• HABARI MPYA

    Saturday, September 26, 2015

    MOTO WAWAKA AFRIKA, MAZEMBE NA MERREIKH LEO KHAROTUM, ETOILE NA ZAMALEK KESHO

    NUSU FAINALI MICHUANO YA KLABU AFRIKA
    Ligi ya Mabingwa
    Leo; El Merreikh (Sudan) Vs TP Mazembe (DRC)
    Kesho; El Hilal (Sudan) Vs USM Alger (Algeria)
    Kombe la Shirikisho
    Leo; Orlando Pirates (A.Kusini) Vs Al Ahly (Misri)
    Kesho; ES Sahel (Tunisia) Vs Zamalek (Misri)
    Kikosi cha TP Mazembe leo kitamenyana na Merreikh mjini Khartoum

    Na Mwandishi Wetu, KHARTOUM
    AFRIKA inawaka moto wikiendi hii kwa mechi za Nusu Fainali za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.
    Washambuliaji nyota wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu wataiongoza Tout Puissant Mazembe katika mchezo wa ugenini leo dhidi ya El Merreikh nchini Sudan.
    Nusu Fainali hiyo ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa itafanyika Uwanja wa Merreikh mjini Khartoum kuanzia Saa 3:00 usiku na Mazembe wamekuwa mjini humo kwa wiki nzima ili kuzoea hali ya joto la Sudan.
    Mabingwa mara nne wa Afrika, Mazembe walifika Nusu Fainali baada ya kuongoza Kundi A, wakati mahasimu wao, Merreikh walimaliza nafasi ya pili katika Kundi B nyuma ya USM Alger ya Algeria.
    Mazembe iliyofungwa bao moja tu katika hatua yote ya makundi, itapigania matokeo mazuri leo ugenini kabla ya kurejea nyumbani Lubumbashi kumaliza kazi.
    “Tumekuwa wenye bahati kuanzia ugenini Sudan kabla ya kucheza nyumbani mchezo wa pili,” amesema Kocha Mkuu wa Mazembe, Patrice Carteron.

    Mshambuliaji wa Azam FC, Kipre Tchetche akimtoka beki wa El Merreikh katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam. Merreikh ilifungwa 2-0 na kwenda kushinda 3-0 Khartoum hivyo kusonga mbele

    “Kuna vitu fulani vya kuvutia katika Uwanja wa Mazembe wakati TPM wanacheza. Huwezi kuchukulia kama ni mambo ya soka tu, unaweza kuhisi Uwanja huu una moyo,”amesema.
    Mchezo wa leo utamkutanisha kocha wa Merreikh, Diego Garzitto na na vigogo wa DRC, ambao aliwaongoza kwa mafanikio mwaka 2009.
    “Nilifundisha Tout-Puissant mara mbili, mwaka 2004 na 2009, na tulishinda taji la Ligi ya Mabingwa mwaka 2009 kabla ya kushiriki Klabu Bingwa ya Dunia,” amesema Garzitto.
    “Ni klabu ambayo naijua vizuri, na ninatarajia kukutana na marafiki Septemba 26, na hususan Oktoba 2 mjini Lubumbashi. Ni wapinzani bora,” ameongeza.
    El Merreikh haijaruhusu nyavu zake kuguswa ndani ya ardhi ya Khartoum tangu mwanzo wa hatua ya makundi, na watapenda kuendelea kuweka rekodi hiyo nzuri kabla ya kwenda Lubumbashi.
    Hii ni mara ya pili miamba hiyo inakutana katika mtoano wa michuano ya Afrika, mara ya kwanza ikiwa mwaka 2012 Mazembe ilipofuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1 baada ya kutoa sare ya 1-1 na El Merreikh mjini Khartoum na kushinda 2-0 nyumbani.

    Etoile du Sahel iliiitoa Yanga SC ya Tanzania katika hatua ya 16 Bora kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya sare ya 1-1 Dar es Salaam na ushindi wa 1-0 Tunisia

    Nusu Fainali nyingine ya Ligi ya Mabingwa inafanyika kesho El Hilal ya Sudan ikiikaribisha USM Alger ya Algeria Uwanja wa El Hilal.
    Aidha, Orlando Pirates ya Afrika Kusini leo itawakaribisha Al Ahly ya Misri katika Nusu Fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho, wakati kesho Etoile du Sahel ya Tunisia itaikaribisha Zamalek ya Misri.
    Ikumbukwe, Merreikh ilianza safari yake kwa kuitoa kwa mbinde Azam FC ya Tanzania kwa ushindi wa jumla wa 3-2, ikifungwa 2-0 Dar es Salaam kabla ya kushinda 3-0 Khartoum katika Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa. 
    Etoile nayo iliitoa Yanga SC ya Tanzania kwa mbinde hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho kwa jumla ya mabao 2-1, baada ya sare ya 1-1 Dar es Salaam na ushindi wa 1-0 mjini Sousse.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MOTO WAWAKA AFRIKA, MAZEMBE NA MERREIKH LEO KHAROTUM, ETOILE NA ZAMALEK KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top