• HABARI MPYA

    Wednesday, September 30, 2015

    WA MKOPO AING’ARISHA SIIMBA SC, YAICHAPA 1-0 STAND UNITED TAIFA

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imepoza machungu ya kipigo cha 2-0 watani, Yanga SC mwishoni mwa wiki, baada ya jioni ya leo kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Stand United katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Ahmada Simba wa Kagera, timu hizo zilishambuliana kwa zamu huku Hassan Dilunga wa Stand United akionyeshana ufundi na kiungo wa Simba SC, Said Ndemla katikati ya Uwanja kipindi cha kwanza.   
    Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Muingereza Dylan Kerr kipindi cha pili kupunguza idadi ya viungo wa kati na kuongeza kiungo mshambuliaji, ndiyo yaliongeza makali ya Simba SC hadi kupata bao.
    Joseph Kimwaga akishangilia baada ya kuifungia bao pekee Simba SC leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam

    Kerr alimtoa Ndemla na kumuingiza Joseph Kimwaga mwanzoni mwa kipindi cha pili na ni mchezaji huyo wa mkopo kutoka Azam FC ndiye aliyekwenda kuipatia bao hilo pekee Simba SC dakika ya 57 kwa shuti kali akimalizia krosi ya Mganda, Simon Sserunkuma.
    Awali, safu ya ushambuliaji ya Simba SC iliyomtegemea Boniface Maganga pekee haikuwa tishio kutokana na Kerr kuanzisha viungo wengi, Justice Majabvi, Jonas Mkude, Pater Mwalyanzi na Ndemla.

    Beki wa Stand United, Nassor Said 'Chollo' akimdhibiti kiungo wa Simba SC, Justice Majabvi ili kipa wake, Frank Muwonge adake mpira
    Mshambuliaji wa SImba SC, Mganda SImon Sserunkuma akimtoka beki wa Stand United, Abuu Ubwa
    Beki wa Simba SC, Hassan Kessy akigombea mpira na beki wa Stand United, Abuu Ubwa
    Beki wa Simba SC, Juuko Murshid akipasua katikati ya wachezaji wa Stand United, Rajab Zahir (kulia) na Erick Kayombo
    Na Simba SC inatimiza pointi 12 baada ya mechi tano, ikiendelea kuwa nyuma ya Yanga SC na Azam FC ambao wameshinda kwa mara ya tano mfululizo tangu kuanza kwa Ligi Kuu Septemba 12. 
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Peter Manyika, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Hassan Isihaka, Jonas Mkude, Justice Matabvi, Said Ndemla/Joseph Kimwaga dk46, Peter Mwalyanzi, Simon Sserunkuma na Boniface Maganga.
    Stand United; Frank Muwonge, Nassoro Said ‘Chollo’, Abuu Ubwa, Philip Imetusela, Rajab Zahir, Hassan Dilunga, Jacob Massawe, Erick Kayombo, Vitalis Mayanja/Hassan Banda dk43, Suleiman Kassim ‘Selembe’/Haroun Chanongo dk60 na Pastory Athanas.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WA MKOPO AING’ARISHA SIIMBA SC, YAICHAPA 1-0 STAND UNITED TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top