• HABARI MPYA

    Saturday, February 20, 2016

    YANGA ‘WAJIHALALISHIA’ SIMBA SC, WAICHAPA 2-0 TAIFA, HII HAIJAWAHI KUTOKEA TANGU 1999

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imerejea kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuwachapa mabao 2-0 watani wao, Simba SC katika mchezo uliofanyika jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ushindi huo uliotokana na mabao ya Donald Dombo Ngoma kipindi cha kwanza na Amissi Joselyn Tambwe kipindi cha pili, unaifanya Yanga ifikishe pointi 46 baada ya kucheza mechi 19, wakati Simba SC iliyocheza mechi ya 20 leo, inabaki na pointi zake 45 na kushuka hadi nafasi ya tatu.
    Matokeo hayo yanaifanya Yanga SC ivune pointi sita msimu huu kwa watani, baada ya mechi ya mzunguko wa kwanza pia kushinda 2-0 Septemba 26, mwaka jana mabao ya Tambwe kipindi cha kwanza Malimi Busungu kipindi cha pili.
    Hii ni mara ya kwanza Yanga inaifunga Simba SC mechi zote za msimu za Ligi Kuu tangu mwaka 1999, msimu ambao Mtibwa Sugar waliibuka mabingwa.
    Donald Ngoma akishangilia baada ya kuifungia Yanga SC bao la kwanza Uwanja wa Taifa leo
    Amissi Tambwe akipambana na beki wa Simba SC, Juuko Murshid leo Uwanja wa Taifa

    Msimu wa 1999, wakati huo Ligi Kuu inadhaminiwa na bia ya Safari Lager inayotengenezwa na kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Yanga iliichapa Simba 3-1 Mei 1, 1999 mabao ya Idd Moshi, Kali Ongala na Salvatory Edward la wapinzani likifungwa na Juma Amir Maftah, wakati marudiano wana Jangwani wakashinda 2-0 Agosti 29, 1999 mabao ya Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ na Mohamed Hussein 'Mmachinga'.
    Katika mchezo wa leo, Simba SC ilipata pigo mapema tu dakika ya 24, baada ya beki wake wa kati, Abdi Banda kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na refa Jonesia Rukyaa wa Kagera kwa kumchezea rafu Ngoma.
    Mshambuliaji wa Zimbabwe, Ngoma akaifungia Yanga SC bao la kwanza dakika ya 39, akitumia makosa ya beki wa kulia wa Simba SC, Hassan Kessy aliyemrudishia pasi fupi kipa wake Vincent Angban raia wa Ivory Coast.
    Ngoma aliye katika msimu wake wa kwanza Yanga SC, baada ya kusajiliwa kutoka Platinum FC ya kwao, aliiwahi pasi ya Kessy kabla haijamfikia Angban na kumlamba chenga kipa kisha kufunga.
    Simba SC walitulia baada ya bao hilo na kucheza kwa tahadhari, wakiendelea kushambulia langoni mwa Yanga SC na kupata kona mfululizo, ambazo hawakuweza kuzitumia kupata bao.
    Kipindi cha pili, mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mganda, Jackson Mayanja kumtoa kiungo Mwinyi Kazimoto na kumuingiza beki Nova Lufunga, yaliidhoofisha safu ya kiungo ya timu hiyo na kuwafanya Yanga waanze kutawala mchezo.
    Krosi maridadi ya winga Godfrey Mwashiuya kutoka upande wa kushoto iliunganishwa nyavuni kwa guu la kulia na Mrundi Tambwe dakika ya 72 kuipatia Yanga SC bao la pili.
    Pamoja na kuwa nyuma kwa 2-0, Simba SC waliendelea kufikisha mipira kwenye eneo la hatari la Yanga, lakini hata hivyo leo safu yake ya ulinzi iliyoongozwa na Vincent Bossou na Mbuyu Twite ilikuwa makini.
    Vikosi vilikuwa;
    Yanga SC: Ally Mustafa ‘Barthez’, Juma Abdul, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Mwinyi Hajji Mngwali, Pato Ngonyani, Deus Kaseke/Godfrey Mwashiuya dk64, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Haruna Niyonzima/Simon Msuva dk52.
    Simba SC: Vincent Angban, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murushid, Abdi Banda, Justice Majabvi, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto/Novat Lufunga dk46, Hamisi Kiiza/Danny Lyanga dk59,Ibrahim Hajib/Brian Majwega dk80 na Said Ndemla.
    Mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, Azam FC imeichapa Mbeya City maabo 3-0 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, mabao ya Kipre Herman Tchetche, John Raphael Bocco na Farid Mussa.
    Azam FC inafikisha pointi 45 kwa ushindi huo, baada ya kucheza mechi 18 na kupanda hadi nafasi ya pili, ikiizidi Simba kwa wastani wa mabao.  
    Mechi nyingine; Mgambo JKT imetoa sare ya 1-1 na Prisons Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Stand United imetoka 1-1 na JKT Ruvu Uwanja wa Kambarage, Shinyanga na Toto Africans imelazimishwa sare ya 1-1 na Kagera Sugar Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA ‘WAJIHALALISHIA’ SIMBA SC, WAICHAPA 2-0 TAIFA, HII HAIJAWAHI KUTOKEA TANGU 1999 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top