• HABARI MPYA

  Thursday, November 08, 2018

  OKWI MCHEZAJI BORA LIGI KUU MWEZI OKTOBA NA PLUIJM AMBWAGA PATRICK J AUSSEMS WA SIMBA KUWA KOCHA BORA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi wa Simba SC ya Dar es Salaam ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi Oktoba wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
  Taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) leo imesema kwamba, Okwi amekuwa Mchezaji Bora wa Oktoba baada ya kuwapiku Eliud Ambokile wa Mbeya City ya Mbeya na Yahya Zayed wa Azam FC ya Dar es Salaam pia. 
  Okwi anakuwa mchezaji bora wa tatu wa msimu, baada ya mchezaji mwenzake wa Simba SC, Meddie Kagere kushinda tuzo ya Agosti na Ambokile kunyakua ya Septemba. 
  Hiyo ni baada ya uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya TPL inayotolewa na TFF, kutokana na mapendekezo kutoka kwa makocha waliopo viwanja mbalimbali ambavyo ligi hiyo inachezwa msimu huu. 
  Emmanuel Okwi wa Simba SC yameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi mwezi Oktoba

  Mholanzi Hans van der Pluijm ameshinda tuzo ya Kocha Bora wa mwezi Oktoba Ligi Kuu

  Kwa mwezi huo Oktoba timu 18 zilicheza michezo mitano kila moja,  isipokuwa Simba na Yanga zilizocheza mechi nne. 
  Katika michezo hiyo minne ambayo Simba ilicheza, Okwi raia wa Uganda alitoa mchango mkubwa kwa kupata pointi 12  kwa kushinda michezo yote na kumaliza ikiwa nafasi ya pili, huku Okwi akifunga mabao 7 kwa mwezi huo, matatu akifunga katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting ambao Simba iliibuka na ushindi wa mabao 5-0.
  Kwa upande wa Ambokile naye alitoa mchango mkubwa kwa Mbeya City kufanikisha kupata pointi 11 baada ya kushinda michezo mitatu na kutoka sare miwili na kushika nafasi ya nane katika msimamo, akifunga mabao manne.
  Kuhusu Zayed alitoa mchango mkubwa kwa Azam akifunga mabao matatu katika michezo mitano ambayo Azam ilicheza ikishinda yote na kupata pointi 15 ikishika nafasi ya kwanza. Aidha, taarifa hiyo imesema kwamba Kocha wa Azam FC, Mholanzi Hans van der Pluijm ameshinda tuzo ya Kocha Bora wa mwezi Oktoba baada ya kuiwezesha klabu yake kuongoza ligi hiyo.
  Pluijm, kocha wa zamani wa Yanga ya Dar es Salaam pia na Singida United ya Singida, amewashinda Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems na wa Mbeya City, Mrundi Ramadhani Nsazwarimo kutwaa tuzo hiyo.
  Pluijm aliiongoza timu yake kupata pointi 15 baada ya kushinda michezo yote mitano iliyocheza na kushika nafasi ya kwanza, huku Aussems akiiongoza Simba kushinda michezo yote minne iliyocheza hivyo kupata pointi 12 na kushika nafasi ya pili, wakati Nsazwarimo alipata pointi 11 akishinda michezo mitatu na kutoka sare mitatu akiiwezesha timu yake kupanda hadi nafasi ya nane.
  Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara ina utaratibu wa kuwazawadia wachezaji bora wa kila mwezi, huku pia mwisho wa msimu kukiwa na tuzo mbalimbali zinazohusu ligi hiyo, ambapo msimu wa mwaka 2017/2018 kulikuwa tuzo 16 zilitolewa kwa washindi wa kada mbalimbali, ambapo kwa ushindi huo Okwi atazawadiwa tuzo, king’amuzi kutoka Azam na Sh milioni moja kwa kuibuka Mchezaji Bora wa mwezi. 
  Makocha wengine walioshinda tuzo ya Kocha Bora wa Ligi Kuu mwezi huu ni mzawa, Amri Said ‘Stam’ wa Mbao FC ya mjini Mwanzana mwezi Agosti na Mwinyi Zahera kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wa Yanga mwezi Septemba.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: OKWI MCHEZAJI BORA LIGI KUU MWEZI OKTOBA NA PLUIJM AMBWAGA PATRICK J AUSSEMS WA SIMBA KUWA KOCHA BORA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top