• HABARI MPYA

    Wednesday, September 23, 2015

    SOKA YA TANZANIA ILIMUHITAJI MALINZI, KAMA AMBAVYO SIMBA NA YANGA...

    NIANZE kwa kusema namshukuru Mungu kwa kunijaalia upeo na maono- maana unaweza ukawa na elimu kubwa, lakini ukakosa kipawa hicho.
    Mara nyingi sana nimekuwa na maono sahihi kiasi cha kuweza kutoa mwongozo mzuri katika kusaidia maendeleo ya soka ya nchi hii.
    Wakati ule napendekeza na kushawishi Jamal Malinzi achaguliwe kuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), nilijua ni mtu ambaye takuja kuleta manufaa katika soka yetu. 
    Leo hii hata kabla ya kutimiza miaka miwili madarakani, tumeona matunda ya Malinzi katika soka yetu. Mkataba wa udhamini wa timu ya taifa, Taifa Stars na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) umeboreshwa.
    Mkataba wa udhamini wa LIgi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara umeboreshwa. Mkataba wa haki za matangazo ya Televisheni wa Azam TV umeboreshwa. Bodi ya Ligi imeboreshwa kwa kuondolewa viongozi ambao hawakuweza kufanya kazi kwa ufanisi na kuwekwa wapya, ingawa bado kuna changamoto ndogondogo zinazofanyiwa kazi.
    Kombe la FA limerudi, tena kwa mara ya kwanza likiwa na udhamini mnono wa Azam TV. Ligi Daraja la Kwanza kwa mara ya kwanza itakuwa na udhamini.
    Kombe la Taifa la wanawake limeanza. Michuano ya vijana ya Copa Coca Cola na Airtel Rising Stars imeboreshwa. Mpango mkakati wa kuunda timu bora ya taifa ya baadaye umeanza kwa kuanzia kuendesha mashindano ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 12, ambao sasa wamewekwa katika shule ya Alliance Academy mjini Mwanza kuendelezwa kisoka na elimu.
    Wakati huo huo kuna timu ya vijana chini ya umri wa miaka 15 inaandaliwa ili miaka miwili ijayo tuwe U17 bora ya ushindani na tayari TFF imeomba uenyeji wa Mashindano ya Afrika ya U17 mwaka 2019.
    Ligi Kuu ya wanawake itaanza mwakani. Ni mengi mazuri Malinzi ameyafanya katika kipindi kifupi tu na kama mambo yatakwenda vizuri, soka ya nchi italeta starehe miaka ijayo.
    Bado kuna changamoto kadhaa Malinzi anatakiwa kupambana nazo na kubwa zaidi ni kuhakikisha kasi na uadilifu wake vinaendana na watendaji aliowaajiri pale TFF, vinginevyo watakuja kumtia doa mbele ya safari.
    Wakati nikimpongeza Malinzi juu ya hayo mengi mazuri, nachukua fursa hii pia kumkumbusha kwamba Tanzania ina wapenzi wawili tu wa soka, mmoja Simba na mwingine Yanga SC.
    Na mpenzi yeyote wa soka nchini, lazima atakuwa anapenda ama Simba, au Yanga SC. Katika hilo tusidanganyane.
    Viongozi wa vyama vya soka kuanzia wilaya, mikoa hadi taifa- wengine Simba na wengine Yanga SC. Viongozi wa klabu nyingine pia, nao wapo wenye mapenzi ya Simba, wengine Yanga SC.
    Waandishi wa Habari za soka, pia tupo kwenye mkumbo huo na ndiyo maana Ezekiel Kamwaga alikuwa Ofisa Habari wa Simba SC na Jerry Muro ni wa Yanga SC.
    Watangazaji wa Redio na Televisheni kadhalika, wapo Simba na Yanga na ndiyo maana Mshindo Mkeyenge alikuwa Katibu Mwenezi wa Yanga SC, na Juma Nkamia alikuwa wa Simba SC. Hata marefa na makocha, nao wana mapenzi na moja ya hizi klabu.
    Baada ya kuwa mpenzi wa Simba, au Yanga na ukiwa na dhamana katika soka ya nchi hii kinachotazamwa ni uadilifu wako katika utendaji. Hauleti upendeleo kwa shinikizo la mapenzi?
    Kama wewe ni Mwandishi wa Habari, je, hauleti mapenzi yako katika uandishi wako, jambo ambalo ni kinyume na maadili ya taaluma?
    Vile vile kwa marefa, je katika uchezeshaji wao hawaingizi mapenzi yao?
    Kwa asilimia kubwa Watanzania tumeshindwa kujidhibiti kwenye suala la Usimba na Uyanga na ndiyo maana nimekuwa nikirudia kuandika, mechi ya mahasimu hao wa jadi, umefika wakati sasa ihamishiwe kwa marefa wa kigeni.
    Na kufanya hivyo kutaiongezea thamani yake na kujenga imani pia ya haki- tuwaache wenyewe baada ya mechi wafungie wachezaji wao kwa tuhuma za kuhujumu.  
    Miaka minne iliyopita, wachambuzi waliobobea wa Televisheni ya kulipia ya kimataifa SuperSport ya Afrika Kusini, waliwahi kuiingiza mechi ya Simba na Yanga katika orodha ya mechi tatu kali za wapinzani wa jadi Afrika - nyingine zikiwa ni kati ya Orlando Pirates na Kaizer Chiefs za Afrika Kusini na Al Ahly dhidi ya Zamalek za Misri.
    Hakuna ubishi kwamba upinzani wa Ahly na Zamalek huo ni dunia nzima - ni zaidi ya upinzani, lakini kwa Afrika fuatilia ligi nyingi, utagundua Simba na Yanga ni mechi yenye mvuto wa kipekee na ndiyo maana SuperSport walikuwa wanakuja kuionyesha ‘Live’ kabla ya Azam TV kununu haki za matangazo ya Ligi Kuu.
    Unaweza kutilia shaka kiwango cha soka cha timu hizo, lakini si upinzani wao kwa maana ya upinzani na hamasa za kishabiki. Watu wanazimia na wengine kufa, kujiua kwa sababu ya Simba na Yanga.
    Upinzani wao ni sehemu ya burudani na kama iko siku zitakuwa timu imara na kucheza soka ya kuvutia, basi burudani itakuwa mara mbili.
    Hata hivyo, kuna mambo mawili au matatu ambayo kwa kiasi fulani yamekuwa yakipunguza ladha ya mechi za watani hao wa jadi.
    Awali tatizo kubwa lilikuwa Uwanja mdogo wa Uhuru, lakini tangu kukamilika kwa Uwanja wa Taifa ambao tumeshuhudia mechi zote zilizochezwa hapo, haijatokea mechi hata moja mashabiki wakajaza viti, mambo yamekuwa mazuri.
    Matatizo mawili yaliyobakia ni viwango vya timu kuboreshwa, ili ifike wakati pamoja na upinzani, kukamiana lakini watazamaji washuhudie soka safi.
    Tatizo la pili ni marefa, kweli ilipofikia na kama kweli lengo ni kuiongezea msisimko zaidi mechi ya watani, waamuzi wa Tanzania wawekwe kando na watumike waamuzi kutoka nje ya nchi, tena ikibidi nje kabisa ya nchi tatu za Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki.
    Rejea mchezo wa Machi 5, mwaka 2011 Uwanja wa Taifa, refa Orden Mbaga aliivuruga mno mechi hiyo, kutokana tu na pengine mchecheto ama kutaka kufanya kile ambacho kinaitwa ‘kubalansi’ mchezo au kukwepa lawama, matokeo yake akafanya madudu.
    Dakika ya 58 Juma Said Nyosso alimkwatua Mzambia Davies Robby Mwape kwenye eneo la hatari akawapa penalti Yanga na kilichofuatia wengi walijua beki huyo wa Simba atatolewa nje kwa kadi nyekundu, badala yake akampa kadi ya njano.
    Ngumu kuamini Mbaga, refa mwenye beji ya Shrikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) hajui alipaswa kufanya nini kwa Nyosso, lakini kwa sababu ni refa wa nyumbani na aliongoza wapinzani wa jadi katika mechi ya nyumbani, alihofia kumtoa mchezaji kwa kadi nyekundu angeshushiwa lawama nzito. Marefa hufanyiwa fujo na kupigwa na mashabiki, labda alihofia hali hiyo pia.
    Dakika ya 73 Simba walipata bao safi la kusawazisha lililofungwa kwa kichwa na Mussa Hassan Mgosi, aliyeuwahi mpira uliotemwa na kipa Mghana Yaw Berko kufuatia shuti la mpira wa adhabu, lililogonga mwamba wa juu na kudondokea nyavuni kabla ya kuokolewa na mabeki wa Yanga.
    Halikuwa bao lenye shaka yoyote, hakukuwa na kuotea wala dosari yoyote, lakini haieleweki kwa nini Mbaga alilikataa bao hilo awali.
    Ilikuwa offside au mpira haukutinga nyavuni hadi akalikataa kwanza? Haijulikani, lakini alilikubali baada ya wachezaji wa Simba kumuambia aangalie kwenye TV kubwa iliyopo uwanjani marudio ya tukio lile na baada ya hapo akaenda kujadiliana na msaidizi wake, ndipo akalikubali.
    Tujiulize, kusingekuwa na ile TV, Simba wangedhulumiwa bao lao?
    Mbaga alichemsha- lakini si Mbaga tu, marefa wengi wa Tanzania waliwahi kutokota kabla yake na nitakumbushia baadhi ya mechi.   
    Machi 31, mwaka 2002 katika fainali ya Kombe la Tusker, Simba ikishinda 4-1, refa Abdulkadir Omar ‘Msomali’ aliivuruga mechi na kuvuruga amani uwanjani pia kwa madudu yake.
    Kwa nini? Katika mechi hiyo ya fainali iliyohudhuriwa na rais mstaafu wa awamu ya pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, chupuchupu ivunjike dakika ya 32, baada ya Madaraka Suleiman kufunga bao ambalo kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Manyika Peter, aliushika mpira kwa makusudi, ili kuuweka sawa. 
    Rais wa Yanga wakati huo, Tarimba Abbas aliinuka na kuwaonyesha ishara wachezaji wake watoke uwanjani na hapo ndipo meza kuu aliyokuwa ameketi mzee Mwinyi, ilipoanza kushambuliwa kwa chupa za maji na mashabiki wa Yanga. Abdulkadir Omar alisubiri hadi vurugu zilipotulizwa na FFU ndipo akaendeleza mchezo. Tarimba alitoka nje na hakutaka kuendelea kushuhudia mchezo huo. Baada ya hapo, alifungiwa na Chama cha Soka Tanzania, (FAT), sasa TFF kabla ya kujiuzulu uongozi wa klabu hiyo baadaye.
    Agosti 18, mwaka 2002 Simba na Yanga zikitoka sare ya 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu, refa Victor Mwandike aliwaacha mashabiki wa Simba midomo wazi kwa kuwapa Yanga penalti ya utata dakika ya 89 na ushei, ambayo Sekilojo Chambua aliitumia vema kuisawazishia bao timu yake, baada ya Simba kutangulia kufunga kupitia kwa Madaraka Suleiman dakika ya 65.
    Oktoba 24, mwaka 2007, refa Osman Kazi alikataa mabao matatu yaliyofungwa na Yanga, yote akidai kipa Juma Kaseja alisukumwa na wachezaji wa Yanga, lakini kwa yeyote atakayerudia kuangalia DVD ya mchezo ule, hawezi kuona ukweli wa madai ya Kazi.
    Awali ya hapo, Kazi aliwahi kupuliza filimbi ya kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza katika Nusu Fainali ya Kombe la Tusker mwaka 2005 mjini Mwanza, wakati mchezaji wa Yanga, Said Maulid ‘SMG’ amekwishawatoka mabeki wa Simba na anakwenda na mpira mbele yake amebaki Juma Kaseja tu.
    Refa ni mwamuzi wa mwisho- lakini kwa wana Yanga walijutia mno tukio lile kwenye mchezo ambao mwishowe walifungwa 2-0, kwa mabao ya kipindi cha pili ya Emmanuel Gabriel na Mussa Mgosi.
    Aprili 19, mwaka 2009, Jerry Tegete aliifungia Yanga bao la kusawazisha kwa mkono na kutengeneza sare ya 2-2, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Refa makini asingeweza kukubali bao lile, hivyo kwa haya yote lazima tukubali marefa wa Tanzania hawawezi tena kuchezesha mechi za watani wa jadi.
    Sababu nyingine za marefa wetu kuzishindwa mechi hizo ni hiyo ya mapenzi yao kwa moja ya timu hizo, kitu ambacho Misri wamekiepuka na mechi ya Zamalek na Ahly inachezeshwa na marefa kutoka nje ya nchi yao.
    Nakumbuka refa kutoka Uganda, Dennis Bate aliyechezesha fainali ya mwisho ya Kombe la Tusker mwaka 2009 kati ya Simba na Yanga, aliiongoza vizuri mechi hiyo na akadhibiti ujanja wote wa wachezaji kutaka kumdanganya na hatimaye aboronge.
    Kuna wachezaji wanaitwa wazoefu wa mechi za Simba na Yanga na hawa wamekuwa wakiwapoteza sana marefa kwa uzoefu wa kucheza mechi hizo, lakini kama marefa watatoka nje ya Tanzania, tena wa kiwango cha beji za FIFA, uhondo wa mechi za watani utaongezeka maradufu. Ila kwa sasa, marefa wetu hawaziwezi tena mechi hizi.   
    Wakati Jumamosi wiki hii miamba hao wanakutana katika mechi ya mzunguko wa kwanza ya Ligi Kuu msimu huu, nawashauri TFF na Bodi ya Ligi Kuu-wakati umefika sasa waache kuweka nta kwenye masikio yao na wakubali kuanza kutumia marefa wa kigeni.
    Jitihada za Malinzi katika kuleta mabadiliko kwenye soka ya Tanzania zinaonekana- lakini kuna mambo mengine asiyachukulie kama madogo, mfano hili la marefa wetu kuchezesha mechi watani. Asante kwa kusoma.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SOKA YA TANZANIA ILIMUHITAJI MALINZI, KAMA AMBAVYO SIMBA NA YANGA... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top