• HABARI MPYA

  Friday, October 19, 2018

  RAIS DK. JOHN POMBE MAGUFULI KULA CHAKULA CHA MCHANA NA WACHEZAJI TAIFA STARS IKULU DAR ES SALAAM LEO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Pombe Joseph Magufuli leo mchana atakutana na wachezaji wa timu ya taifa, Taifa Stars na kula nao chakula cha mchana Ikulu mjini Dar es Salaam.
  Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Rais, (DPC), Gerson Partinus Msigwa amesema katika taarifa yake fupi leo asubuhi kwamba, “Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 19 Oktoba, 2018 atakutana na wachezaji wa Timu ya Taifa (Taifa Stars) na baadaye kula nao chakula cha mchana Ikulu Jijini Dar es Salaam,”.
  Na hiyo inakuja siku mbili tu baada ya Taifa Stars kufufua matumaini ya kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani kufuata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde kwenye mchezo wa Kundi L Jumanne Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

  Rais Dk John Pombe Joseph Magufuli leo atakula chakula cha mchana na wachezaji wa Taifa Stars

  Ushindi huo wa kwanza kwenye mashindano haya, unaifanya Taifa Stars ijisogeze hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi hilo, ikifikisha pointi tano baada ya kucheza mechi nne, ikifungwa moja na sare mbili. 
  Uganda ambayo siku hiyo iliifunga tena Lesotho 2-0 mjini Maseru, ndiyo inaongoza kundi hilo kwa pointi zake 10 za mechi nne, wakati Cape Verde inabaki na pointi zake nne katika nafasi ya tatu. Lesotho ndiyo inashika mkia kwa pointi zake mbili.   
  Shujaa wa Tanzania Jumanne alikuwa Nahodha Mbwana Ally Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji aliyefunga bao moja na kuseti moja katika ushindi huo, ingawa pia alikosa penalti. 
  Samatta alianza kumsetia kiungo mshambuliaji wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Simon Msuva dakika ya 29 kabla ya yeye mwenyewe kufunga bao la pili dakika ya 58 kwa shuti la mbali baada ya  pasi ya kiungo wa Azam FC, Mudathir Yahya Abbas.
  Awali, dakika ya 22 Samatta aligongesha mwamba wa juu mkwaju wa penalti uliotolewa na refa Michael Gasingwa wa Rwanda baada ya beki wa MOL Vidi FC ya Hungary Ianique dos Santos Tavares ‘Stopira’ kumuangusha Msuva kwenye boksi.
  Taifa Stars itasafiri kuifuata Lesotho mwezi ujao kabla ya kukamilisha mechi za Kundi L kwa kumenyana na Uganda Machi mwakani, miezi miwili tu kabla ya kuanza kwa AFCON ya mwakani.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: RAIS DK. JOHN POMBE MAGUFULI KULA CHAKULA CHA MCHANA NA WACHEZAJI TAIFA STARS IKULU DAR ES SALAAM LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top