• HABARI MPYA

  Sunday, November 05, 2017

  SAMATTA: NDOTO ZANGU ZINAKARIBIA KUTIMIA ULAYA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MCHEZAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amesema kwamba ndoto zake zinaelekea kutimia baada ya kuteuliwa katika orodha ya wachezaji 30 wanaowania tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika mwaka huu.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online kwa simu leo, Samatta amesema kwamba amepokea kwa furaha uteuzi huo ambao unazidi kumfanya aamini juhudi zake zinamsogeza karibu na ndoto zake.
  “Nimeupokea kwa furaha uteuzi huu, kwani inazidi kunifanya niamini juhudi zangu zinanisogeza karibu na ndoto zangu. Nadhani wachezaji wenzangu wa Tanzania wanaweza kujifunza kitu kupitia hili,”amesema.
  Pamoja na hayo, Samatta anasikitika ameumia goti la mguu wake wa kulia jana akiichezea klabu yake, KRC Genk ikilazimishwa sare ya 0-0 na Lokeren katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
  Mbwana Samatta aliumia jana akiichezea KRC Genk ikilazimishwa sare ya 0-0 na Lokeren

  Kwa kuumia huko, Samatta amesema kuna wasiwasi asiweze kuja kujiunga na kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo dhidi ya Benin wiki ijayo.
  Nahodha huyo wa Taifa Stars amesema kwamba alipanga kujiunga na kikosi cha timu ya taifa moja kwa moja nchini Benin, lakini sasa atalazimika kusubiri taarifa ya daktari wa klabu yake, Genk juu ya maumivu yake.
  “Baada ya kuumia jana, itanibidi nisubiri ripoti ya daktari wa klabu yangu (Genk) ndiyo nijue kama ninaweza kuja kujiunga na Taifa Stars kwa mchezo huu dhidi ya Benin au ula,  maana inawezekana nimepata maumivu makubwa,”amesema Samatta ambaye jana amecheza mechi yake ya 70 Genk. 
  Lakini alidumu uwanjani kwa dakika 40 tu kabla ya kuumia na kumpisha Nikolaos Karelis aliyekuwa anacheza kwa mara ya pili tangu arejee uwanjani baada ya kuwa nje kwa muda mrefu kutokana na kuwa majeruhi.
  Katika mechi hizo 70, Samatta, mshambuliaji wa zamani wa Mbagala Market, African Lyon na Simba za Tanzania, amefunga mabao 22 kwenye mechi za mashindano yote tangu alipowasili Genk Januari mwaka jana akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Baada ya kucheza nyumbani mfululizo mechi za kirafiki za kimataifa, Taifa Stars sasa itatoka mwezi huu kwenda Benin kucheza na wenyeji Novemba 11, mwaka huu na kikosi cha wachezaji 24 kitaingia kambini leo mjini Dar es Salaam kabla ya kusafiri Novemba 9 kwenda Benin tayari kwa mchezo huo.  
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA: NDOTO ZANGU ZINAKARIBIA KUTIMIA ULAYA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top