• HABARI MPYA

    Monday, November 05, 2018

    TFF YAWAAGIZA YANGA SC KUFANYA UCHAGUZI WA KUZIBA NAFASI ZA MANJI, SANGA NA WAJUMBE WANNE JANURI 13 MWAKANI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeitaka klabu ya Yanga SC kufanya Uchaguzi wa kuziba nafasi za viongozi wake waliojiuzulu ifikapo Januari 13 mwakani, 2019.
    Mwenyekiti mpya wa Kamati ya Uchaguzi TFF, Malangwe Mchungahela amewaambia Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam kwamba Yanga inatakiwa kuanza mchakato wa uchaguzi wake ambao lazima ufanyike Januari 13, 2019.
    Mchungahela amezitaja nafasi zitakazogombewa katika uchaguzi huo ni za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji.
    Na hiyo inafuatia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuiagiza Yanga kuitisha uchaguzi wa kujaza nafasi za viongozi waliojiuzulu ili kuwa na safu imara ya uongozi.

    Mwenyekiti mpya wa Kamati ya Uchaguzi TFF, Malangwe Mchungahela ameitaka Yanga kufanya uchaguzi wake  Januari 13 mwakani

    Kwa mujibu wa kalenda ya Uchaguzi, Novemba 5 hasi 7, 2018 Yanga watatakiwa kutangaza mchakato wa Uchaguzi na kubandika kwenye mbao za matangazo, zoezi ambalo litafanywa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
    Novemba 8- 13,2018 kuchukua na kurudisha fomu za kuomba uongozi, fomu ambazo zitatolewa Makao Makuu ya Klabu ya Yanga SC na fomu nyingine zitapelekwa Makao Makuu ya TFF Karume,Ilala kwa wengine kuchun kulia hapo.
    Novemba 21-22, 2018 itakuwa kipindi cha kuweka pingamizi kwa Wagombea
    Novemba 24-27, 2018 itakuwa kipindi cha kupitia mapingamizi na kufanya usahili wa Wagombea,zoezi ambalo litafanywa na Kamati ya Uchaguzi.
    Novemba 28-30, 2018 kutangaza na kubandika kwenye mbao za matangazo matokeo ya awali ya usahili.
    Orodha ya mwisho ya Wagombea itachapishwa,kutangazwa na kubandikwa kwenye mbao za matangazo Januari 3-5,2019.
    Kipindi cha Kampeni kwa Wagombea kitakuwa kuanzia Januari 6-11,2019.
    Kutakana na mapungufu ya Kamati ya utendaji na mapungufu ya kamati ya Uchaguzi ya Yanga SC na kwa kuzingatia maelekezo ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT), uchaguzi huu utasimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kushirikiana na uongozi wa Yanga SC.
    BMT ilisema katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari wiki iliyopita kwamba, Yanga imebaki na Wajumbe sita kati ya 13 waliochaguliwa katika uchaguzi wa Juni 12, mwaka 2016 Dar es Salaam, hivyo inatakiwa kufanya uchaguzi wa kuziba nafasi zilizo wazi katika uongozi kwa mujibu wa katiba yao.
    Tamko la BMT lilifuatia vikao vilivyohusisha Wazee, Wanachama, Viongozi na wadau mbalimbali wa klabu hiyo vilivyohudhuriwa hadi na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.
    BMT ilisema kwamba uchaguzi huo utasimamiwa na TFF kutokana na mapungufu ya Akidi katika Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo.
    Na kuhusu mkanganyiko wa kadi za uanachama, BMT imeagiza lifanyike zoezi la kusajili wanachama wenye kadi za zamani ili kurejesha umoja na mshikamano ndani ya klabu.  
    Yanga SC imebaki na Wajumbe sita tu wa Kamati ya Utendahi baada ya viongozi wote wakuu kujiuzulu kwa wakati tofauti, wakiwemo aliyekuwa Mwenyekiti, Yussuf Mehboob Manji na Makamu wake, Clement Sanga.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YAWAAGIZA YANGA SC KUFANYA UCHAGUZI WA KUZIBA NAFASI ZA MANJI, SANGA NA WAJUMBE WANNE JANURI 13 MWAKANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top