• HABARI MPYA

  Wednesday, November 01, 2017

  AZAM FC WANAJIPIMA NA ASHANTI UNITED LEO USIKU CHAMAZI

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Azam FC inateremka kwenye Uwanja wake wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kumenyana na Ashanti United katika mchezo wa kirafiki utakaoanza Saa 1:00 usiku.
  Mchezo huo kwa Azam ni sehemu ya maandalizi ya mechi yake ijayo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting Uwanja wa Azam Complex, wakati Ashanti inajiweka sawa kwa mechi za Ligi Daraja la Kwanza.
  Azam itaendelea tena na mazoezi kesho mara mbili kabla ya kushuka dimbani Jumapili kumenyana na Ruvu Shooting.
  Timu hiyo inayodhaminiwa na maji safi kabisa ya Uhai Drinking Water, Benki bora kabisa nchini ya NMB na Tradegents, imekuwa na msimu mzuri hadi sasa ikiwa haijapoteza mchezo wowote kwenye mechi nane za ligi ilizocheza mpaka sasa, ikiwa imeshinda nne na kutoka sare nne.
  Azam FC ni miongoni mwa timu tano za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo zinazofukuzia ubingwa msimu huu ikijikusanyia pointi 16, ikiwa inalingana pointi na timu nyingine tatu zilizo juu yake kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa ambazo ni Simba, Yanga na Mtibwa Sugar.
  Jambo la kufurahisha zaidi linaloifanya kuwa na rekodi nzuri, ndio timu pekee iliyofungwa mabao machache mpaka sasa ikiwa imeruhusu nyavu zake kuguswa mara mbili na katika mechi nane ilizocheza, imefanikiwa kutoka uwanjani bila wavu wake kuguswa kwenye mechi sita.
  Mshambuliaji Mbaraka Yusuph, aliyeibuka kinara Mchezaji Bora wa Azam FC wa mwezi Septemba-Oktoba (NMB Player of the Month) ndiye anayeongoza mpaka sasa kwenye kucheka na nyavu ndani ya kikosi hicho akiwa ametingisha nyavu za wapinzani mara tatu.  
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC WANAJIPIMA NA ASHANTI UNITED LEO USIKU CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top