• HABARI MPYA

    Tuesday, November 14, 2017

    TAIFA STARS WAREJEA DAR, WACHEZAJI WATAWANYIKA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSAFARA wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars umerejea nchini alfajiri ya leo kutoka Benin ambako juzi ilicheza mchezo wa kirafiki.
    Taifa Stars Jumapili ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, Benin katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa l'Amitie, au Urafiki mjini Cotonou ambao ulionyeshwa moja kwa moja na Televisheni ya Azam.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa wa nchini humo, Ligali Praphiou aliyesaidiwa na Bello Razack na Koutou Narcisse, hadi mapumziko wenyeji The Squirrels, walikuwa mbele kwa bao 1-0.
    Bao hilo lilifungwa kwa penalti na mkongwe mwenye umri wa miaka 33, Nahodha, Stephane Sessegnon anayechezea klabu ya Montpellier ya Ufaransa.
    Kocha Salum Mayanga (kushoto) na kiungo Simon Msuva (kulia) wakati wa kuwasili leo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)

    Hata hivyo, ilikuwa ni penalti ya mashaka, kwani mchezaji aliyeugusa mpira huo kwa mkono alikuwa ni wa Benin, Khaled Adenon lakini refa akadhani ni mchezaji wa Tanzania.
    Sessegnon akamtungua kipa namba moja wa Tanzania, Aishi Manula kufunga bao lake la 21 timu ya taifa katika mechi ya 68.
    Wachezaji wa Tanzania wakamlalamikia refa kwa kutowapa penalti dakika ya 32 kufuatia, winga Simon Msuva kuangushwa kwenye boksi baada ya kusukumwa.
    Kipindi cha pili, Tanzania ilikianza kwa nguvu n kasi zaidi wakishambulia kutokea pembeni na hatimaye kufanikiwa kupata bao la kusawazisha.
    Alikuwa ni mshambuliaji wa zamani wa Simba ya Tanzania na Dhofar SC ya Oman, Elias Maguri aliyefunga bao hilo akimalizia krosi ya winga Shiza Kichuya kutoka upande wa kushoto.
    Matokeo haya yanamaanisha Benin imeshindwa kulipa kwa Tanzania, kwani mara ya mwisho, zilipokutana Oktoba 12, mwaka 2014 Taifa Stars ilishinda 4-1, mabao ya Nahodha wa wakati huo, beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ dakika ya 16, kiungo Amri Kiemba dakika ya 39, Thomas Ulimwengu dakika ya 49 na Juma Luizio, wakati la Benin lilifungwa na Suanon Fadel dakika ya 90.
    Wachezaji wote sasa wanarejea klabu zao kwa maandalizi ya michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wikiendi hii na wale wanaocheza nje wanarejea kwenye klabu zao pia.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS WAREJEA DAR, WACHEZAJI WATAWANYIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top