• HABARI MPYA

  Friday, March 03, 2017

  CANNAVARO AWATAKA WANA YANGA WAMPE MUDA ZULU

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  NAHODHA wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ amewataka wapenzi wa Yanga kumpa muda kiungo mpya wa timu hiyo, Mzambia Justin Zulu.
  Zulu alijiunga na Yanga SC katika dirisha dogo Desemba mwaka jana, lakini hadi sasa badi hajawavutia wapenzi wa timu hiyo kiasi kwamba wengine wameanza kuhoji usajili wake.
  Lakini Nahodha Cannavaro amewataka mashabiki wa Yanga wawe watulivu na kumpa muda kiungo huyo wa zamani wa kimataifa wa Zambia na klabu ya Zesco United ya kwao.
  “Mimi ninawaomba wapenzi wa Yanga na wana Yanga kwa ujumla tuwe watulivu, tumvumilie huyu mchezaji ili aendelee kuzoea. Mara nyingi wachezaji huhitaji muda baada ya kuingia katika timu mpya,”alisema Cannavaro.
  Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (kulia) akiwa na kiungo mpya wa timu hiyo, Mzambia Justin Zulu (kushoto)

  Pamoja na hayo, Nahodha huyo amewaomba mashabiki wa Yanga kusahau yaliyopita na kuendelea kuwasapoti wachezaji wao katika kila mechi.
  Cannavaro alisema kwamba Yanga inakabiliwa na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mbali na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Kombe la TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) na wachezaji ilionao ndiyo inayowategemea kwa ajili ya michuano yote hiyo.
  “Kwa hivyo tusahau ya nyuma na tuunganishe nguvu zetu tuendelee kupambana, Ligi Kuu bado mbichi hii, bado tuna nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa. Lakini pia tuna dhamira ya kufanya vizuri katika Ligi ya Mabingwa, hivyo lazima tuunganishe nguvu zetu,”alisema Cannavaro. 
  Baada ya ushindi wa 2-0 dhidi ya Ruvu Shooting Jumatano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga inatarajiwa kushuka tena dimbani Jumapili kumenyana na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
  Kwa sasa, mabingwa watetezi Yanga SC wenye pointi 52 wanazidiwa pointi mbili na vinara, Simba SC wenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 23.     
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: CANNAVARO AWATAKA WANA YANGA WAMPE MUDA ZULU Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top