• HABARI MPYA

  Friday, March 03, 2017

  YANGA YAACHANA NA PLUIJM, YAMUAMBIA HALI YA KIFEDHA MBAYA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imemfukuza Mkurugenzi wake wa Ufundi, Mholanzi Hans van der Pluijm kwa sababu ya hali mbaya ya kifedha inayoikabili klabu hiyo kwa sasa.
  Pluijm ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba Yanga imemuambia kutokana na hali ngumu ya kifedha inayoikabili klabu kwa sasa haiwezi kuendelea kuwa naye.
  “Leo niliitwa na Katibu (Charles Boniface Mkwasa) akaniambia kutokana na hali mbaya ya kifedha ya klabu kwa sasa, hawawezi kuendelea na mimi. Akanipa barua ya kunivunjia mkataba, nikaondoka zangu,”amesema.
  Pluijm anaidai Yanga mishahara ya miezi kadhaa na kutokana na kumvunjia mkataba klabu hiyo inapaswa kumlipa. “Hakuna wasiwasi, nitakaa nao na kuzungumza nao namna ya kulipana,”alisema.
  Hata hivyo, Pluijm amesema anasikitika klabu imefanya maamuzi bila kumshirikisha, kwani naye alikuwa tayari kuvumilia hali ngumu ya sasa. “Nimekuwa Yanga katika wakati mzuri, na hili lililotokea sasa kila mtu anajua, nami nilikuwa tayari kuvumilia, ila wamefanya maamuzi bila kunishirikisha,”alisema.
  Pluijm amesema anaondoka Yanga, lakini anataka ieleweke klabu hiyo ipo ndani ya moyo wake na atakuwa tayari siku moja kurejea tena akihitajika.
  Yanga ilimhamishia Pluijm kwenye Ukurugenzi wa Ufundi Novemba mwaka jana, baada ya kumleta Mzambia, George Lwandamina awe kocha Mkuu.
  Pluijm amefundisha Yanga kwa awamu mbili tangu mwaka 2014 alipoanza kwa kufanya kazi kwa nusu msimu, akimpokea Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts kabla ya kwenda Uarabuni.
  Alikwenda Al Shoalah FC ya Saudi ya Arabia na nafasi yake ikachukuliwa na Mbrazil, Marcio Maximo ambaye naye alifanya kazi kwa nusu msimu kabla ya Pluijm kurejeshwa Januari mwaka jana. 
  Saudi Arabia ambako alikwenda na aliyekuwa Msaidizi wake, Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa – Pluijm  aliondoka baada ya kutofautiana na uongozi wa timu uliotaka kumsajilia wachezaji asiowataka.
  Kabla ya kuhamishiwa kwenye Ukurugenzi wa Ufundi, Pluijm aliiongoza Yanga katika jumla ya mechi 128, akishinda 80, sare 25 na kufungwa 23.
  Katika mechi 19 za nusu msimu mwaka 2014, alishinda 11, sare sita na kufungwa mbili, wakati katika mechi 110 za tangu mwaka jana, alishinda 69, sare 19 na kufungwa 21.
  Msimu uliopita ulikuwa mzuri zaidi kwake, akibeba mataji yote matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).
  Pluijm pia aliiwezesha Yanga kufika hatua ya makundi ya michuano ya Afrika (Kombe la Shirikisho) kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998 na mara ya pili kihistoria. Yanga ilifika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka huu baada ya mwaka 1998 kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.
  Na kwa mafanikio hayo, haikuwa ajabu Pluijm akishinda tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwishoni mwa msimu uliopita. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA YAACHANA NA PLUIJM, YAMUAMBIA HALI YA KIFEDHA MBAYA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top