• HABARI MPYA

  Wednesday, November 07, 2018

  KAMATI YA MAREKEBISHO YA KATIBA TASWA YAANZA MCHAKATO IKIOMBA USHIRIKIANO WA WANACHAMA WAKE ILI IKAMILISHE ZOEZI MAPEMA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAMATI ya marekebisho ya Katiba ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) imeanza mchakato kuhusu marekebisho ya katiba ya chama hicho kama ilivyoagizwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT). 
  Katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari leo, Katibu Mkuu TASWA Amir Mhando amesema kwamba, Kamati ya Katiba inayoongozwa na Mwenyeketi wa zamani wa chama hicho, Boniface Wambura inaomba ushirikiano wa waandishi wote wa habari za michezo nchini kufanikisha jukumu hilo kwa wakati uliopangwa na BMT,  ili chama kifanye Uchaguzi Mkuu na kupata viongozi wapya. 
  Mhando amesema kutokana na suala la muda kuwa mfupi, Kamati imeandaa utaratibu wa kupokea maoni ya waandishi wa habari za michezo kwa njia mbalimbali kabla ya kuiwasilisha kwa Kamati ya Utendaji ya TASWA kupata baraka na kuitisha mkutano wa pamoja wa wadau kupitisha rasimu ya katiba hiyo. 
  Katibu Mkuu TASWA, Amir Mhando (kulia) akiwa na Mwenyeketi wa chama hicho, Juma Pinto (kushoto)

  "Wadau wenye maoni kuhusu mambo wanayotaka yaongezwe au yapunguzwe katika Katiba ya sasa ya TASWA watume maoni yao kwa email ifuatayo: katibataswatz@yahoo.com, katibataswa2018@yahoo.com na mwisho wa kupokea maoni ni Jumanne Novemba 13, 2018. 
  Pia wanaweza kufanya mawasiliano kwa ajili ya kupata nakala ya Katiba kwa Katibu Msaidizi wa Kamati, Gift Macha kwa email machagift@gmail.com,"amesema Mhando. 
  Amesema Kamati ya Katiba ya TASWA imeundwa kutokana na agizo la Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe aliyeitaka BMT isitishe uchaguzi wa TASWA uliokuwa umepangwa kufanyika Novemba 25 mwaka huu na badala yake BMT ikutane na viongozi wa TASWA pamoja na baadhi ya wanahabari wa michezo kuona namna ya kuifanyia marekebisho Katiba ya TASWA iendane na wakati. 
  Licha ya Wambura ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), viongozi wengine ni Katibu wa Kamati Amir Mhando ambaye pia ni Katibu Mkuu wa TASWA na mwanahabari Gift Macha ambaye ni Katibu Msaidizi wa Kamati. 
  Wajumbe ni Katibu Mkuu wa zamani wa TASWA, Abdul Mohammed, Mhazini wa zamani wa TASWA, Nasongelya Kilyinga na wanahabari Thabit Zacharia na Devotha Kihwelu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAMATI YA MAREKEBISHO YA KATIBA TASWA YAANZA MCHAKATO IKIOMBA USHIRIKIANO WA WANACHAMA WAKE ILI IKAMILISHE ZOEZI MAPEMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top