• HABARI MPYA

    Sunday, November 20, 2016

    KIPRE AWASHANGAA SIMBA NA YANGA KUMSAJILIA MAGAZETINI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa zamani wa Azam FC, Kipre Herman Tchetche amesema kwamba hajazungumza na Simba wala Yanga kuhusu mpango wa usajili.
    Mchezaji huyo wa Al Suwaiq ya Oman, aliiambia BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE jana kwamba hastaajabu chochote juu ya kelele za Simba na Yanga, kwani kawaida tangu anacheza Tanzania kusema zitamsajili.
    “Sijazungumza na timu yoyote. Kwanza hata namba yangu ya sasa sidhani kama wanayo. Ila ni kawaida yao hao tangu nipo huko wanasema hivyo hivyo,”alisema.
    Tchetche alisema kwamba kwa sasa ameelekeza akili yake kwa mwajiri wake, Al Suwaiq katika Ligi Kuu ya Oman hadi atakapomaliza Mkataba wake Mei mwakani. “Sifikirii kubaki hukiu baada ya kumaliza mkataba huu, ila sijajua nitakwenda wapi,”alisema.
    Lakini Kipre Tchetche amewataka Simba na Yanga waache porojo kwenye vyombo vya Habari na kama kweli wanamtaka wawasiliane naye.
    “Tangu nipo Tanzania magazeti yalikuwa yanaandika Kipre anakwenda Yanga au Simba, lakini sikuwahi kuzungumza na kiongozi yeyote wa hizo timu. Nimekwishawazoea hao, naona huwa wanajifurahisha, kwa sababu kama wananitaka kweli wangenitafuta,”alisema.
    Tchetche  
    Kipre Tchetche alijiunga na Al-Nahda Al-Buraimi ya Ligi Kuu ya Oman mapema msimu huu, lakini baada ya klabu hiyo kushindwa kulipa ada ya uhamisho dau la dola za Kimarekani 50, 000 zaidi ya Sh. Milioni 100 za Tanzania, Azam FC ikamuuza Suwaiq.
    Na Tchetche akalazimika kuhamia Al Suwaiq FC kwa Mkataba wa mwaka mmoja kufuatia klabu hiyo kumalizana na Azam FC na anaendelea vizuri na maisha huko kwa sasa.
    Kipre Tchetche alijiunga na Azam FC mwaka 2011 kwa pamoja na pacha wake, Kipre Michael Balou baada ya wote kung’ara katika kikosi cha Ivory Coast kilichokuja kucheza michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Challenge) Dar es Salaam.
    Na pacha wake, Balou ametemwa pia Azam FC baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu, kufuatia ndugu yake kuondoka mwishoni mwa msimu uliopita.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIPRE AWASHANGAA SIMBA NA YANGA KUMSAJILIA MAGAZETINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top