• HABARI MPYA

    Friday, November 09, 2018

    KAKOLANYA NA YAHYA ZAYED HATARINI KUWAKOSA LESOTHO BAADA YA KUUMIA MAZOEZINI TAIFA STARS LEO AFRIKA KUSINI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIPA Beno Kakolanya Yanga SC na mshambuliaji Yahya Zayed wa Azam FC wameibua hofu katika kambi ya timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars baada ya kuumia leo asubuhi mjini Bloemofontein nchini Afrika Kusini. Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Mario Ndimbo amesema kwamba Taifa Stars lo imeendelea na maandalizi yake kuelekea mchezo wa kutafuta tiketi ya kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2019 dhidi ya Lesotho Novemba 18 mjini Maseru.
    Na bahati mbaya katika mazoezi hayo, kipa Beno Kakolanya na mshambuliaji Yahya Zayed walipumzishwa baada ya kugongana, ingawa taarifa ya madaktari inasema wachezaji hao wataendelea na mazoezi kuanzia kesho.

    Wachezaji wanaocheza nje wataanza kuripoti kambini Jumapili Novemba 11,2018. Wanaotarajiwa kuanza kuripoti ni Ramadhan Kessy(Nkamia,Zambia),Himid Mao (Petrojet,Misri),Rashid Mandawa(BDF,Botswana) na Abdi Banda (Baroka, Afrika Kusini) n waliobaki wataripoti kuanzia Novemba 12.
    Taifa Stars watakuwa wageni wa Mamba wa Lesotho Novemba 18, mwaka huu Uwanja wa Setsoto mjini Maseru katika mchezo wa Kundi L kufuzu AFCON ya mwakani na kuelekea mchezo huo, wameweka kambi Afrika Kusini kwa siku 10 tangu Jumanne.
    Wachezaji waliopo kambini na Stars ni makipa Aishi Manula wa Simba SC, Aaron Kalambo wa Tanzania Prisons, Beno Kakolanya wa Yanga SC na Benedictor Tinocco wa Mtibwa Sugar zote za nyumbani.     
    Mabeki ni Shomary Kapombe, Erasto Nyoni wa Simba SC, Ally ‘Sonso’ Abdulkarim wa Lipuli FC, Kelvin Yondan, Gardiel Michael wa Yanga SC, Aggrey Morris na Abdallah Kheri wa Azam FC, zoyte za nyumbani.
    Viungo ni Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya wa Azam FC, Salum Kimenya wa Tanzania Prisons, Feisal Salum wa Yanga SC, Jonas Mkude na Shiza Kichuya wa Simba SC zote za nyumbani na washambuliaji ni Thomas Ulimwengu aliye huru baada ya kuvunja mkataba na Al Hilal ya Sudan mwishoni mwa wiki, John Bocco wa Simba SC na Yahya Zayed wa Azam FC zote za nyumbani.
    Kikosi hicho chini ya makocha Emmanuel Amunike anayesaidiwa na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi na mzawa Hemed Suleiman ‘Morocco’, Meneja Danny Msangi, Mtunza Vifaa Ally Ruvu na Madaktari Richard Yomba na Gilbert Kigadya kitaingia kambini nchini Afrika Kusini wiki ijayo kabla ya kwenda Lesotho siku moja kabla ya mchezo wa Novemba 18.
    Wachezaji wanaocheza nje mabeki ni; Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia, Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, viungo ni Himid Mao wa Petrojet ya Misri, Simon Msuva wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, na washambuliaji Nahodha Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji, Shaaban Iddi Chilunda wa CD Tenerife ya Hispania na Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana watajiunga na timu wiki ijayo.
    Baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Cape Verde Oktoba 16 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, Taifa Stars sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi L kuwania tiketi ya Cameroon mwakani, ikifikisha pointi tano baada ya kucheza mechi nne, ikifungwa moja na sare mbili. 
    Uganda ambayo siku hiyo iliifunga tena Lesotho 2-0 mjini Maseru, ndiyo inaongoza kundi hilo kwa pointi zake 10 za mechi nne, wakati Cape Verde inabaki na pointi zake nne katika nafasi ya tatu. Lesotho ndiyo inashika mkia kwa pointi zake mbili.   
    Taifa Stars itahitimisha mechi zake za Kundi L kwa kumenyana na Uganda Machi 22 mwakani, miezi miwili tu kabla ya kuanza kwa AFCON ya mwakani.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAKOLANYA NA YAHYA ZAYED HATARINI KUWAKOSA LESOTHO BAADA YA KUUMIA MAZOEZINI TAIFA STARS LEO AFRIKA KUSINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top