• HABARI MPYA

    Wednesday, September 30, 2015

    NI ADHABU KUBWA, LAKINI NYOSSO AMEVUNA MATUNDA YA UFEDHULI WAKE

    APRILI 21, mwaka 2007 mchezo kati ya Simba SC na Ashanti United wa Ligi Ndogo kuelekea mfumo mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ulivunjika kipindi cha kwanza.
    Mchezo huo ulivunjika dakika ya 42 kipindi cha kwanza, baada ya mashabiki wa Simba SC kuvamia uwanjani kufanya fujo.
    Chanzo cha vurugu hizo ni aliyekuwa beki wa Ashanti United, Juma Said Nyosso kumtia dole nyuma aliyekuwa mshambuliaji wa Simba SC, Joseph Kaniki ‘Golota’.
    Kaniki naye mtoto wa mjini, Mwananyamala, Dar es Salaam- hakukubali kudhalilishwa namna ile, akampiga Nyosso. 

    Refa akamtoa kwa kadi nyekundu Kaniki na mashabiki wa Simba SC hawakuweza kuvumilia, wakavamia uwanjani kutaka kuwapiga wachezaji wa Ashanti. Polisi wakaingia kutawanya mashabiki kwa mabomu ya machozi. Mchezo ukaishia hapo.
    Wakati huo, mechi za Ligi Kuu hazionyeshwi moja kwa moja kwenye Televisheni na hakuna kamera iliyonasa tukio la Nyosso kumdhalilisha Kaniki. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likaipa ushindi Ashanti United na Kaniki akafungiwa.
    Dhuluma mbaya iliyomuumiza Kaniki na tangu hapo hakupenda kuendelea kucheza Tanzania, akaondoka zake na hadi leo yuko Ulaya.
    Aprili 18, mwaka 2010, aliyekuwa beki wa Yanga SC, Amir Maftah alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kichwa beki wa Simba SC wakati huo, Juma Said Nyosso. 
    Maftah alifanya hivyo baada ya kutiwa dole nyuma na Nyosso. Bahati nzuri katika Uwanja mkubwa na usalama wa hali ya juu, hakuna vurugu zilizotokea Yanga SC ikifungwa 4-3.
    Yanga SC ilimuacha Maftah baada ya msimu kwa kitendo cha kumpiga kichwa Nyosso na kutolewa kwa kadi nyekundu kiasi cha kuiachia pengo timu hadi ikafungwa.
    Maftah mtoto wa Rwegasore, Mwanza mjini alishindwa kuvumilia udhalilishwaji- akamtandika kichwa Nyosso, lakini Yanga SC wakadhani alifanya vile kuhujumu timu.
    Nyosso akaathiri maisha ya mchezaji mwingine- Maftah ambaye bahati nzuri alisajiliwa Simba SC msimu uliofuata kwa kifua cha mjomba wake, Ibrahim Masoud ‘Maesteo’ aliyekuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu wakati huo.
    Januari 28, mwaka huu (2015), Juma Nyosso tena alinaswa na kamera akimtia dole nyuma aliyekuwa mshambuliaji wa Simba SC, Elias Maguri katika mchezo ambao Wekundu wa Msimbazi walifungwa 2-1 na Mbeya City Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Siku zilizofuata picha ya Nyosso anamtia dole Maguri ilitokea kwenye kurasa magazeti ya michezo nchini na ukawa mjadala mkubwa.
    Kwa mara ya kwanza, Nyosso akaadhibiwa kwa tabia hiyo, akifungiwa mechi nane za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Cha kustaajabisha, Mbeya City haikutoa tamko lolote kulaani tabia ya mchezaji wake- na iliendelea kumhudumia vizuri hadi akamaliza adhabu yake na kurudi kazini.
    Lakini wengi waliamini kwa adhabu ile Nyosso hatarudia. Tuliomtarajia Nyosso mpya, atakayeanza kucheza kwa uadilifu- kumbe tulijidanganya mno.
    Jumapili ya Septemba 27, mwaka huu (2015), kamera ya BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE (mtandao nambari moja wa habari za michezo, hususan soka Tanzania) ilimnasa vizuri Nyosso akimtia dole Nahodha wa Azam FC na Taifa Stars (wakati fulani), John Raphael Bocco dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Tukio hilo lilitokea kipindi cha kwanza katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Nyosso alitumia mwanya wa refa Martin Saanya kutatua mgogoro baina ya wachezaji wa timu hizo kwa kumtomasa mwenzake nyuma.
    Bocco alionyesha utulivu na ustaarabu wa hali ya juu licha ya kuonyesha dalili zote za kukasirishwa na kitendo hicho, kwani alimfuata refa Martin Saanya kuwasilisha malalamiko yake.
    Saanya hakuonekana kuyatilia mkazo malalamiko ya Bocco, ambaye alipandisha hasira na kutaka kumpiga Nyosso kama si refa huyo kuwatenganisha.
    Benchi la Ufundi la Azam FC lilipeleka ushahidi wa picha kwa refa wa akiba, Soud Lila wa Dar es Salaam pia, ambaye alitoa maelekezo picha hizo zipelekwe kwa Ofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Iddi Mshangama.
    Tukio hilo lilionekana kabisa kumnyima raha Bocco na kushindwa kucheza katika kiwango chake kuanzia hapo, ingawa Azam FC ilifanikiwa kushinda 2-1.
    Haya ni matukio manne, matukio mawili ya awali wachezaji wenzake walimpiga, lakini baada ya Kaniki na Maftah kufungiwa, wengine wameogopa kumpiga.
    Maguri hadi leo anaumia na nafsi yake namna alivyodhalilishwa na Nyosso- na sasa Bocco naye ana kinyongo na beki huyo wa Mbeya City aliyepita Ashanti, Simba SC na Coastal Union.
    Maguri na Bocco wameheshimu sheria za soka- hawakujibu mapigo kwa Nyosso, lakini haimaanishi hawajaumizwa na alichowafanyia na kati yetu mimi na wewe msomaji hatujui hisia za wachezaji hao zikoje.  
    Na jana TFF, imemfungia miaka miwili na kumtoza fainai ya Sh. Milioni 2 Nyosso baada ya ushahidi wa picha kumuonyesha akifanya udhalilishaji huo.
    Ni adhabu kubwa, kuliko waliyowahi kuchukuliwa wachezaji wengine nap engine ipo nje ya kanuni za adhabu za mashindano nchini. Adhabu ambayo wengi wataifurahia, kwa sababu wamemchoka Nyosso na matukio yake.
    Katika mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Mataifa ya Kusini mwa Amerika, Copa America beki  Gonzalo Jara wa Chile, alimtia dole mshambuliaji wa Uruguay, Edinson Cavani ambaye alijibu kwa kumzaba kibao usoni.
    Cavani akaonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa kwa kadi nyekundu na Jara baadaye akafungiwa kutocheza mechi mbili zilizosalia za Copa America ya mwaka huu, ambayo Chile walishinda. Klabu yake, Mainz ya Ujerumani ililaani vikali kitendo hicho na ikaona haiwezi kuendelea kuwa na mchezaji huyo, ikatangaza kumuuza- na kwa bahati mbaya hadi sasa hakuna timu iliyojitokeza kutaka kumnunua.
    Adhabu aliyopewa ni Nyosso ni kubwa, lakini haifikii ‘majeraha’ aliyowasababishia wenzake kwa udhalilishaji aliowafanyia. Watu wamekasirika na walitaka Nyosso afungiwe maisha. 
    Naamini, adhabu kubwa tunayoitaka itatolewa na Mbeya City na baadaye kuungwa mkono na klabu zote nchini. Mbeya City imuache Nyosso na klabu nyingine yoyote isiwe tayari kumsajili hata bure.
    Adhabu ambayo imewahi kutolewa na Simba SC, ilipoamua kumuacha mchezaji huyo akiwa katika ubora wake miaka mitatu iliyopita tu kwa sababu ya kuchoshwa na tabia zake zisizo za kiungwana na kiuanamichezo.
    Adhabu kama ambayo Mainz wamempa Jara na kuungwa mkono na mawakala ambao hawajisumbui kumtafutia timu mchezaji huyo wa kimataifa wa Chile.
    Huwezi kufikiria Nyosso ataishije kwa adhabu hii, ikiwa soka ndiyo ajira yake- ikiwa yeye hakufikiria machungu ya dhalili aliyokuwa anawafanyia wenzake. Na tuseme amevuna matunda ya ufedhuli wake.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NI ADHABU KUBWA, LAKINI NYOSSO AMEVUNA MATUNDA YA UFEDHULI WAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top