• HABARI MPYA

    Tuesday, November 06, 2018

    TAIFA STARS WAMEONDOKA ALFAJIRI KWENDA KUWEKA KAMBI AFRIKA KUSINI KUJIANDAA NA LESOTHO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIKOSI cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kimeondoka Alfajiri ya leo kwenda mjini Blomofontein, Afrika Kusini kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Lesotho katikati ya mwezi huu kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon.
    Taifa Stars watakuwa wageni wa Mamba wa Lesotho Novemba 18, mwaka huu Uwanja wa Setsoto mjini Maseru katika mchezo wa Kundi L kufuzu AFCON ya mwakani na kuelekea mchezo huo, watakuwa kambini Afrika Kusini kwa siku 10.
    Wachezaji waliosafiri na Stars leo pamoja na makipa Aishi Manula wa Simba SC, Aaron Kalambo wa Tanzania Prisons, Beno Kakolanya wa Yanga SC na Benedictor Tinocco wa Mtibwa Sugar zote za nyumbani. 
    Mabeki ni Shomary Kapombe, Erasto Nyoni wa Simba SC, Ally ‘Sonso’ Abdulkarim wa Lipuli FC, Kelvin Yondan, Gardiel Michael wa Yanga SC, Aggrey Morris na Abdallah Kheri wa Azam FC, zoyte za nyumbani.
    Viungo ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya wa Azam FC, Salum Kimenya wa Tanzania Prisons, Feisal Salum wa Yanga SC, Jonas Mkude na Shiza Kichuya wa Simba SC zote za nyumbani na washambuliaji ni Thomas Ulimwengu aliye huru baada ya kuvunja mkataba na Al Hilal ya Sudan mwishoni mwa wiki, John Bocco wa Simba SC na Yahya Zayed wa Azam FC zote za nyumbani.
    Kikosi hicho chini ya makocha Emmanuel Amunike anayesaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi na mzawa Hemed Suleiman ‘Morocco’, Meneja Danny Msangi, Mtunza Vifaa Ally Ruvu na Madaktari Richard Yomba na Gilbert Kigadya kitaingia kambini nchini Afrika Kusini wiki ijayo kabla ya kwenda Lesotho siku moja kabla ya mchezo wa Novemba 18.
    Wachezaji wanaocheza nje mabeki ni; Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia, Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, viungo ni Himid Mao wa Petrojet ya Misri, Simon Msuva wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, na washambuliaji Nahodha Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji, Shaaban Iddi Chilunda wa CD Tenerife ya Hispania na Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana watajiunga na timu wiki ijayo.
    Baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde Oktoba 16 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Taifa Stars sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi L kuwania tiketi ya Cameroon mwakani, ikifikisha pointi tano baada ya kucheza mechi nne, ikifungwa moja na sare mbili. 
    Uganda ambayo siku hiyo iliifunga tena Lesotho 2-0 mjini Maseru, ndiyo inaongoza kundi hilo kwa pointi zake 10 za mechi nne, wakati Cape Verde inabaki na pointi zake nne katika nafasi ya tatu. Lesotho ndiyo inashika mkia kwa pointi zake mbili.   
    Taifa Stars itahitimisha mechi zake za Kundi L kwa kumenyana na Uganda Machi 22 mwakani, miezi miwili tu kabla ya kuanza kwa AFCON ya mwakani.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS WAMEONDOKA ALFAJIRI KWENDA KUWEKA KAMBI AFRIKA KUSINI KUJIANDAA NA LESOTHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top