• HABARI MPYA

  Saturday, November 04, 2017

  SINGIDA UNITED V YANGA: MWENDELEZO WA UPINZANI WA PLUIJM NA LWANDAMNA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  WAKATI Yanga imewafuata Singida United kwa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara leo Uwanja wa Namfua, pamoja na vita ya ubingwa kuna kitu kingine kinatazamwa.
  Nacho si kingine zaidi ya upinzani wa makocha wa timu hizo, Mholanzi Hans van der Pluijm wa Singida na Mzambia, George Lwandamina wa Yanga SC.      
  Lwandamina alikuja Yanga Novemba mwaka jana kuchukua nafasi ya Pluijm aliyeiongoza timu hiyo kwa vipindi viwilli tangu mwaka 2014.
  Yanga ilipendezewa na Lwandamina baada ya mafanikio yake ya kuifikisha Zesco United Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka jana na ikataka ayahamishie mafanikio yake hayo Jangwani.
  Hans van der Pluijm (kushoto) wakati anamkabidhi timu ya Yanga George Lwandamina (kulia) Novemba mwaka jana
  Yanga ikaachana na Pluijm ambaye atakumbukwa kwa mambo mawili makubwa – kwanza kufuta utamaduni wa timu hiyo kufungwa mabao mengi na timu za Kaskazini mwa Afrika na pili kuweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kuiwezesha timu hiyo kuifunga timu ya Misri na kuanzisha utamaduni wa kushinda dhidi ya timu za Kaskazini mwa Afrika kwa ujumla.
  Lakini pia, Pluijm alikuwa kocha kiboko ya Simba, kwani katika mechi tano alizoiongoza timu hiyo dhidi ya mahasimu wake hao wa jadi, ameshinda mbili, sare mbili na kufungwa moja, wakati tangu Lwandamina aanze kazi Jangwani, Yanga haijaonja ushindi dhidi ya Wekundu wa Msimbazi, wakifungwa mara tatu na sare moja. 
  Kwa sababu hiyo, Yanga walimpa uanachama mwalimu huyo, ingawa wiki hii uongozi wa Singida United umesema uanachama huo ulikoma alipoondoka Jangwani na leo ataifunga timu yake hiyo ya zamani.
  Mchezo wa leo ni fursa kwa Pluijm kuwathibitishia Yanga walikosea kumuondoa yeye, wakati kwa Lwandamina ni nafasi ya kuwahakikishia wana Jangwani walifanya maamuzi sahihi kumpa nafasi hiyo mbele ya Mholanzi huyo.
  Huu ni mchezo wa pili kwa timu hizo kukutana baada ya Agosti 6, mwaka huu Yanga kuifunga Singida United 3-2 katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Siku hiyo, Yanga ilitoka nyuma kwa 2-1 na kushinda mabao 3-2, Emmanuel Martin akifunga bao la ushindi dakika ya 90 na ushei akimalizia pasi ya mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe.
  Kiungo Mzimbabwe, Thabani Scara Kamusoko alianza kuifungia Yanga bao la kwanza dakika ya tano kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya mshambuliaji mpya, Ibrahim Ajib kuangushwa umbali wa mita 25.
  Mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Azam Rwanda kwa misimu yote miwili iliyopita, Dany Usengimana akaifungia Singida United bao la kusawazisha dakika ya nane akitumia vizuri makosa ya nabeki wa Yanga kuchanganyana.
  Mshambuliaji Mzimbabwe, Simbarashe ‘Simba’ Nhivi Sithole akaifungia bao la pili Singida dakika ya 23 akitumia tena makosa ya safu ya ulinzi ya Yanga, kabla ya Mrundi Tambwe kuisawazishia Yanga kwa penalti dakika ya 83 kufuatia kipa Said Lubawa kumchezea rafu kiungo chipukizi, Said Mussa.   
  Lakini kwenye mchezo huo, Singida walipoteza mikwaju miwili ya penalti, wa kwanza dakika ya kwanza kabisa Elisha Muroiwa akipaisha juu ya lango na ya pili, kipa Rostand akiokoa shuti la pembeni la mshambuliaji Atupele Green. 
  Na baada ya kipigo hicho, Pluijm akarudi nyuma na kurekebisha kidogo usajili wake, akiwaongeza kipa Peter Manyika kutoka Simba na mshambuliaji Michelle Katsavairo kutoka klabu ya Keizer Chiefs ya Afrika Kusini, huku akimuacha Mzimbabwe mwenzake, Wisdom Mtasa.
  Ikumbukwe huu ni mchezo wa kwanza kufanyika Uwanja wa Namfua, baada ya Singida kuwa inatumia Uwanja wa mkoa jirani, Jamhuri mjini Dodoma katika mechi zake za awali tangu ipande Ligi Kuu.
  Na baada ya ukarabati uliokuwa unafanyika Namfua kukamilika, leo Singida United wanacheza nyumbani kwa mara ya kwanza na kwa mara ya pili dhidi ya Yanga. Ni Lwandamina tena, au Pluijm atasherehekea baada ya dakika 90? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SINGIDA UNITED V YANGA: MWENDELEZO WA UPINZANI WA PLUIJM NA LWANDAMNA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top