• HABARI MPYA

    Friday, September 25, 2015

    SIMBA SC WAIBUA UPYA KESI YA MESSI, HANS POPPE AWAPA TFF HADI OKTOBA VINGINEVYO MZIGO UNATUA FIFA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema kwamba Azam FC wasifikiri suala la Ramadhani Yahya Singano ‘Messi’ limeisha- kwani wanajipanga kwenda FIFA.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE leo mjini Dar es Salaam, Poppe amesema kwamba anastaajabishwa na ukimya wa TFF juu ya kutolea ufafanuzi Mkataba wa Messi wa Simba SC, wakati waliahidi kufanya hivyo.
    “Hili suala halijaisha na huko mbele ya safari litakuja kuwagharimu Azam FC. Maana TFF wakiendelea kulikalia kimya sisi tutakwenda FIFA kutafuta haki yetu na hiyo itakuwa mbaya sana kwa Azam FC, kwa sababu sisi tunajua na tuna uhakika na Mkataba wetu,”alisema Poppe.  
    Julai mwaka huu, TFF iliamua Messi ni mchezaji huru licha ya Simba SC kudai ina Mkataba naye na kumruhusu kujiunga na timu yoyote, naye akasaini Azam FC.
    Hans Poppe amesema TFF waakiendelea kukalia kimya suala la Mkataba wa Messi hadi Oktoba watapeleka kesi FIFA

    Baada ya kikao na pande zote mbili Julai, Kamati ya Sheria Maadili na Hadhi za Wachezaji ya TFF ilisema kwamba Simba SC walishindwa kutekeleza baadhi ya vipengele vya Mkataba, hivyo wanapoteza haki za kummiliki mchezaji huyo. 
    Chini ya Mwenyekiti wake, Richard Sinamtwa, Kamati hiyo ilijiridhisha Messi hakuwahi kupewa nyumba ya kuishi na Simba SC jambo ambalo ni kinyume cha Mkataba baina yake na klabu hiyo.
    Simba SC iliwakilishwa na Hans Poppe na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Collins Frisch wakati Messi alifika na Mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji Tanzania (SPUTANZA), Mussa Kisoky kwenye kikao hicho. 
    Messi aliyeibukia timu ya vijana ya Simba SC miaka minne iliyopita, hivi karibuni aliishutuma klabu yake hiyo iliyomuibua kisoka kwamba imeghushi Mkataba wake.
    Messi alidai Mkataba wake halali ulikuwa unamalizika mwaka huu, na si huu wa sasa ambao inaelezwa utamalizika mwakani.
    Lakini Simba SC imeendelea kusistiza mchezaji huyo alikuwa ana Mkataba wa miaka mitatu.
    Awali, Sekretarieti ya TFF, chini ya Katibu wake, Selestine Mwesigwa ilizikutanisha pande zote mbili, mchezaji na Simba SC na kuamuru waketi chini na kutayarisha Mkataba mpya baada ya kuona huu wa sasa una mushkeli.
    Hata hivyo, Messi akakataa na kuamua kulihamishaia suala hilo Kamati ya Sheria ambayo mwishowe imempa kile alichotaka ‘kuwa mchezaji huru’.
    Messi (kulia) akikabidhiwa jezi ya Azam FC baada ya kusaini Mkataba

    “Tuliwasilisha ushahidi wote mbele ya Kamati, tumeonyesha mshahara wake ulikuwa kiasi gani na tumeonyesha kwa nini alikuwa anapewa laki moja (100,000) zaidi mwezi.
    Ni ili akalipie kodi ya nyumba, lakini bado hatukueleweka. Baadaye TFF ilisema itatolea ufafanuzi suala la Mkataba kama ni feki au halali, lakini nashangaa wamekaa kimya hadi leo. Sasa kama itafika Oktoba mwishoni bado wako kimya, sisi tutakwenda FIFA,”amesema Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
    Poppe amewatahadharisha Azam FC na TFF kwamba suala hilo likifika FIFA litakuwa zito na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya klabu na mchezaji.
    “TP Mazembe imewahi kupokonywa ushindi katika Ligi ya Mabingwa wa Afrika baada ya kututoa sisi kwa sababu ya kutumia mchezaji mwenye Mkataba na timu nyingine kama Messi.
    Watu wanakumbuka hapa, sisi tulirudi kwenye mashindano baada ya Mazembe kuondolewa na yule mchezaji akafungiwa, sasa wao wafanye dharau tu, lakini wajue sisi tutakwenda popote kufuata haki yetu,”amesema.
    Mwaka 2011 TP Mazembe ya DRC iiitoa Simba SC kwa jumla ya mabao 6-3 baada ya kuifunga 3-1 Lubumbashi na 3-2 Dar es Salaam katika hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa, lakini Wekundu wa Msimbazi wakarudishwa mashindanoni baada ya kushinda rufaa waliyomkatia beki wa Mazembe, Janvier Besala Bokungu, aliyevunja mkataba kinyume cha taratibu na klabu ya Esperance ya Tunisia.
    Simba SC ikacheza mechi ya mkondo mmoja na Wydad Casablanca ya Morocco mjini Cairo, Misri na kufungwa 3-0, hivyo kuangukia kwenye hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho Afrika, ambako ilitolewa na DC Motema Pembe ya DRC kwa mabao 2-1.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC WAIBUA UPYA KESI YA MESSI, HANS POPPE AWAPA TFF HADI OKTOBA VINGINEVYO MZIGO UNATUA FIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top