• HABARI MPYA

  Friday, November 09, 2018

  REFA MJERUMANI AMLIMA KADI YA NJANO SAMATTA GENK IKILAZIMISHWA SARE YA 1-1 NA AKINA PEPE ULAYA

  Na Mwandishi Wetu, GENK
  REFA Mjerumani, Tobias Stieler jana amemuonyesha kadi ya njano mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta timu yake, KRC Genk ikilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Besiktas ya Uturuki katika mchezo wa Kundi I UEFA Europa League.
  Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk, Samatta alikuwa na wakati mgumu mbele ya mabeki wa Besiktas walioongozwa na mkongwe, beki wa zamani wa Real Madrid, Kleper Laveran Lima Ferreira maarufu Pepe na kisiki cha Croatia, Domagoj Vida na haikuwa ajabu alipoonyeshwa kadi ya njano dakika ya 35. 
  Nahodha wa Tanzania, Samatta naye akamsababishia kadi ya njano pia, beki wa Ureno Pepe dakika ya 80, wakati mchezaji mwingine aliyeonyeshwa kadi ya njano jana ni Necip Uysal dakika ya 15.
  Refa Mjerumani, Tobias Stieler (kulia) akimuonyesha kadi ya njano mshambuliaji wa Genk, Mbwana Samatta jana 


  Mshambuliaji wa Genk, Mbwana Samatta akijitetea mbele ya refa Tobias Stieler kabla ya kuonyeshwa kadi ya njano 

  Katika mchezo huo, Besiktas walitangulia kwa bao la kiungo mkongwe wa Ureno, Ricardo Quaresma dakika ya 16 akimalizia pasi ya Mustafa Pektemek, kabla ya Sander Berge kuisawazishia Genk dakika ya 87, akimalizia pasi ya Bryan Heynen.
  Kwa matokeo hayo, Genk inapanda kileleni mwa Kundi I ikifikisha pointi saba baada ya kucheza mechi nne, ikifuatiwa na Sarpsborg yenye pointi tano sawa na Malmo FF wakati Besiktas yenye pointi nne inashika mkia baada ya timu zote kucheza mechi nne.
  Na Samatta jana amefikisha mechi 128 katika mashindano yote tangu amejiunga na Genk Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na amefunga jumla ya mabao 51.
  Katika Ligi ya Ubelgiji amecheza mechi 99 na kufunga mabao 36, Kombe la Ubelgiji mechi nane mabao mawili na Europa League mechi 21 mabao 14.
  Kikosi cha KRC Genk kilikuwa; Vukovic, Maehle, Aidoo, Dewaest, Uronen, Heynen, Malinovskyi/Berge dk59, Pozuelo, Ndongala/Ingvartsen dk89, Paintsil/Fiolic dk66 na Samatta.
  Besiktas: Zengin, Tokoz/Ljajic dk73, Pepe, Vida, Erkin, Uysal, Ozyakup/Vagner Love dk90, Medel, Quaresma, Lens/Pektemek dk12 na Babel.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: REFA MJERUMANI AMLIMA KADI YA NJANO SAMATTA GENK IKILAZIMISHWA SARE YA 1-1 NA AKINA PEPE ULAYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top