• HABARI MPYA

    Thursday, October 25, 2018

    BAO LA DAKIKA ZA MWISHONI LA ‘FEI TOTO’ LAIPA USHINDI YANGA SC DHIDI YA KMC NA KURUDI JUU LIGI KUU

    Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imarejea nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya KMC FC ya Kinondoni usiku wa leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Yanga SC sasa inafikisha pointi 22 baada ya ushindi huo kutokana na mechi nane tu ilizocheza, ikizidiwa pointi mbili tu na Azam FC inayoongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 24 za mechi 10, wakati mabingwa watetezi, Simba SC sasa ni wa tatu kwa pointi zao 20 za mechi tisa.
    Haukuwa ushindi mwepesi, kwani iliwalazimu mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu kusubiri hadi dakika ya 89 kupata bao lao pekee la ushindi.
    Bao hilo limefungwa na kiungo Mzanzibar, Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ kwa shuti la kiufundi la mpira wa adhabu baada ya Matheo Anthony kuangushwa karibu na eneo la hatari.

    Wachezaji wa Yanga SC wakimpongeza Feisal Salum baada ya kufunga bao la ushindi dakika ya 89

    KMC ikiongozwa na kipa mkongwe, Juma Kaseja aliyekuwa anacheza dhidi ya timu yake ya zamani, ilifanikiwa kuwabana Yanga kwa sehemu kubwa ya mchezo huo.
    Ilibidi kocha Mwinyi Zahera kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) apunguze viungo na kuongeza washambuliaji ili kuongeza kasi ya mashambulizi dakika zxa mwishoni.
    KMC waliokuwa wakicheza kwa kujihami zaidi na kushambulia kwa kushitukiza, mara mbili walikaribia kupata mabao kipindi cha pili.
    Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Stand United imemaliza hasira zake za kufungwa na Simba SC wiki iliyopita kwa kuichapa Mtibwa Sugar ya Morogoro mabao 2-1 jioni ya leo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.
    Mabao yote ya Stand United leo yamefungwa na Nahodha wake, Jacob Massawe dakika za 49 na 71, wakati la Mtibwa Sugar limefungwa na Ismail Mhesa dakika ya 64.
    Kwa ushindi huo, Stand United inafikisha pointi 14 baada ya kucheza mechi 11 na kupanda hadi nafasi ya 11 kutoka ya 13, wakati Mtibwa Sugar baada ya kupoteza mechi ya pili mfululizo Kanda ya Ziwa, kufuatia kufungwa pia na Mbao FC mjini Mwanza, wanabaki na pointi zao 17 baada ya kucheza mechi 11.  
    Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, bao la dakika ya pili la mshambuliaji Eliud Ambokile limeipa ushindi wa 1-0 Mbeya City dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Nayo Ndanda FC imeibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Biashara United ya Mara Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara leo. Mabao ya Ndanda yamefungwa na Vitalis Mayanga dakika ya 19 na Ismail Mussa dakika ya 48, wakati la Biashara United limefungwa na Jerome Lambele dakika ya 71.  
    Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Beno Kakolanya, Paul Godfrey, Gardiel Michael, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Kelvin Yondan, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mrisho Ngassa, Raphael Daudi/Maka Edward dk77, Heritier Makambo, Thabani Kamusoko/Amissi Tambwe dk74 na Deus Kaseke/Matheo Anthony dk63.
    KMC FC; Juma Kaseja, Aaron Lulambu, Rayman Mgungila, Ally Ally, Sadallah Lipangile, Ally Msengi, Abdul Hassan, Abdallah Masoud ‘Cabaye’/James Msuva dk81, Omar Ramadhani/Ramadhani Kiparamoto dk72, Mohammed Mkopi na Emmanuel Mvuyekure.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BAO LA DAKIKA ZA MWISHONI LA ‘FEI TOTO’ LAIPA USHINDI YANGA SC DHIDI YA KMC NA KURUDI JUU LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top