• HABARI MPYA

    Monday, November 12, 2018

    YANGA SC WAITISHA MKUTANO WA DHARULA NOVEMBA 24 DAR…NA JUMATANO WANA MECHI YA KIRAFIKI NA REHA FC

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Utendaji ya klabu ya Yanga imeitisha mkutano wa dharula wa wanachama wake ambao umepangwa kufanyika Novemba 24 katika ukumbi utakaotajwa baadaye.
    Taarifa fupi ya klabu leo haikuwa na maelezo zaidi kuhusu mkutano huo, lakini inakuja siku moja baada ya Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Yanga SC kuthibitisha kurejea kwa Yussuf Manji kuendelea kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo.
    Mkuchika alisema jana katika mkutano na Waandishi wa Habari makao makuu ya klabu kwamba kufuatia tamko la kurejea kwa Manji, nafasi ya Uenyekiti haitajazwa katika uchaguzi ujao Januari 13, mwakani.
    Mkuchika aliionyesha na kuwasomea Waandishi wa Habari barua iliyoandikwa na Manji kujibu ombi la wanachama wa klabu hiyo kumtaka aendelee na nafasi hiyo baada ya yeye kuandika barua ya kujiuzulu Mei mwaka jana baada ya miaka 11 akianza kama mfadhili mwaka 2006.

    Yanga imeitisha mkutano wa dharula wa wanachama wake Novemba 24  

    Wanachama wa Yanga walikataa ombi la Manji kujiuzulu katika mkutano wa Juni 10, mwaka huu Bwalo la Maofisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay mjini Dar es Salaam.
    “Kifupi anasema, nimepokea uamuzi wa wanachama wa Yanga, kwa bahati mbaya kipindi ninachoandikiwa mimi nipo kwenye matibabu, tarehe 15 Desemba madaktari wangu wanasema nitakuwa nimekamilika. Kwa hiyo pamoja na kwamba nimerudi kama Mwenyekiti, nitafanya kazi za kwenda ofisini kila mara kuanzia tarehe 15 Januari,”amesema Mkuchika akiisoma barua hiyo. 
    Mkuchika amesema Januari 15 Manji ataanza rasmi kazi za Yanga na kwenye makampuni yake baada ya kupitia kipindi kirefu cha misukosuko na Serikali kuanzia Januari hadi Oktoba mwaka jana, kwanza akikamatwa na kuwekwa ndani kwa tuhuma za kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya na baadaye kuwekwa rumande akidaiwa kumiliki pasipoti mbili na uhujumu uchumi, kesi ambazo zote zilifutwa.
    Katika hatua nyingine, Mkuchika amepinga uchaguzi wa klabu hiyo kusimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    “Suala lingine ambalo limeleta sitofahamu, ni uchaguzi wa Yanga kusimamiwa na TFF, kila klabu iliyosajiliwa kwa Msajili ina taratibu zake za kuwachagua viongozi wake, sijui kama itaanza Yanga mara ya kwanza,”.
    “Tumewaita viongozi wa kamati ya Utendaji wametuambia Kamati ya uchaguzi wanayo, ipo hai, lakini sisi Baraza la wadhamini tukasema, hata kama Kamati ya Uchaguzi ya Yanga haipo, wanatakiwa waunde Kamati ya uchaguzi ili isimamie uchaguzi. Uchaguzi wa Yanga kusimamiwa na Kamati ya uchaguzi isiyo ya Yanga tunavunja katiba ya Yanga,” alisema Mkuchika, ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora. 
    Uchaguzi mdogo wa Yanga SC kujaza nafasi za viongozi waliojiuzulu baadaa ya kuchaguliwa Juni mwaka 2016 unatarajiwa kufanyika Januari 13 mwakani na baada ya kurejea kwa Manji, nafasi zitakazojazwa ni Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na Wajumbe wanne, Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Hashim Abdallah waliojiuzulu.  
    Waliobaki katika Kamati ya Utendaji pamoja na Manji ni Wajumbe wanne, Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala, Samuel Lukumay na Hussein Nyika.
    Fomu za wagombea zinatolewa makao makuu ya klabu Sh. 200,000 kwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti na Sh. 100,000 kwa Ujumbe.
    Wakati huo huo: Klabu ya Yanga itakuwa na mchezo wa kirafiki Jumatano dhidi ya Reha FC ya Daraja la Kwanza Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
    Mechi hiyo inafuatia jana timu hiyo kupata ushindi wa 1-0 kwenye mchezo mwingine wa kirafiki dhidi ya African Lyon Uwanja wa Uhuru pia.
    Na mfungaji wa bao hilo, kiungo Pius Charles Buswita leo amepokea taarifa za kufiwa na motto wake, kwao Musoma mkoani Mara.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WAITISHA MKUTANO WA DHARULA NOVEMBA 24 DAR…NA JUMATANO WANA MECHI YA KIRAFIKI NA REHA FC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top