• HABARI MPYA

    Saturday, November 10, 2018

    BILIONEA 'MO' DEWJI AKUTANA NA UONGOZI MPYA SIMBA SIKU MOJA BAADA YA CAF KUTOA RATIBA LIGI YA MABINGWA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MFANYABIASHARA Bilionea, Mohammed ‘Mo’ Dewji amekutana na Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo iliyochaguliwa katika uchaguzi Mkuu wa klabu uliofanyika Novemba 5 mjini Dar es Salaam.
    Kikao hicho kilihusisha viongozi waliomaliza muda wao, chini ya kaimu Rais Salum Abdallah ‘Try Again’ na Mdhamini wa klabu, Ramesh Patel. 
    Mo Dewji alitambulishwa rasmi Bodi ya Ukurugenzi ya Simba chini ya Mwenyekiti, Swedy Nkwabi na Wajumbe Hussein Kitta Mlinga, Dk. Zawadi Ally Kadunda, Suleiman Haroub Said, Mwina Mohammed Kaduguda na Asha Ramadhani Baraka.
    Bilionea Mohammed ‘Mo’ Dewji (kulia) akiwa na Mdhamini wa klabu ya Simba SC, Ramesh Patel (kushoto) kwenye kikao cha leo 

    Mo Dewji, Mbunge wa zamani wa Singida Mjini, kukubali kununua asilimia 49 za hisa za klabu ya Simba SC kulingana na maelekezo ya Serikali badala ya asilimia 51 alizotaka yeye awali katika mkutano Desemba 3, mwaka jana, ambao uliazimia kumfanya mwanahisa mkuu wa klabu katika mfumo mpya wa uendeshwaji.
    Mo pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 miezi miwili iliyopita, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.
    Wanachama 1320 walihudhuria mkutano huo wa Desemba 3, mwaka jana kutoka Dar es Salaam na mikoa jirani na kwa furaha ya ushindi huo, Mo Dewji alitoa ahadi 10 za kuleta mabadiliko makubwa, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa nyasi za asili na nyasi bandia pamoja na hosteli ya kisasa ya wachezaji.
    Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC na viongozi waliomaliza muda wao katika kikao cha leo
    Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC na viongozi waliomaliza muda wao katika kikao cha leo 

    Aliyekuwa Kaimu Rais wa Simba SC, Salum Abdallah 'Try Again' akiwa na Mjumbe mpya, Asha Baraka 

    Na uchaguzi wa Jumapili iliyopita Simba SC ulifanyika baada ya uongozi uliopita ulioingia madarakani juni 30, mwaka 2014 chini ya Rais, Evans Elieza Aveva, Makamu wa Rais, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Wajumbe Iddi Kajuna, Said Tully, Collins Frisch, Ally Suru na Jasmine Badour kumaliza muda wake.
    Lakini Aveva na Kaburu hawakufanikiwa kumalizia muda wao madarakani, kufuatia kuwekwa rumande katika gereza la Keko tangu Juni 29, mwaka jana kwa tuhuma za kughushi nyaraka, kesi ambayo bado inaendelea katika Mahakama ya Kisutu mjini Dar es Salaam.
    Na Julai 1, mwaka jana, Kamati ya Utendaji iliwateua ‘Try Again’ na Iddi Kajuna kukaimu nafasi za Aveva na Kaburu na hao ndiyo waliosimamia mchakato mzima wa mabadiliko ya klabu kuelekea uchaguzi huo.
    Mohammed Dewji akiwa katika picha ya pamoja na viongozi waliomaliza muda wao
    Mdhamini wa klabu, Ramesh Patel akitoa maelezo kwenye kikao cha leo

    Mjumbe wa Bodi ya Ukurugenzi, Mwina Kaduguda akizungumza kwenye kikao cha leo

    Nkwabi ambaye amekidhi matakwa ya Katiba mpya ya Simba SC kuwa na elimu ya Shahada sasa ataongoza Bodi ya Wakurugenzi itakayokuwa na Wajumbe wanane chini yake huku akiwa na mamlaka ya kuteua Wajumbe wengine wanne, kati yao mmoja lazima awe mwanamke ili kukamilisha Bodi ya Ukurugenzi ya watu wanane.
    Aidha, Mo Dewji anakutana na Bodi ya Ukurugenzi ya klabu siku moja tu baada ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutaja ratiba ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018- 2019, Simba ikipangiwa kuanza na Mbabane Swallows Swaziland katika Raundi ya Awali ya mchujo.
    Mohammed Dewji akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC na viongozi waliomaliza muda wao
    Mmoja wa Wajumbe waliohudhuria kikao hicho wakizungumza
    Aliyekuwa Kaimu Rais, Salum Abdallah 'Try Again' (kulia) akimpa somo Mwenyekiti wa Bodi, Swedi Nkwabi

    Na Wekundu wa Msimbazi, wakifanikiwa kuvuka mtihani huo, watakwenda hatua ya mwisho ya mchujo kuwania kuingia hatua ya makundi ya michuano hiyo, ambako watamenyana na mshindi kati ya Uniao Desportiva Do Songo ya Msumbiji na Nkana FC ya Zambia, anayochezea beki wake wa zamani, Mtanzania, Hassan Kessy aliyewahi kucheza na Yanga pia.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BILIONEA 'MO' DEWJI AKUTANA NA UONGOZI MPYA SIMBA SIKU MOJA BAADA YA CAF KUTOA RATIBA LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top