• HABARI MPYA

    Sunday, February 21, 2016

    VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA VIACHIWE SAKATA LA UPANGAJI MATOKEO

    TIMU moja ya kupanda Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu ujao kati ya tatu, bado haijajulikana licha ya kumalizika kwa mechi za makundi yote matatu, A, B na C ya Ligi Daraja la Kwanza wiki iliyopita.
    Hiyo inafuatia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kukataa kuamua timu ya kupanda kutoka Kundi C, baada ya kutilia shaka matokeo ya michezo miwili ya mwisho ya kundi hilo.
    Geita Gold SC inayofundishwa na Nahodha wa zamani wa Simba SC, Suleiman Matola iliifunga mabao 8-0 JKT Kanembwa ugenini kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, wakati Polisi Tabora ilishinda 7-0 nyumbani dhidi ya JKT Oljoro Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

    Baada ya kupitia taarifa hizo na vielelezo vingine, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imetilia shaka matokeo ya mechi hizo kutokana na kuwapo dalili za upangaji wa matokeo.
    Na kwa kuwa suala hilo linahusisha masuala ya kinidhamu, na kwa kuzingatia Ibara ya 50 (1) na (11) ya Katiba ya TFF na Ibara ya 69 ya Kanuni za Nidhamu za TFF, Kamati ya Saa 72 imemuelekeza Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa apeleke suala hilo kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya uchunguzi na hatimaye kufanya uamuzi.
    Timu mbili zilizopanda bila kupingwa ni African Lyon kutoka Kundi A na Ruvu Shooting Kundi B, ambazo sasa zitacheza tena Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Ukirejea matokeo ya mechi mbili za mwisho za Kundi C, ni kweli yanatia shaka na kwa namna yoyote, TFF haikukosea wala kukurupuka kuamua kusitisha kwanza kutangaza timu ya kupanda kutoka kundi hilo.
    Baada ya matokeo ya mwisho ya kundi hilo, ukihusisha ushindi wa mvua ya mabao wa Geita Gold na Polisi Tabora, timu zote zinamaliza zikiwa zinalingana kwa kila kitu; kuanzia pointi 30 kila timu hadi tofauti ya mabao ambayo ni 15. 
    Maana yake ni kwamba kanuni nyingine ya michuano inabidi itazamwe ili kuamua timu ya kuungana na Lyon na Ruvu kupanda Ligi Kuu. Isipokuwa kabla ya kufika huko, TFF imeona ichunguze matokeo baada ya kuyatilia shaka.
    Binafsi, ninaunga mkono uamuzi wa TFF, wa kuchunguza kwanza matokeo ya michezo hiyo kabla ya kuyahalalisha, kisha kupiga hatua nyingine mbele katika kusaka timu ya kupanda Ligi Kuu.
    Lakini tu, bado sijaelewa TFF itatumia njia zipi kuchunguza zaidi kama hakukuwa na upangaji matokeo kwenye michezo hiyo, japokuwa suala hilo limepelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF.
    Ni dhahiri kwamba, suala la kupanga matokeo lazima lilianzia kwenye mawasiliano kwanza, baina ya wahusika kama viongozi wa timu, wachezaji na marefa ndiyo makubaliano yakafuatia kutekelezwa.
    TFF ilisema washukiwa mbalimbali watahojiwa na Kamati ya Nidhamu, ambayo situjui ina ujuzi au utaaalmu gani katika masuala kama hayo.
    Binafsi ninaamini, suala hilo si la kuishia Kamati ya Nidhamu pekee, bali Kamati hiyo ya TFF inapaswa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama vya taifa, kama Usalama wa Taifa, TAKUKURU na Idara ya Upepelezi ya Jeshi la Polisi.
    Vyombo hivi vitatu, ambavyo mara kadhaa hufanya kazi kwa ushirikiano, ninaamini vikishirikishwa vitatoka na majibu yasiyo na shaka kabisa juu ya hofu iliyopo sasa. Ni kwa sababu vina ujuzi wa hali ya juu kupambana na uhalifu wa aina hii. 
    Sitaki kuamini Kamati ya Nidhamu pekee kuita watu na kuwahoji tu itatoka na majibu ya kutuondoa hofu, la hasha – bali kwa kuzishirikishwa Usalama wa Taifa, TAKUKURU na Idara ya Upelelezi ya jeshi la Polisi.
    Vyombo vyote hivyo vipo kwa ajili ya masuala kama hayo na sioni ni kwa nini visiachiwe wajibu wake, ili mwisho wa siku tujue mbivu na mbichi kuhusiana na wasiwasi uliopo. 
    Nchi nyingi duniani zilizofanikiwa kiuchunguzi kung’amua michezo michafu ya aina hii katika soka yake, zilihusisha vyombo vya ulinzi na usalama.
    Soka ya Ufaransa ilichafuka kwa kashfa ya upangaji matokeo mwaka 1994, baada ya Rais wa klabu ya Olympique de Marseille, Bernard Tapie, kutuhumiwa kuhonga timu pinzani na matokeo yake timu yake ikashushwa daraja.
    Marseille ilivuliwa ubingwa wa msimu wa 1992/93 wa Ligi Kuu ya Ufaransa na kupokonywa tiketi za kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, UEFA Super Cup na Klabu Bingwa za Dunia baada ya kukutwa na kashfa ya kununua mechi.
    Marseille ilikutwa na hatia ya kuwahonga wachezaji watatu, Jacques Glassmann, Jorge Burruchaga na Christophe Robert wa Valenciennes FC, ili wacheze chini ya kiwango kuiacha timu hiyo ishinde kiulaini.
    Nyota hao watatu walipigiwa simu na mchezaji wa Marseille, Jean-Jacques Eydelie, wakiahidiwa fedha ili wacheze chini ya kiwango na pia wahakikishe hawachezi rafu ili wachezaji wa Marseille wasiumie, kwani walikuwa wanakabiliwa na mechi ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 1993.
    Kutokana na kashfa hiyo ya rushwa, Tapie, ambaye aliwahi kuwa Waziri katika serikali ya Ufaransa, alifungwa miaka miwili jela kwa kuhusika na makosa hayo.
    Soka ya Italia nayo ilitikiswa na kashfa ya upangaji matokeo mwaka 2006, ikizihusisha timu za Ligi Kuu (Serie A) na za Daraja la Kwanza (Serie B), ambazo ni Juventus, AC Milan, Fiorentina, Lazio na Reggina.
    Na zilinaswa kwa msaada wa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyofanikiwa kunasa mawasiliano ya simu kati ya viongozi wa timu hizo, makocha, wachezaji na marefa wakipanga mikakati ya kuhongana.
    Juventus walituhumiwa kuhonga fedha ili wapangiwe marefa wawatakao – na kutokana na makosa hayo, klabu hiyo ilishushwa daraja huku Fiorentina na Lazio, AC Millan na Reggina zikipokwa pointi na kupigwa faini.
    Mkurugenzi wa zamani wa Juventus, Luciano Moggi, alifunguliwa mashtaka ya makosa ya jinai kwa makosa ya rushwa na baadaye alihukumiwa kifungo cha miaka mitano na miezi minne jela.
    Mmiliki wa Fiorentina, Diego Della Valle na Rais wa Lazio, Claudio Lotito walihukumiwa kifungo cha miezi 15 jela na faini ya Euro 25,000 kila mmoja. 
    Mtendaji mkuu wa zamani wa AC Milan, Leonardo Meani alihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela, wakati Makamu wa Rais wa zamani wa Shirikisho la Soka la Italia, Innocenzo Mazzini alihukumiwa kifungo cha miezi 26 jela – na refa mstaafu Massimo De Santis alifungwa miezi 23 jela.
    Kwa Tanzania ajabu TFF imeshindwa kabisa kuviomba vyombo vya ulinzi na usalama kuingilia kati kashfa za upangaji matokeo, ambayo tafsiri yake ni rushwa, licha ya wakati fulani kuibuka wachezaji wakiwatuhumu baadhi ya viongozi kuwataka kuwahonga.
    Tangu awamu ya Leodegar Tenga, Rais alitemtangulia Jamal Malinzi TFF, tuhuma za wasiwasi juu ya rushwa kwenye soka ya Tanzania vimekuwa vikifanyiwa kazi kwa ujanja ujanja tu.
    Tusidanganyane, Kamati za TFF haziwezi kuibuka na majibu sahihi juu ya uhalifu wa aina hii – pasipo kuvishirikisha vyombo vya ulinzi na usalama vya taifa letu. 
    Na ninaposema majibu, haimaanishi yawe kweli matokeo yalipangwa – bali hata majibu tofauti yatatosha kumaliza wasiwasi uliopo.
    Miaka mitatu iliyopita, wasiwasi uliingia klabu ya Azam FC juu ya wachezaji wake wanne, kipa Deo Munishi ‘Dida’ ambaye sasa anachezea Yanga na mabeki Aggrey Morris, Erasto Nyoni na Said Mourad kuhongwa ili waihujumu hiyo.
    Lakini uongozi wa Azam FC, uliwasimamisha kwa muda wachezaji hao na kulikabidhi suala hilo TAKUKURU, ambayo mwishowe iliwasafisha wachezaji hao.
    Naam, sasa TFF ifuate taratibu nzuri kitaalamu na kisheria katika sakata la wasiwasi wa matokeo ya mechi za mwisho Kundi C Daraja la Kwanza. Jumapili njema. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VYOMBO VYA ULINZI NA USALAMA VIACHIWE SAKATA LA UPANGAJI MATOKEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top