• HABARI MPYA

  Wednesday, December 16, 2015

  KELVIN FRIDAY ATUA MTIBWA SUGAR KWA MKOPO, BRYSON APELEKWA NDANDA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Kevin Friday amejiunga na Mtibwa Sugar kwa mkopo. 
  Pamoja na Friday, Makamu Mwenyekiti wa Azam FC, Nassor Idrisa 'Father' amesema beki Ismail Gambo 'Kussi' amekwenda kwa mkopo Mwadui ya Shinyanga, kiungo Bryson Raphael amekwenda kwa mkopo Ndanda ya Mtwara, kiungo Omary Wayne ametua kwa mkopo Coastal Union ya Tanga.
  Akitolea ufafanuzi wa suala la Kelvin Friday kwenda Mtibwa, wakati anatakiwa kwenye majaribio katika timu ya St. Georges ya Ethiopia, Father alisema wameamua kufanya hivyo ili kuwahi muda wa usajili wa Tanzania uliofungwa jana na atakwenda huko mambo yakiwa yameshakamilika.
  Kelvin Friday ametua Mtibwa Sugar kwa mkopo kutoka Azam FC

  “Kipindi chake cha kwenda kwenye majaribio kipo mbele na dirisha letu la usajili limefungwa jana, tumempeleka huko ili aendelee kucheza wakati akisubiria mambo yake ya kwenda huko kukamilika bahati nzuri kocha aliyemuomba ni Mart Nooij, aliyewahi kuwa Kocha Taifa Stars,” alisema.
  Father aliongeza kuwa: “Tayari hivi sasa tumeshatuma pasipoti yake, nyaraka zake kwa ajili ya kumuombea viza, mambo yote hayo yakishakamilika atakwenda mara moja na akifaulu majaribio klabu zote mbili tutakaa chini na kukubaliana. Sisi tunaamini ya kuwa atafaulu na mambo mengine kuendelea.”
  Friday, 20, anatakiwa na mabingwa hao wa Ethiopia kwa majaribio ya muda wa wiki moja n tayari uongozi wa Azam FC umepokea kwa mikono miwili suala hilo na umempa baraka zote za kwenda huko mambo yakishakamilika.
  Pamoja na kuwatoa wachezaji hao kwa mkopo, Azam FC imemsajili kipa wa zamani wa Tukuyu Stars, Prisons za Mbeya, Moro United, African Lyon, Yanga, Simba za Dar es Salaam na St George ya Ethiopia, Ivo Mapunda.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KELVIN FRIDAY ATUA MTIBWA SUGAR KWA MKOPO, BRYSON APELEKWA NDANDA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top