• HABARI MPYA

    Monday, November 12, 2018

    TAIFA STARS KUONDOKA AFRIKA KUSINI IJUMAA KUIFUATA LESOTHO KWA AJILI YA MCHEZO WA JUMAPILI KUFUZU AFCON

    Na Mwandishi Wetu, BLOEMFONTEIN
    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars itaondoka mjini Bloemfontein, Afrika Kusini Ijumaa kwenda Maseru kwa basi kwa ajili ya mchezo wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon dhidi ya wenyeji, Lesotho Jumapili.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo, Meneja wa Taifa Stars, Danny Msangi amesema kwamba wachezaji wanne wanaocheza nje walikuwa wamewasili hadi leo asubuhi na mchana huu wanatarajiwa kumpokea mwingine.
    Msangi amewataja wachezaji waliowasili ni mabeki Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia na washambuliaji Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana na Thomas Ulimwengu aliyevunja mkataba na El Hilal ya Sudan, ambaye alikuwa wa kwanza kuwasili kambini tangu Dar es Salaam.
    Meneja wa Taifa Stars, Danny Msangi (kushoto) akiwa na wachezaji wa kusini mwa Afrika, Hassan Kessy, Abdi Banda na Rashid Mandawa mjini Bloemfontein jana 
    Mshambuliaji wa CD Tenerife, Shaaban Iddi Chilunda yupo nyumbani Tanzania kushughulikia pasipoti

    Msangi amesema kwamba mchana wa leo anatarajia kumpokea kiungo wa Petrojet ya Misri, Himid Mao wakati kesho watampokea kiungo mshambuliaji, Simon Msuva wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco.
    Msangi amesema kwamba mshambuliaji Shaaban Iddi Chilunda wa CD Tenerife ya Hispania anaweza kuwasili leo kutoka Dar es Salaam alipokwenda kurekebisha pasipoti yake.
    Nahodha, Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji yeye kwa sababu hayumo kwenye programu za mchezo na Lesotho Jumapili kuokana na adhabu ya kadi za njano anayotumikia, Msangi amesema atajiunga na timu Alhamisi kuongeza morali ya kambi.
    Wachezaji wengine waliopo kambini ni makipa Aishi Manula wa Simba SC, Aaron Kalambo wa Tanzania Prisons, Beno Kakolanya wa Yanga SC na Benedictor Tinocco wa Mtibwa Sugar zote za nyumbani.     
    Mabeki ni Shomary Kapombe, Erasto Nyoni wa Simba SC, Ally ‘Sonso’ Abdulkarim wa Lipuli FC, Kelvin Yondan, Gardiel Michael wa Yanga SC, Aggrey Morris na Abdallah Kheri wa Azam FC, zoyte za nyumbani.
    Viungo ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya wa Azam FC, Salum Kimenya wa Tanzania Prisons, Feisal Salum wa Yanga SC, Jonas Mkude na Shiza Kichuya wa Simba SC zote za nyumbani na washambuliaji ni John Bocco wa Simba SC na Yahya Zayed wa Azam FC zote za nyumbani.
    Kikosi hicho chini ya makocha Emmanuel Amunike anayesaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi na mzawa Hemed Suleiman ‘Morocco’, Meneja Danny Msangi, Mtunza Vifaa Ally Ruvu na Madaktari Richard Yomba na Gilbert Kigadya kitaingia kambini nchini Afrika Kusini wiki ijayo kabla ya kwenda Lesotho siku moja kabla ya mchezo wa Novemba 18.
    Taifa Stars inahitaji ushindi dhidi ya Lesotho Jumapili ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu AFCON ya pili tu kihistoria kwao tangu ile ya mwaka 1980 nchini Nigeria.
    Kwa sasa, Stars inashika nafasi ya pili kwenye Kundi L kwa pointi zake tano baada ya kucheza mechi nne, ikishinda moja, sare moja na kufungwa moja, ikiizidi kwa pointi moja Cape Verde. 
    Uganda ambayo ni kama imekwishafuzu, inaongoza kundi hilo kwa pointi zake 10 za mechi tano pia, wakati Lesotho yenye pointi mbili ni ya mwisho. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS KUONDOKA AFRIKA KUSINI IJUMAA KUIFUATA LESOTHO KWA AJILI YA MCHEZO WA JUMAPILI KUFUZU AFCON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top