• HABARI MPYA

  Monday, February 08, 2016

  HESHIMA KWENU FM ACADEMIA KWA WIMBO “MOYO WANGU”

  MIEZI kadhaa nyuma nilisifia wimbo Twanga Pepeta "Usiyaogope Maisha" kwa namna ulivyoshirikisha waimbaji wachache akiwemo Ally Chocky, Rama Pentagon na Saleh Kupaza.
  Nilipenda sana ushiriki huo wa waimbaji wachache, nikapenda pia ufupi wa nyimbo nikiamini ndio msingi wa mahitaji ya soko la sasa hivi.
  Kwa bahati mbaya sana waimbaji wengi wa Twanga hawakupendezwa na mageuzi yale yaliyofanywa na mtunzi Ally Chocky kwa kuwapiga benchi waimbaji wengine katika wimbo huo, ikafika hatua hata baadhi yao kususa kuitikia pale unapopigwa 'live' jukwaani.

  Napenda sana muziki wa dansi, lakini niwe mkweli, nachukia sana nyimbo ndefu pasipo na ulazima wa nyimbo kuwa ndefu, nachukia nyimbo zinazoimbwa na waimbaji wengi pasipo na ulazima wa kufanya hivyo - Waimbaji watano hadi sita kila mmoja anatupia kipande chake, halafu baada ya hapo watafuata marapa watatu kila mmoja na pande lake, kwa kweli huwa inachusha.
  Kwa bahati mbaya au nzuri mimi ni muumin wa muziki wa zamani na kwa yeyote mwenye kumbukumbu na muziki wa zamani atabaini kuwa hiki kinachoanza kufanywa sasa na wasanii wa dansi kupunguza urefu wa nyimbo na msururu wa waimbaji, si kipya wala si kufuata mkumbo wa bongo fleva, bali ndiyo hali halisi iliyokuwepo kwenye muziki wa zamani wa dansi.
  Tafuta nyimbo kama Rangi ya Chungwa, Georgina, MV Mapenzi, Chatu, Ngalula, Makumbele, Ogopa Tapeli, Tuma na nyingine nyingi halafu tazama muda uliotumika na kisha uliza waimbaji mastaa waliopigwa benchi kwenye hizo nyimbo. 
  Kuna wimbo mmoja mpya wa FM Academia unaokwenda kwa jina la "Moyo Wangu" utunzi wake mwimbaji anayejulikana zaidi kwa jila la 33. Niseme sentensi moja tu kwa Wazee wa Ngwasuma: HESHIMA KWENU.
  “Moyo Wangu” ni aina ya nyimbo ambazo zitaleta ukombozi kwenye muziki wa dansi – wimbo mfupi, ujumbe unaoeleweka, uimbaji mzuri, mpangilio safi wa vyombo, achilia mbali ubora wa video yake.
  Kwa sehemu kubwa ya wimbo, mwimbaji aliyetawala ni 33, asindikizwa kwa mbali na Redock Mauzo. Waimbaji wenye majina makubwa kama Nyoshi el Saadat, Patcho Mwamba, Pablo Masai  na King Blaze wamekaa kando lakini bado kazi imesimama ile mbaya.
  Kumekuwa na malalamiko kila kukicha kuwa vituo vya radio na televisheni vimekuwa vikiubania muziki wa dansi. Sitaki kuegemea sana upande huo ila ukweli ni kwamba kuna wakati wasanii na wadau wa muziki dansi wanakuwa kama ile hadithi ya “Kwenye msafara wa mamba kenge nao wamo”.
  Kwamba inafika wakati hata mwenye nyimbo mbovu naye analalamika kuwa muziki dansi unabaniwa. Hii ni kasumba mbaya ambayo itazidi kuudidimiza muziki wa dansi baada ya kuukomboa.
  Wakati mwingine wanamuziki wa dansi wapime ubora wa nyimbo zao kabla ya kulalamika - unapotoa nyimbo ambayo ndani yake waimbaji ni kama wanaimba nyimbo tano tofauti, yaani kila mmoja na maudhui yake, halafu mpangilio wa vyombo haushawishi hata mtu kunesa nesa, kisha ukalalamika kuwa wimbo wako unabaniwa basi unakuwa huna tofauti na kenge kwenye msafara wa mamba.
  “Moyo Wangu” wa FM Academia ni aina ya nyimbo ambazo kama itakosa ‘air time’ ya kutosha kwenye vituo vya radio na televisheni, basi wadau wa muziki wa dansi wanastahili kulalamika - ni jambo la ajabu wimbo kama huo kutiwa kapuni.
  Nichukue fursa hii kuwaammbia FM Academia wimbo huu ni moja ya silaha yao muhimu katika kurejea safari ya mafanikio waliyozoa kwenye albam ya “Dunia Kigeugeu”, - hawapaswi kubweteka na badala yake watumie nguvu kubwa kuusambaza kila kona.
  Majuzi nilimsikia Ally Chocky akizungumza na kituo kimoja cha radio ambapo licha kusema kuwa muziki wa dansi hauwezi kufa, lakini akawaasa wanamuziki wenzake kufanya mageuzi kwa kutengeneza nyimbo nzuri na fupi. Kwangu mimi naamini ngoma hii ya “Moyo Wangu” ni aina ya mabadiliko anayoyataka Chocky.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HESHIMA KWENU FM ACADEMIA KWA WIMBO “MOYO WANGU” Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top