• HABARI MPYA

    Saturday, November 19, 2016

    ANGBAN HATARINI KUTEMWA SIMBA SC

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    LICHA ya kudaka vizuri mzunguko wote wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara akiiwezesha Simba SC kumaliza kileleni mbele ya mabingwa watetezi, Yanga, lakini kipa Muivory Coast, Vincent Atchouailou de Paul Angban yupo hatarini kutemwa.
    Hiyo inatokana na baadhi ya wadau wa Simba SC kutoridhishwa na udakaji wake katika kipindi chote cha kuwa kwake Simba SC.
    Na tayari Simba SC imeanza kuangalia uwezekano wa kusajili kipa mwingine wa kigeni, ingawa wazo la kumtema Angban linakabiliwa na upinzani wa ndani kwa ndani, kutokana na wadau wengine wa timu hiyo kuridhishwa na uwezo wa mlinda mlango huyo. 
    Angban amedaka jumla ya mechi 56 Simba na kufungwa mabao 25 huku mechi 34 akisimama langoni bila kuruhusu nyavu zake kuguswa

    Miongoni mwa makipa ambao Simba SC inataka kuwasajili ili imteme Angban, ni Mmalawi Owen Chaima wa Mbeya City aliye katika msimu wake wa kwanza Ligi Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Lakini kwa kuwa uongozi wa Simba SC umekubaliana kuheshimu maamuzi ya benchi la Ufundi, basi ripoti ya dawati hilo chini ya Kocha Mkuu, Mcameroon Joseph Marius Omog ndiyo imebeba mustakabali wake wa Angban.
    Kamati ya Utendaji ya Simba SC ilikuwa na kikao juzi usiku na miongoni mwa mamno iliyoyajadili ni taarifa ya benchi la Ufundi baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu na kuelekea mzunguko wa pili.  
    Hadi mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu unafikia tamati mapema mwezi huu, Angban ndiye aliyekuwa kipa mwenye rekodi nzuri zaidi, akifungwa mabao sita tu katika mechi 15.
    Angban pia aliweka rekodi ya kudaka mechi sita mfululizo bila kufungwa. Baada ya kufungwa katika sare ya 1-1 na Yanga Oktoba 1, mwaka huu – Angban akadaka mechi tano mfululizo zilizofuata bila kuruhusu bao, Simba ikishinda 2-0 dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Sokoine, 2-0 na Kagera Sugar, 1-0 na Mbao, 3-0 na Toto Africans zote Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na 3-0 na Mwadui Uwanja wa Kambarage. 
    Rekodi hiyo ilivunjwa katika mchezo uliofuata Novemba 6, Simba SC ikilala 1-0 mbele ya African Lyon Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na kipa huyo mrefu akaenda kufungwa tena mabao mawili katika mechi iliyofuata tena Novemba 9 Wekundu wa Msimbazi wakipigwa 2-1 Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
    Na hapo ndipo ‘wabaya wa Angban’ walipoanza kujitokeza wakimtoa kasoro kibao na kupendekezwa aachwe.  
    Kipa huyo wa zamani wa Chelsea FC ya England, alisajiliwa Simba SC msimu uliopita baada ya kufeli majaribio Azam FC, alikotua awali kujaribu bahati yake akashindwa kumvutia kocha Muingereza Stewart Hall aliyekuwa anaiongoza timu hiyo wakati huo.
    Lakini mbele ya Muigereza mwingine, Dylan Kerr aliyekuwa anaifundisha Simba SC msimu uliopita, Angaban akafuzu majaribio na kusajiliwa.  Mlinda mlango huyo aliyezaliwa Februari 2, mwaka 1985 mjini Anyama, alikuja Tanzania akitokea klabu ya Ligi Kuu ya kwao, Ivory Coast, Jeunesse.
    Vincent Angban aliwahi kuchezea timu ya vijana ya Chelsea chini ya umri wa mika 21 ingawa alikuwa amevuka umri huo katika harakati za kutafuta kusajiliwa The Blues, lakini pamoja na kuonyesha uwezo Stamford Bridge, haikuwa bahati yake jezi ya bluu.
    Kipa huyo aliibukia katika klabu ya vijana ya Rio Sport d'Anyama kabla ya kupandishwa kikosi cha kwanza mwaka 2005, ambako hata hivyo miaka miwili baadaye aliondoka na kwenda kujiunga na Sawe Sports msimu wa 2006/2007.
    Mwaka 2007, Angban akajiunga na ASEC Mimosas ambako alikuwa kipa wa kwanza hadi mwanzoni mwa msimu wa 2009 alipoumia na nafasi yake kuchukuliwa na Daniel Yeboah. 
    Yeboah akawavutia zaidi makocha wa timu hiyo kwa ubora wake wa kuokoa michomo na akaendelea kudaka hata Angban alipopona.
    Baada ya kumaliza Mkataba wake ASEC, Angban akarejea Jeunesse na baadaye akaenda London kudakia U21 ya Chelsea.
    Amewahi kudakia timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Ivory Coast katika michuano ya Afrika nchini Benin mwaka 2005 na aliiwakilisha pia nchi yake katika Michezo ya Olimpiki mwaka 2008.
    Amedakia pia timu ya taifa ya wakubwa ya Ivory Coast ‘Tembo’ katika michuano ya CHAN ikiwemo ile ya mwaka 2009 na ndiye aliyesimama langoni katika mechi na Tanzania, Taifa Stars ikishinda 1-0 bao pekee la Mrisho Ngassa.   
    Kwa sasa Angban ndiye kipa namba moja Simba SC mbele ya chipukizi, Peter Manyika na Dennis Richard waliopandishwa kutoka timu ya vijana msimu uliopita.
    Na tangu ametua Simba SC, Angban amedaka jumla ya mechi 56 na kufungwa mabao 25 huku mechi 34 akisimama langoni bila kuruhusu nyavu zake kuguswa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ANGBAN HATARINI KUTEMWA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top