• HABARI MPYA

  Monday, November 12, 2018

  OBREY CHIRWA AANZA KAZI KWA KISHINDO AZAM FC, AKUTANA TENA NA PACHA WAKE WA TANGU PLATINUMS, DONALD NGOMA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI mpya wa Azam FC, Obrey Chirwa, leo asubuhi ameanza kufanya mazoezi kwa mara ya kwanza kwenye timu yake hiyo mpya.
  Staa huyo wa zamani wa Yanga SC ya Dar es Salaam na FC Platinum ya Zimbabwe, amejiunga na Azam FC akitokea Nogoom ya Misri kwa usajili huru baada ya kufikia makubaliano ya kuvunja mkataba na timu hiyo.
  Chirwa amejumuika mazoezini kwa mara ya kwanza na wenzake, wakati timu hiyo ikianza rasmi kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) dhidi ya Ruvu Shooting utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Novemba 22 mwaka huu.
  Obrey Chirwa akiwa mazoezini na timu yake mpya, Azam FC leo asubuhi Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam 
  Obrey Chirwa akifanya mazoezi kwa bidii leo asubuhi Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam 
  Obrey Chirwa amekutana tena na mchezaji mwenzake wa zamani wa FC Platinums ya Zimbabwe na Yanga SC, Donald Ngoma
  Obrey Chirwa atafanya kazi tena na kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm waliyekuwa naye Yanga SC 

  Kwa mara nyingine tena Cirwa anaungana na rafiki yake wa siku nyingi, Donald Ngoma, ambaye walicheza naye Platinum ya Zimbabwe kwa takribani miaka sita kabla ya kufanya tena kazi pamoja wakiwa Yanga na sasa Azam FC, mara zote mbili hapa Tanzania wakiunganishwa na Kocha Mkuu, Hans Van Der Pluijm, ambaye kwa sasa anaifundisha Azam FC.
  Mazoezi hayo yaliyosimamiwa na Kocha Pluijm, yalikuwa ni makali lengo kuu ni kurudisha ufiti kwa wachezaji baada ya mapumziko ya takribani siku sita.
  Aidha mazoezi hayo yalihudhuriwa na wachezaji wote ukiondoa sita waliojiunga na timu za Taifa, nahodha Aggrey Morris, Abdallah Kheri, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya, Yahya Zayd (wote Taifa Stars) huku Nickolas Wadada akiwa na Uganda ‘The Cranes’.
  Nyota mwingine Tafadzwa Kutinyu, ambaye alikuwemo mazoezini leo anatarajia kujiunga na timu ya Taifa ya Zimbabwe muda keshokutwa Jumatano.
  Wakati mechi za ligi zikielekea raundi ya 14, kikosi cha Azam FC hadi sasa kinashika usukani kikiwa na pointi 30 baada ya kushinda mechi tisa na sare tatu huku wakiwa hawajapoteza mchezo wowote na nyavu zikitikiswa mara mbili tu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: OBREY CHIRWA AANZA KAZI KWA KISHINDO AZAM FC, AKUTANA TENA NA PACHA WAKE WA TANGU PLATINUMS, DONALD NGOMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top