• HABARI MPYA

  Wednesday, March 01, 2017

  NGOMA: ‘MADUDU’ YA VIONGOZI YANANIONDOA YANGA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa Yanga, Mzimbabwe Donald Dombo Ngoma amesema ataondoka katika klabu hiyo kukwepa mambo ya ovyo ya uongozi.
  Ngoma amesema hayo wakati akizungumzia tuhuma dhidi yake juu ya kutocheza mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Simba Jumamosi, Yanga ikichapwa mabao 2-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  “Mimi na klabu tumefikia katika hatua ambayo nitachukua maamuzi muda si mrefu nitakupa taarifa sahihi za kuondoka kwangu kutokana na mambo ya ovyo ya viongozi wa klabu,”ameandika Ngoma katika akaunti yake ya Instagram leo asubuhi.
  Donald Ngoma (katikati) amesema kwamba ataondoka Yanga baada ya kuchoshwa na 'madudu' ya uongozi wa timu
  Aidha, mchezaji huyo amesema kwamba mashabiki na wapenzi wa Yanga wamekuwa wakimshutumu na kumtukana kutokana na taarifa zisizo za kweli zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu yeye.  
  “Nimekuwa kimya wakati wote nikitukanwa juu ya sababu za kutocheza, wakati ukweli ni kwamba mimi nina maumivu ya goti. Taarifa nyingi zimekuwa zikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba sitaki kucheza kwa sababu ninataka kuondoka katika timu, nashangaa wapi wanapata hizo taarifa,”amesema Ngoma.
  Amesema Daktari ambaye Yanga walimtumia kumtibu yeye alikuwa ‘tapeli’ na ameilia fedha klabu bila kufanya kazi yoyote.
  “Daktari alikula fedha za viongozi wa klabu na kuwadanganya kwamba alikuwa ananitibu amenipeleka hospitali, wakati ukweli ni kwamba nilikuwa ninatibiwa katika hospitali nyingine kwa gharama zangu mwenyewe,”amesema Ngoma.
  Mchezaji huyo mrefu mwenye nguvu na kasi uwanjani, amesema kwamba baadaye Daktari huyo alipoulizwa alisema kwamba niko fiti kucheza, wakati ukweli ni kwamba sikuwa tayari kabisa kucheza.
  “Alikuwa anawaambia watu kwamba maumivu yangu yanaweza kupona ndani ya wiki mbili, wakati Daktari halisi aliyekuwa ananitibu alisema ninahitaji kati ya wiki sita hadi nane kupona. Tazama huyu Daktari feki alivyoleta mtafaruku kati yangu na timu,”amelalamika Ngoma.
  Donald Dombo Ngoma anaelekea kukamilisha msimu wake wa pili tangu ajiunge na Yanga akitokea Platinums FC ya Zimbabwe mwaka 2015.
  Na amekuwa mchezaji muhimu tangu ajiunge na klabu hiyo yenye maskani yake, Jangwani, Dar es Salaam kiasi kwamba kila alipokosekana pengo lake lilionekana.     
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NGOMA: ‘MADUDU’ YA VIONGOZI YANANIONDOA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top