• HABARI MPYA

    Wednesday, September 02, 2015

    YANGA SC WANA MATATIZO GANI, AU KUNA MTU ‘ANAJIPIGIA HELA’?

    KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) juzi imegawa vifaa vya michezo kwa klabu za Simba na Yanga SC kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara. 
    Ikumbukwe klabu hizo kongwe Tanzania, kwa pamoja zinadhaminiwa na TBL kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager kwa zaidi ya miaka mitano sasa.
    Katika vifaa hivyo walivyokabidhiwa kwenye hafla fupi iliyofanyika Dar es Salaam, Yanga SC walikabidhiwa aina mpya kabisa ya jezi ambazo hawakuzitumia misimu iliyopita.
    Simba SC walikabidhiwa jezi ambazo walilizizindua mwezi uliopita katika tamasha lao la kila mwaka, Simba Day Agosti 8, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

    Wakati wa uzinduzi wa jezi zake mpya, Simba SC iliingia Mkataba na kampuni pia kwa ajili ya kuuza jezi za mashabiki, ambazo zitakuwa sawa na jezi mpya za timu.
    Maana yake, Simba SC imefanikiwa kuua soko la jezi feki zilizokuwa zinauzwa kote nchini na kuwaelekeza mashabiki wake kwenye jezi halisi mpya za timu kwa msimu huu.
    Simba SC itafanikiwa kukusanya fedha kwa ajili ya mauzo ya jezi kwa msimu huu, baada ya muda mrefu wa kuwa hainufaiki na chochote kwa sababu jezi zilizokuwa zinauzwa zilikuwa feki.
    Sasa kiongozi wa Simba anaweza kumuonya shabiki wake asinunue jezi feki, kwa kuwa tayari jezi halisi zipo na zimetolewa na uongozi.
    Yanga SC wameendelea kushuhudia mashabiki wake wakivaa jezi feki na klabu ikiendelea kukosa mamilioni kutokana na mradi huo.
    Lakini kumbe wakati wote Simba SC wakifanya mkakati wa kuzindua jezi mpya hadi kuziingiza sokoni, Yanga SC nao walikuwa tayari wanajua jezi zao za msimu mpya ni zipi.
    Mwishoni mwa wiki kwenye mitandao ya kijamii, jezi mpya za Yanga SC zilivuja na juzi kweli ikadhihirika haswa ndizo zenyewe.
    Ajabu, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaanza wiki ijayo lakini hakuna mchakato wowote wa Yanga SC kutoa jezi maalum kwa mashabiki wake.
    Hivi kwa nini Yanga SC wanapuuza biashara hii ambayo inaziingizia fedha nyingi hadi klabu za Ulaya, au sasa tuanze kuhisi labda wapo viongozi ndani ya klabu wananufaika kwa njia za panya na mradi huo?
    Kwa sababu haiwezekani pamoja na kelele nyingi zinazopigwa  na vyombo habari uongozi wa Yanga SC umeendelea kuwa kimya kabisa tena kwa biashara ambayo maslahi yake yako wazi.
    Nembo ya Yanga SC ni lulu- kwa kuwa mabingwa wa Bara tu pekee ingewafanya wauze kwa wingi kila bidhaa yenye nembo yao.
    Lakini hakuna asiyefahamu kwamba hii ni klabu yenye wapenzi wengi zaidi nchini- kuliko mahasimu wao, Simba SC maana yake wana rasilimali watu nzuri mno, ambayo inasikitisha wanashindwa kuitumia.
    Ndiyo maana sasa leo mimi na wewe ndugu msomaji tujiulize, kuna matatizo gani pale Yanga SC, au kuna mtu anawazidi ujanja wenzake? Alamsiki.    
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WANA MATATIZO GANI, AU KUNA MTU ‘ANAJIPIGIA HELA’? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top