• HABARI MPYA

  Thursday, March 02, 2017

  HANS POPPE: USHINDI DHIDI YA YANGA UWE CHACHU YA UBINGWA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe amewaambia wachezaji wa klabu hiyo ushindi wa 2-1 dhidi ya Yanga Jumamosi uwe chachu ya ubingwa.
  Simba SC walikaa sawa kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya ushindi wa 2-1 dhidi ya mahasimu, Yanga Jumamosi ya Februari 25, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Na baada ya ushindi huo, Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Hans Poppe amesema kwamba wachezaji wa timu hiyo hawapaswi kubweteka.
  Hans Poppe (kushoto) amewaambia wachezaji wa Simba ushindi dhidi ya Yanga uwe chachu ya ubingwa

  “Wanatakiwa kuuchukulia ushindi huo kama chachu ya kufanya vizuri zaidi katika mechi zijazo na kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu mwishoni mwa msimu,”alisema jana katika mahojiano na Bin Zubeiry Sports – Online.
  Hans Poppe amesema kwamba ubingwa wa Ligi Kuu upo miguuni mwao wachezaji wa Simba sasa ni jukumu lao kuhakikisha wanashinda mechi zote zilizosalia ili kuendelea kuwa mbele ya Yanga.
  “Mbio za ubingwa bado ngumu, kama unavyoona hatumuachi mbali sana Yanga, ni tofauti ya pointi mbili, kiasi kwamba tukijiruhusu hata kutoa sare moja tu, watatufikia tena kwa bahati mbaya hakuna mechi tena na Yanga msimu huu,”alisema.
  Poppe amewaambia wachezaji wa Simba kama wameweza kushinda mechi ngumu dhidi ya Yanga basi wataweza kushinda mechi nyingine zote zilizosalia iwapo hawatafanya mzaha wala dharau.
  Simba SC inaongoza Ligi Kuu kwa sasa kwa pointi zake 54 za mechi 23, wakifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga yenye pointi 52. 
  Wekundu hao wa Msimbazi wanatarajiwa kushuka tena dimbani Jumamosi kumenyana na Mbeya City katika mfululizo wa Ligi Kuu Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HANS POPPE: USHINDI DHIDI YA YANGA UWE CHACHU YA UBINGWA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top