• HABARI MPYA

    Sunday, November 20, 2016

    HILI LA FARID MUSSA, INASIKITISHA KWA KWELI

    NILISTAAJABU kidogo kocha Charles Boniface Mkwasa alipoteua kikosi kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Zimbabwe mwezi huu bila kumuorodhesha na kinda Farid Mussa Malik.
    Lakini hata kabla sijauliza, nilijua sababu za Mkwasa kutomuita Farid na ni za msingi kwa mwalimu yeyote angezitumia kama kigezo cha kutomchukua mchezaji.
    Farid hajacheza mechi yoyote msimu huu baada ya msimu mzuri uliopita akianza kwa kishindo soka ya kimataifa na kuonyesha kipaji kikubwa kilichowaduwaza wengi.
    Hiyo ni kwa sababu Azam FC imemtoa kwa mkopo Farid kwenda CD Tenerife kwa makubaliano maalum. Na hiyo ilifuatia Farid kufuzu majaribio katika klabu hiyo katikati ya mwaka alipokwenda na Mkurugenzi wa klabu yake, Yussuf Bakhresa.
    Farid alitua Hispania Aprili 21 baada ya kuichezea Azam FC katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Esperance mjini Tunis, Tunisia ikifungwa 3-0 na kutolewa kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya awali kushinda 2-1 Dar es Salaam.
    Na ilimchukuwa wiki moja tu Farid kuwakuna kwa kipaji chake makocha wa Tenerife na kutaka kumnunua, lakini Azam ikakataa na kuamua kumtoa kwa mkopo.
    Azam FC haijamsajili Farid katika kikosi chake cha Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu kwa kuwa imemtoa kwa mkopo Tenerife ambayo tayari imemuombea hadi Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC). 
    Kutokana na kutocheza tangu Agosti, Farid sasa ametemwa hadi Taifa Stars na wasiwasi ni kwamba itaathiri zaidi kipaji cha mchezaji huyo aliyekuwa anainukia vizuri katika soka ya kimataifa.
    Haijulikani ni nini haswa kinamkwamisha Farid kupata visa, kwani mwezi uliopita Azam FC ilitoa taarifa ya kupata kibali cha mchezaji huyo kufanya kazi Hispania, maana yake alikuwa huru kwenda kuanza kujiunga na timu hiyo ya Daraja la Kwanza.
    Farid mwenyewe akiulizwa amekuwa akisema kwamba kila anapokwenda Ubalozi wa Hispania hapa nchini amekuwa akipewa tarehe nyingine ya kwenda tena kuuliza.
    Na juzi, Farid alisema jibu la mwisho kaambiwa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba sasa atasafiri hadi Hispania kwenda kuzungumza na Tenerife juu ya suala hilo.
    “Bado sijafanikiwa kupata visa, wameniambia Saad (Kawemba) anakwenda Hispania kukutana na viongozi wa Deportivo Tenerife. Sasa inabidi nisubiri aende akazungumze nao, kisha atanifahamisha. Kwa sasa niko njia panda,”alisema Farid.
    Farid alikwenda Hispania akiacha ofa nyingine za majaribio na kusajiiwa moja kwa moja na timu nyingine za Ulaya ikiwemo Ubelgiji, ambako Mtanzania mwingine, Mbwana Samatta anacheza – kwa matarajio kwamba amefanya uamuzi sahihi.
    Lakini sasa maamuzi yake yanamtafuna – kwani amejikuta amekaa nyumbani bila kucheza katika umri ambao ndiyo anapaswa kupigana kujipambanua kwenye soka la soka.
    Uwezo alioonyesha ndani ya muda mfupi tu akicheza mechi kubwa dhidi ya Nigeria, Algeria, Misri na Chad ilitosha kujiridhisha Tanzania imepata mchezaji mwingine mzuri.
    Kwa nchi za wenzetu zenye kujua faida ya kuwa na wachezaji wenye vipaji kama Farid asingeachwa apotee kwa urahisi namna hii.
    Sisi huku hatujali. Ndiyo maana mara zote tunafanikiwa kuibua vipaji vinavyofanya vizuri katika mashindano makubwa ya vijana ya kimataifa kama Copa Coca Cola na Airtel Rising Stars, lakini baadaye tunavitelekeza.
    Farid anakwama vipi kwenda Hispania kama hadi Tenerife imemuombea ITC? Watanzania wanakwenda Hispania kila siku kwa shughuli mbalimbali na wengine wanaishi kabisa huko.
    Farid alikuwa huko kwa majaribio, kwa nini sasa kapata timu inashindikana kwenda Hispania? Kwa kweli inasikitisha tu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HILI LA FARID MUSSA, INASIKITISHA KWA KWELI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top