• HABARI MPYA

    Tuesday, November 14, 2017

    LWANDAMINA AREJEA LEO KUIANDAA YANGA DHIDI YA MBEYA CITY

    Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
    KOCHA wa Yanga, Mzambia George Lwandamina anatarajiwa kurejea leo Dar es Salaam kutoka kwao, Zambia ambako alikwenda kwa mazishi ya mpwa wake.
    Lakini Lwandamina, mchezaji wa zamani wa Mutondo Stars, Mufulira Blackpool na Mufulira Wanderers pamoja na timu ya taifa ya Zambia, hataweza kuwahi mazoezi ya leo, bali atakuwa tayari kuanza kazi kesho.
    Katika kipindi cha chote cha wiki nzima ya Lwandamina kuwa Zambia, kikosi cha Yanga kimekuwa kikiendelea na mazoezi chini ya makocha Wasaidizi, Mzambia mwingine, Noel Mwandila na wazawa, Nsajigwa Shadrack na Juma Pondamali.   
    Lakini katika mazoezi hayo, Yanga iliwakosa wachezaji wake wengi waliokuwa na timu za taifa ya U-23 na ya wakubwa, Taifa Stars.
    Kocha Mzambia wa Yanga, George Lwandamina (kulia) anatarajiwa kurejea leo Dar es Salaam kutoka kwao, Zambia

    Ikabidi wachezaji wa timu ya vijana, Yanga B wapelekwe kufanya mazoezi na wachezaji wachache wa timu ya wakubwa.
    Yanga inatarajiwa kushuka dimbani Jumapili kumenyana na Mbeya City, Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam katika mfululizo wa Ligi Kuu. 
    Kwa ujumla baada ya mapumziko ya kupisha mechi za kirafiki za kimataifa zikiwemo za kufuzu Kombe la Dunia, Ligi Kuu inatarajiwa kurejea wikiendi hii na Ijumaa Singida United wataikaribisha Lipuli ya Iringa Uwanja wa Namfua, wakati Azam FC watakuwa wageni wa Njombe Mji FC Jumamosi Uwanja wa Saba Saba.
    Azam FC wana taji moja tu la Ligi Kuu kwenye kabati lao, walilotwaa mwaka 2013-2014 baada ya kupanda msimu wa 2008-2009.
    Mechi nyingine za Jumamosi, Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Ndanda FC Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Stand United n Mwadui FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Maji Maji na Mbao FC Uwanja wa Maji Maji mjini Songea na Simba SC dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Yanga inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 17, sawa na Mtibwa Sugar, nyuma ya Simba na Azam zenye pointi 19 kila moja.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LWANDAMINA AREJEA LEO KUIANDAA YANGA DHIDI YA MBEYA CITY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top