadili za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Toleo la 2013 kinachotamka “(1) depending on their function, information of a confidential nature divulged to persons bound by this Code while performing their duties shall be treated as confidental or sectret by them as an expression of loyalty, if the information is given with the understanding or communication of confidentiality and is consistent with the TFF principles; (2) the obligation to respect confidentiaity survives the termaination of any relationship which makes a person subject to this Code”.

    ii).  Shitaka la pili
    Kamati imejiridhisha kuwa kitendo cha Ndugu Revocatus Kuuli, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, kutoa maelezo ya kusimamisha uchaguzi wa klabu ya Simba kwenye vyombo mbalimbali vya habari huku akituma nyaraka kutoka Shirikisho kwa waliowahi kuwa viongozi wa klabu hiyo, kinaonyesha kuwepo kwa mgongano wa kimaslahi. Aidha Ndugu Kuuli alimtumia barua ya TFF Ndugu Michael Wambura kuhusiana na mambo ya mpira huku akifahamu kuwa Ndugu Wambura amefungiwa kutojihusisha na masuala ya mpira wa miguu ndani na nje ya nchi maisha. Kamati iliona kuwa kitendo hicho cha Ndugu Kuuli kililenga katika kuvuruga amani iliyokuwepo katika klabu ya Simba na kingeweza kusababisha vurugu katika mpira wa miguu nchini. Kitendo hicho ni kinyume na kifungu cha 19(2) cha Kanuni za Maadili za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Toleo la 2013 kinachosema “persons bound by this Code shall avoid any situation that could lead to conflicts of interest. Conflicts of interest arise if persons bound by this Code have, or appear to have, private or personal interests that detract from their ability to perform their duties with integrity in an independent and purposeful  manner. Private or personal interests include gaining any possible advantage for the persons bound by this Code themselves, their family, relatives, friends and acquaintances”.

    iii).  Shitaka la tatu
    Kamati imejiridhisha kuwa vitendo hivi vya Ndugu Revocatus Kuuli, vimeshusha hadhi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kwa vile alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, ambayo ina jukumu la kusimamia upatikanaji wa viongozi bora wa mpira wa miguu. Ndugu Kuuli alikaririwa na kituo kimoja cha redio akisema kuwa hawezi kuhudhuria kikao cha Kamati ya Maadili ya TFF kwa vile “…hizo ni tuhuma za kipuuzi zinazoweza kufanywa na wapuuzi; mi siwezi kwenda kwenye kikao hicho nina kazi nyingi za kufanya…” Pia alisisitiza kuwa hana mpango wa kuwa kiongozi wa mpira wa miguu. 
    Kamati ilijiridhisha kuwa Ndugu Kuuli alitumiwa wito kupitia barua Kumb. Na. TFF/ADM/LM.791/2018 ya tarehe 29 Oktoba 2018. Barua hiyo ilitumwa kwa njia za ems, barua pepe na WhatsApp. Kutokana na kauli zake, inaonysha wazi kuwa Ndugu Kuuli alifanya vitendo hivyo kwa kudhamiria. Kitendo hicho ni kinyume na ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF ya Mwaka 2013 (kama ilivyorekebishwa Mwaka 2015) inayotamka kuwa “TFF members shall at all times comply with the following ethical principles: (1) to behave ethically and act with integrity in all situations, keeping in mind that a reputation for integrity is of the utmost importance to TFF and its objectives.”
    Baada ya kujiridhisha kuwa Ndugu Revocatus Kuuli amefanya makosa hayo, Kamati inamfungia kutojihusisha na masuala ya mpira wa miguu ndani na nje ya nchi maisha. Adhabu hii imetolewa kwa mujibu wa kifungu cha 73(8)(b) cha Kanuni za Maadili ya TFF Toleo la 2013, kwa kuzingatia uzito wa makosa yake, ambayo yangeweza kusababisha vurugu na sintofahamu katika mpira wa miguu nchini. 
    Kamati ilisikitishwa na kauli za kebehi, dharau na kashfa zilizokuwa zikitolewa na Ndugu Revocatus Kuuli kupitia vyombo mbalimbali vya habari. Kamati inaamini kuwa Ndugu Kuuli, akiwa kiongozi wa umma, anawajibika kuzingatia maadili ya utumishi wa umma ili kutoharibu taswira ya utumishi wa umma mbele ya jamii. Kitendo chake cha kuita tuhuma dhidi yake ni za kipuuzi na zinaweza kusikilizwa na wapuuzi siyo tu kimeshusha hadhi ya Shirikisho bali pia kimeudhalilisha mpira wa miguu. Aidha kwa nafasi yake kama wakili msomi, ilitarajiwa kuwa anaelewa misingi ya utawala wa sheria; hivyo hakupaswa kuzungumza na vyombo vya habari kwa lugha isiyopendeza na yenye maudhi; tena bila kuwa na mamlaka ya kufanya hivyo. Kwa kuzingatia nafasi yake ya uongozi katika utumishi wa Umma, Kamati inaiomba Sekretarieti ya TFF kuwasilisha mbele ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, vielelezo vyote vinavyoonyesha ukiukwaji wa maadili uliofanywa na Ndugu Revocatus Kuuli ili ijiridhishe kama hakuna ukiukwaji wa maadili ya umma au uvunjaji wa miiko ya uongozi.

    6.0               HITIMISHO
    Kamati inalishauri Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuongeza umakini wakati wa kufanya uteuzi wa viongozi wa Kamati mbalimbali ili kuepuka watu wasio na maadili kupata nafasi nyeti zenye kufanya maamuzi ya mpira wa miguu. Aidha Kamati inawaasa viongozi wa mpira nchini kuzingatia mipaka ya kazi yao ili kuepuka mgongano na migogoro ya kiutendaji. Vile vile viongozi wa mpira wa miguu wanashauriwa kuwa makini wanapotoa kauli zao wakati wanazungumza na vyombo vya habari.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YAMFUNGIA MAISHA KUTOJIHUSISHA NA SOKA WAKILI MSOMI REVOCATUSS KUULI ALIYEUWEKA MADARAKANI UONGOZI WA KARIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top